Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya Diwani Athumani
------------------------------------------
Na Gordon Kalulunga,
Mbeya
MKOA wa Mbeya ukiwa
ni moja ya mikoa inayoongoza kwa migogoro na kesi za ardhi, imefikia hatua sasa
wananchi wameanza kuviziana na kuuana.
Mkulima wa Kijiji
cha Suma wilayani Rungwe Saita Mboma(65), amefariki dunia baada ya kuvamiwa
usiku nyumbani kwake na kukatwakatwa na mapanga.
Taarifa ya Jeshi la
polisi mkoa wa Mbeya iliyosambazwa kwenye vyombo vya habari leo na kusainiwa
na kamanda wa polisi Diwani Athumani, imesema tukio hilo lilitokea Juni 22,
mwaka huu kijijini hapo na kukutwa na mauti Juni 24, mwaka huu.
‘Kabla hajapatwa na
mauti alikimbizwa katika hospitali ya Makandana wilayani humo kwa ajili ya
matibabu ambapo taarifa zinasema kuwa alikuwa akiishi peke yake na alivamiwa
akiwa amelala na chanzo ni mzozo wa muda mrefu wa mashamba’’ imeeleza taarifa
hiyo.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa
watuhumiwa wa tukio hilo wamekamatwa ambao ni Salum Mwambona(45) na Feda Busila
ambao wote ni wakazi wa kijiji cha Itagata na taratibu za kuwafikisha
mahakamani zinafanywa.
Wakati huo huo,
ajali za barabarani zimegeuka janga la mkoa wa Mbeya ambapo hazipiti siku Nne
bila kupoteza maisha ya watanzania au kupata ulemavu wa kudumu.
Katika mwendelezo wa
ajali hizo, askari Polisi wa kikosi cha FFU Jijini Mbeya, amefariki papo hapo
baada ya kugongwa na gari eneo ya barabara ya Benki kuu Jijini hapa.
Taarifa polisi,
imesema kuwa ajali hiyo ilitokea Juni 23
mwaka huu.
Taarifa hiyo imesema
kuwa gari na dereva asiyefahamika, liligonga gari T.741 BXU aina ya March
lililokuwa limeegeshwa eneo la hilo kisha kumgonga mtembea kwa miguu askari
Polisi aitwaye EX.G 9386 PC Patrick(23)
na kusababisha kifo chake papo hapo.
‘’Chanzo
kinachunguzwa. Dereva alikimbia na gari mara baada ya tukio na mwili wa
marehemu umesafirishwa kwenda Dodoma kwa ajili ya mazishi na yeyote mwenye
taarifa za alipo dereva huyo na gari atoe taarifa kwenye mamlaka husika ili
sheria iweze kuchukua mkondo wake’’ imesema taarifa hiyo.
Mbali na ajali hiyo,
jana Juni 25, mwaka huu, ajali nyingine imesababisha kifo cha Vedasto
Emmanuel(20) na majeruhi kwa watu watano eneo la Njia panda Ilomba Jijini
Mbeya.
Watu waliojeruhiwa
katika ajali hiyo ni Lusajo John(22), Yohana Daud(20), Hussein Mbilinyi(20),
ambao wamelazwa hospitali ya rufaa ya Mbeya na mwingine ni Andrew Daud(20).
No comments:
Post a Comment