Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiwasili
katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Narita,Japan ambapo atahudhuria
Mkutano wa tano wa (TICAD)unaofanyika katika mji wa Yokohama.Kushoto ni
Balozi wa Tanzania nchini Japan Bibi Salome Sijaona.(picha na Freddy
Maro).
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amewasili nchini Japan jioni ya leo, Jumatano, Mei 29, 2013, kuhudhuria
Mkutano wa Tano wa Kuzungumzia Maendeleo ya Afrika ujulikanao kama Tokyo International Conference on African Development (TICAD – V) unaoanza Yokohama, mji mkubwa wa pili katika Japan, Jumamosi, Juni Mosi hadi 3, mwaka huu, 2013.
Kwenye
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Narita mjini Tokyo, Rais Kikwete ambaye
anafuatana na Mama Salma Kikwete amepokewa na Balozi wa Tanzania katika
Japan Mheshimiwa Mama Salome Sijaona na maofisa wengine wa Ubalozi wa
Tanzania katika Japan.
Rais Kikwete
amewahi kuwasili nchini Japan kabla ya Mkutano wa TICAD V kwa vile ni
mmoja wa viongozi wawili wa Afrika waliopangwa kuonana na Waziri Mkuu wa
Japan Mheshimiwa Shinzo Abe kabla ya kuanza kwa Mkutano wenyewe wa
TICAD V.
Mheshimiwa
Abe ambaye ndiye amemwalika Rais Kikwete kufanya ziara ya kikazi ya wiki
moja katika Japan wakati huu anakutana na Rais Kikwete mapema ili
kuweza kupata maoni, msimamo na matarajio ya Afrika kabla ya kuanza kwa
Mkutano wa TICAD V.
Mkutano wa
mwaka huu utakwenda sambamba na sherehe za kumbukumbu ya miaka 20 ya
Mkutano wa TICAD ambao ulifanyika kwa mara ya kwanza mjini Tokyo mwaka
1993.
Mkutano huo –
TICAD V utawashirikisha viongozi wa Afrika, viongozi wa Japan na
washirika wa maendeleo ya Afrika ikiwamo Benki ya Dunia (WB), Benki ya
Maendeleo ya Afrika (AfDB), Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU)
na Shirika la Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (UNDP) na utafunguliwa na
Waziri Mkuu wa Japan mwenyewe, Mheshimiwa Abe.
Wengine
waliopangwa kuzungumza kwenye sherehe hiyo ya ufunguzi wa Mkutano huo
mkubwa ni Waziri Mkuu wa Ethiopia Mheshimiwa Hailemariam Desalegn ambaye
ni Mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika (AU), Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa Mheshimiwa Ban Ki Moon na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Afrika
Mheshimiwa Dkt. Nkosazana Dlamini Zuma.
Mbali na
kukutana kwa mazungumzo na Waziri Mkuu Abe, Rais Kikwete pia atakuwa
miongoni mwa kundi la viongozi wa Afrika watakaokutana na Mfalme wa
Japan, H.M. Akihito.
Katika
mkutano kati ya viongozi hao wawili, Waziri Mkuu wa Japan anatarajiwa
kuwa atatangaza kuwa Japan inaifutia Tanzania deni la dola za Marekani
milioni 220 likiwa ni deni la mchele ambao Tanzania iliupata kutoka
Japan chini ya mikataba iliyotiwa saini kati ya mwaka 1980 na 1983 kati
ya Mamlaka ya Chakula ya Japan na Serikali ya Tanzania.
Aidha,
inatarajiwa kuwa Mheshimiwa Abe atatangaza rasmi kuwa Japan itagharimia
ujenzi wa barabara ya juu kwa juu (fly-over) katika eneo la Ubungo, Dar
es Salaam, kama moja ya hatua za kupunguza msongamano wa magari katika
jiji hilo.
Kabla ya
kuanza TICAD V, Rais Kikwete pia atakutana na kuzungumza na wakuu wa
mashirika makubwa na kimataifa ya kibiashara na uchumi ya Japan ambayo
yanaendesha shughuli zake katika Afrika ama yanapenda kuanzisha shughuli
katika Tanzania.
Kesho,
Alhamisi, baada ya kuwa amekutana na Mheshimiwa Abe, Rais Kikwete
atakwenda Kawasaki ambako atakutana na viongozi wa Kampuni ya Natori
Holding Management ambayo imeamua kuwekeza katika sekta ya nguo na
kilimo cha pamba katika Tanzania.
Baadaye
kesho, Mheshimiwa Rais atatembea Jumba la Makumbusho la Sayansi la
Kampuni ya Toshiba, maarufu duniani kwa utengenezaji wa kompyuta za aina
ya Toshiba na vifaa vingine vya elektroniki. Baadaye, Rais atatembelea
na kuzungumza na wanafunzi wa Shule ya WASEDA kuhusu nafasi na mchango
wa Tanzania katika uhusiano wake na Japan.
Keshokutwa,
Ijumaa, Rais Kikwete atatembelea Shirika la Sumitomo ambalo limewekeza
katika ujenzi wa kituo cha umeme cha Kinyerezi cha Dar Es Salaam ambacho
kitatoa megawati 220 na linataka kuwekeza katika miradi ya miundombinu
kwa kushirikiana na sekta binafsi katika Tanzania.
Akiwa
Sumitomo, Rais Kikwete atashuhudia utiaji saini wa ujenzi wa mradi wa
umeme wa Kinyerezi baina ya Sumitomo Corporation yenyewe, Benki ya
Maendeleo ya Japan – JBIC na Wizara ya Fedha ya Tanzania.
Mchana wa
keshokutwa, Rais Kikwete atakuwa miongoni mwa viongozi wachache wa
Afrika walioalikwa na Waziri Mkuu Mheshimiwa Abe kuzungumzia hali ya
Somalia.
Katika
mkutano huo, Mheshimiwa Abe anataka kupata mawazo ya viongozi hao
wachache wa Afrika ambayo yatawasilishwa kwenye Mkutano wa 39 wa wakuu
wa Nchi Tajiri na Zenye Viwanda Vingi Duniani – G-8 uliopangwa
kufanyika Lough Erne, Uingereza mwezi ujao, Juni 17-18, 2013.
Aidha, Rais
Kikwete siku hiyo hiyo, atakutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa
Kampuni ya Marubeni, moja ya makampuni makubwa zaidi ya biashara katika
Japan ambayo imeonyesha nia ya kujenga Kiwanda cha Kuchakata Gesi Asilia
na Kuzalisha Umeme katika Tanzania.
Jioni ya
siku hiyo, Rais Kikwete atahudhuria hafla maalum ya kitaifa
inayoandaliwa na Mheshimiwa Abe kwa ajili ya viongozi wote
watakaohudhuria Mkutano wa TICAD V.
Mkutano wa
TICAD V miongoni mwa mambo mengine utajadili mchango wa sekta binafsi,
biashara na uwekezaji kama injini za maendeleo, jinsi gani Afrika
inavyoweza kuimarisha sekta ambazo zimejithibitisha kuwa misingi ya
kukua kwa uchumi wa Bara la Afrika, Ajenda ya Maendeleo baada ya mwaka
2015 ambao ni mwisho wa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia
(MDG’s). Hatimaye, mkutano huo utatoa Azimio ya Yokohama 2013 na Mpango
wa Utekelezaji wa Yokohama kwa miaka 2013 hadi 2017.
Mikutano ya
TICAD (TICAD Policy Forum and Conference) ilianzishwa mwaka 1993 na
Japan kwa kushirikiana na UN, UNDP na Benki ya Dunia kwa njia ya
kujadili na kuendeleza ajenda ya maendeleo ya Bara la Afrika.
Chini ya
mchakato huo wa TICAD, Japan hujenga mazingira ya kuunga mkono ajenda
ya maendeleo ya Bara la Afrika ambalo nalo ndilo linamiliki na kuongoza
jukumu la kimsingi la kujiendeleza kwa kushirikiana na Bara la Asia na
Jumuia ya Kimataifa.
Tokea
ulipofanyika mkutano wa kwanza – TICAD 1 mjini Tokyo Oktoba 5-6, mwaka
1993, imefanyika mikutano mingine mitatu na kujenga mazingira mazuri
zaidi ya jinsi Japan na Jumuia ya Kimataifa inavyoweza kuchangia
maendeleo ya Afrika.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
26 Mei, 2013
No comments:
Post a Comment