SAKATA
la kijana Bonny Fabian Kavishe kudaiwa kumuua kwa kumpiga risasi baba
yake, mzee Livingstone Kavishe akiamini ni mwizi sasa ni simulizi ya
machozi kufuatia kusomwa kwa waraka mzito ulioandikwa na mtuhumiwa huyo
ambaye bado yupo mahabusu ya Polisi Mlandizi, Bagamoyo, Pwani
Waraka
huo ulizidi kuwatoa machozi baadhi ya waombolezaji siku ya mazishi
yaliyofanyika Marangu, Wilaya ya Moshi Vijijini, Mkoa wa Kilimanjaro
kutokana na maneno yenye huruma ya Bonny kuomba msamaha.
WARAKA ULIANDIKIWA NDANI YA MAHABUSU
Habari
zisizo na chenga wala kumulika tochi zinasema, mtuhumiwa akiwa mahabusu
aliamua kuandika waraka huo na kumpa ndugu yake mmoja (jina
halikupatikana) akimpa maelekezo kwamba usomwe siku ya mazishi ya mzee
huyo kabla hajafukiwa kaburini kwa vile yeye hatakuwepo.
“Kwa
kweli inauma sana! Jamaa alipoona hatapata ruhusa ya askari ili
akashiriki mazishi ya baba yake aliomba karatasi na kalamu na kuandika
waraka, akampa ndugu yake mmoja, akamwambia usomwe siku ya mazishi ya
marehemu kabla hajafukiwa kaburini,” kilisema chanzo.
MWILI WAAGWA NYUMBANI KWA MTUHUMIWA, WASAFIRISHWA NA WARAKA
Jumatano
ya Mei 15, mwaka huu, mwili wa marehemu mzee Kavishe uliagwa nyumbani
kwa mtuhumiwa licha ya yeye kutokuwepo na ukasafirishwa kwenda Marangu
kwa mazishi.
Miongoni
mwa mambo yaliyozingatiwa kwenye kusafirisha mwili huo ni uwepo wa
waraka huo ambao mtuhumiwa aliomba usomwe mbele ya waombolezaji siku ya
mazishi.
MANENO NDANI WARAKA NI HAYA
Siku
ya mazishi, mwanaume aliyepewa jukumu la kuongea kwa niaba ya familia
aliusoma waraka huo huku waombolezaji wakiwa makini kumsikiliza.
Alisema
waraka huo umeandikwa kwa mikono ya Bonny Kavishe, licha ya kuzungumzia
mambo mengine, aliwaomba msamaha ndugu, jamaa na marafiki kwamba
wamsamehe kwa kitendo cha kumuua baba yake.
Alisema
alifanya kitendo hicho bila kukusudia na wala hajui nini kiliendelea.
Haikuwa nia yake kumtoa uhai baba yake aliyefikia nyumbani kwake
Mlandizi kwa ajili ya kusherehekea harusi ya mdogo wa mtuhumiwa huyo
iliyofanyika Mei 11, mwaka huu.
WARAKA WAWATOA MACHOZI WAOMBOLEZAJI
Chanzo
kinasema: Yaani wakati waraka huo ukisomwa ndugu na jamaa walilia sana
ikawa ni machozi mara mbili. Kwanza kwa mzee Kavishe kufariki dunia,
pili kwa sababu ya ndugu yao huyo ambaye yuko mahabusu kutokana na
kumuua baba yake. Sehemu kubwa ya waraka huo, Bonny alikuwa akiomba
msamaha.
MTUHUMIWA AFUNGA KULA NA KUNYWA
Maneno
mengine yaliyopatikana ndani ya waraka huo ni mtuhumiwa kusema tangu
siku ya tukio hilo, Mei 12, mwaka huu ambapo alikamatwa na kuswekwa
mahabusu, hakula wala kunywa kitu chochote kwa muda wa saa 48 kwa sababu
akili yake ilikinai kufuata utaratibu wa kibinadamu kufuatia kitendo
cha kumtoa uhai baba yake.
TUMEFIKAJE HAPA?
Mzee
Kavishe alitoka Marangu mkoani Kilimanjaro na kufika Mlandizi kwa ajili
ya harusi ya mtoto wake ambaye ni mdogo wa Bonny, aitwaye Boniface
Fabian Kavishe.
Baada
ya harusi kumalizika, familia ilirudi nyumbani kwa Bonny kwa ajili ya
kupumzika. Marehemu aliandaliwa chumba chake ambapo aliingia kulala huku
akiwatakia usiku mwema wanaye.
Usiku
wa saa tisa kuelekea Jumapili, mzee Kavishe aliamka, akatoka kwenda
chooni. Alipomaliza alirudi ndani lakini kwa vile macho yake yalikuwa
hayaoni vizuri alishindwa kutambua chumba alichokuwa amelala hivyo
akajikuta akiingia chumba alicholala mwanaye Bonny na mkewe Eva.
Inadaiwa
wakati huo Eva alikuwa macho, ila Bonny alikuwa usingizini. Eva
alishtuka kusikia kitasa cha mlango kikishikwa na mtu kuingia, akapiga
kelele za mwiziii! Mwizii jamani!
Kelele
hizo zilimwamsha Bonny ambaye naye bila kujua, alichukua bastola kutoka
kwenye makazi yake na kumfyatulia ‘mwizi’ huyo. Risasi ilichomoka kwa
kasi na kumwingia mzee huyo kwenye paji la uso ambapo alianguka chini na
kukata roho papohapo.
Baada
ya tukio hilo Bonny alitoka kitandani na kwenda kuwasha taa kwa lengo
la kumtambua ‘mwizi’ huyo. Hamadi! Kumbe ni baba yake ambaye muda mfupi
nyuma walikuwa kwenye cherekochereko za harusi wakila na kunywa kwa
furaha.
MKUU WA KITUO AMWELEZEA MTUHUMIWA
Paparazi
wetu alipata nafasi ya kuzungumza na Mkuu wa Kituo cha Mlandizi,
Bagamoyo, Pwani, Afande Shaban Musa ambapo alikiri kutokea kwa tukio
hilo, akasema uchunguzi bado unaendelea na mtuhumiwa mpaka juzi Jumapili
anashikiliwa na jeshi hilo.
Akaongeza:
Hili kweli ni jambo la kuhuzunisha kwani mtuhumiwa si mtu wa shari,
mpole sana lakini nilishangaa siku hiyo kumwona anakimbilia hapa kituoni
mwenyewe na kusema amemuua baba yake.”
Marehemu Kavishe alizikwa Mei 17, 2013.
Mungu ailaze pema peponi rojho yake. Amina.
chanzo:globalpublishers
No comments:
Post a Comment