Pages

Wednesday, June 26, 2013

Ujio wa Obama Dar: Ulinzi mkali JNIA, wasafiri kulazimika kubadili ratiba



Dar es Salaam. Maandalizi ya ujio wa Rais wa Marekani, Barack Obama nchini yanazidi kupamba moto huku maofisa wa usalama wa Marekani wakipiga kambi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam.
Aidha, kutokana na ujio huo, Serikali imeagiza mashirika yote ya ndege kubadili ratiba zao za safari Julai Mosi, siku ambayo Rais huo atatua nchini.
Jana, waandishi wetu walishuhudia pilikapilika za kuimarisha ulinzi katika uwanja huo jambo ambalo uongozi wa uwanja huo jambo wamelieleza kwamba halijawahi kutokea.
Ulinzi haujawahi kutokea
Mkurugenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Moses Malaki alisema jana kwamba ratiba za uwanjani hapo zitabadilika kutokana na uzito wa ugeni huo.
Alisema kwa kawaida anapokuja kiongozi mkubwa wa kitaifa katika uwanja huo hakuna ndege inayoruhusiwa kutua kwa kipindi cha nusu saa.
“Ni kweli hali hiyo pia itakuwapo atakapokuja Rais Obama na safari za ndege zitabadilika kulingana na ratiba ya kutua na kuondoka kwa Rais huyo,” alisema Malaki.
Pia alisema ulinzi katika uwanja huo umeimarishwa kwa mwezi mmoja sasa na tangu wakati huo, maofisa wa usalama wa Marekani wamekuwa wakifika kwa nyakati mbalimbali.
“Sijawahi kuona ulinzi mkali kama huu, wamekuja marais wengi hapa nchini lakini ulinzi huu ni wa kutisha, sijui kwa sababu gani?” alisema Malaki.
Alisema awali, wakati maofisa hao walipoanza kuwasili nchini hawakutambua ni mgeni gani anayetarajia kufika lakini baadaye walipelekewa taarifa kuwa ni Rais Obama na baadaye walitaarifiwa kuwa angetua saa 8.40 mchana, Julai Mosi.
Mkurugenzi huyo alisema Rais Obama atakuja na ndege nne, moja itakayombeba, ya pili kwa ajili ya mizigo, ya tatu itakuwa ya waandishi wa habari na maofisa wa usalama na ya mwisho ni kwa ajili ya dharura ambayo itaegeshwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Malaki alisema maofisa wa Marekani wanaowasili nchini wamekuwa wakifanya shughuli mbalimbali za kuhakikisha kuwa hali ya usalama inaimarishwa na kuwaacha wazawa wakifanya shughuli za kawaida.chanzo gazeti la mwanainchi

No comments:

Post a Comment