Dar
es Salaam. Rais Jakaya Kikwete amekemea vikali vurugu zilizotokea jana
mkoani Mtwara baada ya kusomwa bungeni kwa Bajeti ya Wizara ya Nishati
na Madini.
Akizungumza
katika eneo la Kizota, Dodoma wakati wa kuweka jiwe la msingi la ujenzi
wa Barabara ya Dodoma kwenda Iringa, Rais Kikwete alisema wote
waliohusika na vurugu hizo watasakwa na kuchukuliwa hatua kali.
Rais
Kikwete alisema rasilimali inayopatikana mahali popote pale nchini
inatakiwa kutumiwa na Watanzania wote... “Hivi watu wa Nyarugusu wadai
dhahabu ya pale au kinachopatikana Chalinze basi kisitumiwe na watu wa
Morogoro! Hivi tutakuwa na taifa kweli?,” alihoji kwa ukali Rais
Kikwete.
Rais
Kikwete alisisitiza kuwa Serikali itawasaka wale wote wanaoongoza vurugu
hizo na watawajibishwa kwa makosa hayo... “Tutawasaka hawa watu na
viongozi wao hata kama wana mapembe kiasi gani, tutayakata.”
Alichosema Waziri Muhongo
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema mradi wa
kusafirisha gesi kutoka mkoani Mtwara kwenda Dar es Salaam, umeanza kwa
kasi na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda atakwenda huko wiki ijayo kuweka jiwe
la msingi.
Akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini jana, Waziri Muhongo alisema:
“Mradi wa
kujenga bomba la gesi uko palepale na unaendelea kwa kasi na Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda ataenda kuweka jiwe la msingi wiki lijalo.”
“Tumezungumza
mengi kuhusu suala hilo na hata viongozi wa watu wa Mtwara walipelekwa
nje kujifunza faida zake, lakini hata kama hawajaelewa, nimetoa kijitabu
kinachozungumzia faida mbalimbali watakazopata wana Mtwara katika mradi
huo.”
Profesa
aliyeanza hotuba yake kwa kueleza machapisho mbalimbali yaliyotolewa na
wizara yake kufafanua faida za gesi ya Mtwara kwa taifa, alisema mradi
huo uliozinduliwa Novemba mwaka jana na Rais Kikwete, unahusisha ujenzi
wa bomba lenye urefu wa kilometa 532 na kipenyo cha nchi 36.
“Bomba
hilo lina uwezo wa kusafirisha futi za ujazo za gesi milioni 784 kwa
siku. Mradi utahusisha mitambo miwili ya kusafirisha gesi asilia katika
maeneo ya Mnazi Bay- Madimba (Mtwara) na Kisiwa cha Songosongo (Lindi).
Utagharimu Dola za Marekani 1,225.3 milioni,” alisema.
Alisema
kazi za usanifu wa mradi na ulipaji fidia kwa wananchi wapatao 3,092
waliopisha maeneo ya mradi, zimekamilika na hatua za awali za ujenzi wa
mitambo ya kusafirisha gesi asilia zimeanza.
“Visima
hivyo ni kwa ajili ya mitambo ya kusafirisha gesi asilia katika eneo la
Madimba na kwa matumizi ya wananchi,” alisema na kubainisha kuwa vifaa
mbalimbali vya ujenzi wa nyumba za wafanyakazi wa mradi vimewasili
nchini mwishoni mwa Aprili mwaka huu.
Upinzani
Msemaji
wa Kambi ya Upinzani katika Wizara ya Nishati na Madini, John Mnyika
amepinga mradi huo wa kusafirisha gesi akitaka kwanza mikataba yote
iwekwe wazi na wananchi washirikishwe ili wajue faida yake.
“Kambi
rasmi ya upinzani inayoongozwa na Chadema inaitaka Serikali isiendelee
na ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam hadi; Mosi,
itakapoweka wazi kwa Bunge mikataba yote inayohusu uendelezaji wa gesi
asilia ikiwamo ya ujenzi wa bomba hilo, pili ikutane na wananchi
kuwashirikisha na kuhakikisha manufaa kwa taifa na kwao,” alisema
Mnyika.
Hata
hivyo, mjadala wa bajeti hiyo ulisitishwa jana na Spika wa Bunge, Anne
Makinda alipoahirisha Bunge saa 11.00 jioni ili kutoa nafasi kwa Kamati
ya Uongozi ya Bunge kujadili suala hilo baada ya kuonekana kuwa
limekoleza zaidi mgogoro huo.
“Wiki
mbili zilizopita tulipopanga tutajadili bajeti hii tulisikia (wananchi)
walipanga kufanya matatizo na kweli leo wakati tunajadili tayari
wamefanya matatizo. Nafikiri wengi hapa mnataka tujadili suala hili kwa
dharura, nakiri suala hilo lipo. Naiagiza Serikali kesho watoe hali
halisi ilivyo kule Mtwara.
Faida za gesi kwa Wanamtwara
Waziri
Muhongo ametaja moja ya faida za ujenzi wa bomba hilo kwa wananchi wa
mikoa ya kusini kuwa ni tozo ya asilimia 0.3 ya mauzo ya gesi asilia
pamoja na huduma za zahanati, shule, umeme, maji na ufadhili wa mafunzo
katika Vyuo vya Veta na sekondari.
“Faida
nyingine zitakazopatikana ni ujenzi wa viwanda mbalimbali ikiwamo cha
Saruji cha Dangote ambacho ujenzi wake umeanza, kiwanda cha mbolea,
mtambo wa kufua umeme wa MW 400 kupitia Kampuni ya Symbion na njia za
kusafirisha umeme ya msongo wa KV 220 kutoka Mtwara hadi Songea.”
“Aidha,
Kampuni ya Schlumberger ya Houston, Marekani imejenga karakana kubwa
Mtwara ambayo itakuwa inatengeneza vifaa vya uchimbaji, utafutaji na
uendelezaji wa rasilimali za mafuta na gesi.”
Baadhi ya
wabunge wa mikoa ya Kusini wamesema hotuba ya Bajeti ya Wizara ya
Nishati na Madini haina mkakati wowote wenye lengo la kutatua mgogoro wa
gesi asilia unaendelea mkoani Mtwara.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti, walisema mgogoro huo umefikia pabaya na njia pekee
ya kuutatua ni Serikali kufanya mazungumzo na wananchi.
“Ni
vigumu kusema hotuba ya Serikali inaweza kutatua tatizo hilo,” alisema
Mbunge wa Viti Maalumu (CUF), Clara Mwatuka na kuongeza kuwa
kinachoonekana ni kama Serikali inatumia mabavu kushughulikia suala
hilo.
Mbunge wa Lindi Mjini (CUF), Salum Barwany alisema kinachotakiwa ni Serikali kuandaa mjadala wa kina na wakazi wa Mtwara.
No comments:
Post a Comment