Pages

Thursday, July 25, 2013

Aliyevua nguo kortini kumlalamikia hakimu afungwa jela maisha


Jefferson Muthee Ng'ang'a
Kwa Mukhtasari
Mwanamume aliyevua nguo mbele ya hakimu kumshurutisha ajiondoe katika kesi ya wizi wa mabavu amehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kumnyang’anya kimabavu afisa wa polisi bastola.
MWANAUME aliyevua nguo mbele ya hakimu kumshurutisha ajiondoe katika kesi ya wizi wa mabavu jana alihukumiwa kifungo cha maisha kwa kumnyang’anya kimabavu afisa wa polisi bastola.
Jefferson Muthee Ng’ang’a mwenye umri wa mika 19 hakuhurumiwa na Hakimu mwandamizi Bi Lucy Mbugua licha ya kumweleza “ akisukumwa jela nyanya yake na mama yake watateseka sana.”


“Ulikuwa na nia ya kusababisha kifo cha Konstebo Koech Kiptoo kwa vile ulimpiga rungu kisogo na kumlemaza kabisa. Konst Kiptoo aliumia kichwani na kupoteza ufahamu kwa muda wiki mbili.” akasema Bi Mbugua.

Ng’ang’a aliyezua kioja kortini mwezi Mei mwaka huu aliomba korti msamaha akisema “ndoto yake ni kuwa mwanasoka wa kimataifa na itakatizwa akisukumwa korokoroni na yuko na umri mdogo.”
“ Mimi nilitazamia kuimarisha kipawa changu cha usakataji kambumbu na kufikia kiwango cha kimataifa.Lakini jinsi mambo yalivyo ndoto hiyo imeambulia patupu.Naomba usinihukumu kifo.Nyanya yangu na mama yangu watasononeka na kuumia kimaisha kwa vile nilikuwa tegemeo lao. Baba yangu alikufa nikiwa gerezani. Naomba unihurumie,” akasema Ng’ang’a akijitetea baada ya kupatikana na hatia ya kumnyang’anya kimabavu Konstebo Koech Kiptoo bastola ikiwa na raundi 15 za risasi mnamo Machi 22, 2012.

Mbali na bastola hiyo mshtakiwa alimnyang’anya afisa huyo wa polisi kitambulisho cha kazi , kadi za benki na pia simu ya rununu. Thamani ya vitu hivyo vyote ni Sh190,270.

Pia alimjeruhi Konst Kiptoo kichwani alipomtwaga kwa rungu.

Konst Kiptoo alilalazwa hospitali ya Forces Memorial kwa wiki mbili kabla ya kupata fahamu.

Baada ya kumpora afisa huyo wa usalama bastola, mshtakiwa alifulululiza moja kwa moja hadi kijiji cha Malaa kilichoko wilayani Kangundo Kaunti ya Machakos na kutekeleza uhalifu.

Kule kijijini Malaa mshtakiwa alitumia bastola hiyo kumjeruhi John Kilonzo Mwinzi na kumunyang’anya simu na pesa. Mlalamishi huyo alikutwa shambani mwake akiwa na wafanyakazi watatu Bi Mercy Nthambi Mulwa, Bi Damaris Wayua Musee na Bi Tina Mwikali Musee.

Risasi

Vile wahenga walinena siku za mwizi ni 40 mshtakiwa alionekana na wanakijiji akiwashambulia walalamishi hao wakiwa shambani “ lakini hawangemkaribia kwa vile alikuwa anapiga risasi angani kuwatisha.”

Msamaria mwema alipigia maafisa wa polisi katika kituo cha Kangundo.

“ Mshtakiwa alikutwa kijijini Malaa akiwa na bastola na risasi mbili. Baada ya kufanyiwa ukaguzi ilitambuliwa kuwa ni bastola aliyoporwa Konst Kiptoo katika Muthaiga Drift eneo la Mathare Nairobi.”akasema Bi Mbugua.

Hakimu huyo alisema mshtakiwa alipatikana akiwatisha na kuwapora umma akitumia bastola hiyo.

No comments:

Post a Comment