Pages

Tuesday, May 21, 2013

WIZARA YAENDELEA KUSISITIZA MSD ILIUZIWA ARV ‘FEKI’ WIZARA YAENDELEA KUSISITIZA MSD ILIUZIWA ARV ‘FEKI’


ARVs a27e5
Serikali kupitia Wizara ya ya Afya na Ustawi wa Jamii imeendelea kusisitiza kwamba Kampuni ya TPI Ltd iliiuzia Bohari ya Dawa (MSD) dawa bandia za kupunguza makali ya Ukimwi aina ya TT-VIR 30 toleo Na.0C.01.85,kwa mujibu wa nyaraka zilizopo na kwamba dawa hizo zilibainika kuwa ni bandia.
Msisitizo huo umetolewa katika vyombo vya habari jana na ofisi ya Wizara ya afya na Ustawi wa jamii kupitia kwa msemaji wake Nsachris Mwamwaja ili kuondoa mkanganyiko ambao umeanza kujitokeza kwa wananchi.
Katika taarifa hiyo Serikali imesema kuwa kama ilivyoelezwa katika taarifa mbalimbali za umma zilizokwisha kutolewa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na TFDA kuhusiana na suala hili, bado inasisitizwa dawa hizo zilikuwa bandia.
"Tunapenda kusisitiza kwamba, waziri katika hotuba yake hakukanusha kuwa Kampuni ya TPI Ltd iliiuzia MSD dawa bandia bali alieleza kwamba uchunguzi wa awali katika kiwanda cha kampuni hiyo haukuonyesha dawa hiyo ilizalishwa na TPI Ltd bali vifungashio ni vya TPI Ltd na nyaraka zinaonesha TPI Ltd kuiuzia MSD dawa hizo bandia,"ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha, msemaji huyo wa wizara katika taarifa hiyo alieleza kuwa vyombo vya usalama bado vinaendelea kulichunguza suala hilo ili kubaini chanzo na wahusika wakuu wa dawa hizo bandia .
Hivyo kwa kuzingatia unyeti wa suala hilo,wizara imetoa wito kwa vyombo vya habari kusubiri hatma ya uchunguzi unaofanywa na vyombo vya usalama na kuepuka kutoa taarifa ambazo zinaweza kupotosha umma na jitihada kubwa za Serikali katika kupambana na dawa bandia nchini.
Mnamo Mei 9, 2013, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi katika kuhitimisha hoja ya bajeti ya wizara alitolea ufafanuzi suala la dawa bandia ya ARV kufuatia hoja zilizokuwa zimetolewa na Zarina Madabida (Mb) kuhusu kuhusika kwa Kiwanda cha Dawa cha Tanzania Pharmaceutical Industries Ltd (TPI) katika sakata la dawa bandia ya ARV.

No comments:

Post a Comment