Bi. Rejina Moshwa (37) mkazi wa Kijiji cha Isoso akizungumza na mwandishi wa habari kutoka Clouds FM Aziz Kindamba
Paschal Kulwa Manyinzi (42) mkazi wa Kijiji cha Isoso akiwa katika picha na baadhi ya watoto wake baada ya mazungumzo na Thehabari.com
Paschal Kulwa Manyinzi (42) mkazi wa Kijiji cha Isoso akiwa katika picha na baadhi ya watoto wake baada ya mazungumzo na Thehabari.com
………………..
Na Thehabari.com, Kishapu
WASUKUMA
ni moja ya makabila nchini Tanzania ambayo awali yalishikilia desturi
ya familia kuwa na idadi kubwa ya watoto. Familia moja yaani baba na
mama waliendelea kuzaa kadri walivyo jaaliwa kupata watoto bila kujali
ukubwa wa familia.
Mume pia hakuwa na kizuizi katika familia cha kuongeza mke mwingine
endapo atakuwa na ardhi (mashamba) na mifugo (hasa ng’ombe) ya kutosha
kuweza kuihudumia familia aliyonayo.
Wapo walioamini kwamba kuwa na ukubwa wa familia ni kuongeza nguvu kazi katika uzalishaji kwa kutumia ukubwa wa familia.
Hata
hivyo pia wapo walioamini uzazi ni mpangilio wa Mungu hivyo haupaswi
kupangiliwa na wazazi bali mola mwenyewe. Hivyo basi familia za imani
hii ziliendelea kuza hadi pale uwezo wa kupata watoto ulipopotea wenyewe
au vizuizi vingine.
Hata
hivyo sasa hivi mambo yamebadilika kiuchumi, hali ni ngumu hivyo
familia nyingi zinapangia idadi ya watoto. Waliojisahau na kuendelea
kuzaa idadi kubwa ya watoto pasipo na uwezo kuwamudu wanajuta na
kutamani wangelipata uelewa wa elimu hiyo awali.
Hali
hii ya majuto ndiyo inayozikuta baadhi ya familia katika vijiji anuai
Kata ya Kishapu, mkoani Shinyanga, baada ya kuzungumza na mwandishi wa
makala haya. Familia hizi zimejikuta na idadi kubwa ya watoto kiasi cha
baba na mama kushindwa kuwapatia mahitaji ya msingi watoto wao hivyo
familia kuendelea kuwa na maisha duni kiuchumi.
Bi.
Rejina Moshwa (37) mkazi wa Kijiji cha Isoso ni miongoni mwa familia
zinazojutia uamuzi wa kuwa na idadi kubwa ya watoto. Anasema familia yao
ilikuwa na jumla ya watoto 10, lakini bahati mbaya wawili walifariki
dunia hivyo kubakia na watoto nane ambao ni mzigo mkubwa hivi sasa.
“…Hatukuwa
na elimu ya kupangilia watoto tulizaa mfululizo kadri ya tulivyo
jaaliwa, lakini watoto hawa sasa ni mzigo kwetu, tunajuta. Tumeshindwa
kuwasomesha na wamekosa muelekeo…na hata upatikanaji wa chakula cha
familia nzima ni tatizo…hasa ukichangia na hivi karibuni ukame uliibuka
eneo hili mambo yamezidi kuwa mabaya,” anasema Bi. Moshwa.
Paschal
Kulwa Manyinzi (42) ni mume wa Bi. Rejina Moshwa, anasema licha ya kuwa
na mifugo kidogo yeye ni mkulima wa mazao mchanganyiko yaani Pamba,
mtama, karanga na viazi. Anakiri watoto wake mwenyewe kuwa mzigo mkubwa
kimalezi kwa sasa. “Wakati tunaanza kuzaa nilifuata mila na desturi za
zamani, unajua zamani suala la kuzaa halikuwa la kupangilia, mtu ulikuwa
unazaa tuu…suala la kupangilia limeanza juzi.
“Zamani
(enzi za wazazi wetu) idadi kubwa ya watoto katika familia ilikuwa ni
nguvu kazi…lilikuwa likizaidia katika kilimo…kama mtu ulikuwa hauna
familia kubwa ulitapata shida kwenye kilimo. Lakini dunia ya sasa huwezi
kuzaa kama mimi ni mzigo,” anasema Manyinzi.
Hata
hivyo licha ya ukubwa wa familia hii haina ardhi ya kutosha kwa ajili
ya kilimo kwani heka tano ambazo inadai ilipewa kwa urithi toka kwa
wazazi wa Manyinzi imetwaliwa na Serikali kwa ajili ya shughuli za
maendeleo na kubaki heka moja. Familia hii inalazimika kukodi ardhi kwa
ajili ya kilimo kila msimu wa kilimo.
Modesta
Machia (43) ni Mkazi wa Kijiji cha Kishapu, Kata ya Kishapu Wilaya ya
Kishapu. Anasema yeye na mumewe wana jumla ya watoto nane walio hai kati
ya 10 ambao walibahatika kuwazaa. Anasema watoto wawili walitangulia
mbele za haki. Anasema watoto walionao kwa sasa ni mzigo katika malezi.
“…Mwanzoni
tulikuwa tunazaa haraka haraka kwa kuwa hatukuwa na uelewa juu ya uzazi
wa mpango…lakini laiti ningejua nisingelikubali kupata idadi kubwa ya
watoto kama ilivyo sasa…lakini nimepata uelewa nikiwa nimechelewa na
nimefunga kizazi kabisa,” anasema Bi. Machia. Anasema mume wake kwa sasa
ni muhudumu wa usafi katika zahanati ya kijiji chao.
Mwanamama
huyu anashauri familia nyingine kuzaa kwa mpangilio na kuzingatia
kipato cha familia ili kupunguza umaskini wa kiuchumi katika familia.
Anasema mwanamke kuzaa mfululizo hushindwa kuchangia shughuli za
kujiongezea kipato katika familia na hata kuchoka mapema kwenye shughuli
za uzalishaji mali.
Hata
hivyo changamoto nyingine kwa uzazi wa idadi kubwa ya watoto ipo kwa
akinamama pekee, kwani inapotokea mke na mume wakatofautiana na kufikia
kuachana, idadi kubwa ya kinababa humuachia mke watoto waliozaa na yeye
kwenda kuoa sehemu nyingine.
Bi.
Paskazia John mama mwenye watoto nane amekubwa na hali kama hiyo, kwani
baada ya kuzaa na mumewe watoto nane walikorofishana na kutengana hivyo
mwanaume kumuachia watoto wote nane ambao kwake ni mzigo mara dufu.
Anasema unapoolewa katika familia ya kisukuma hasa maeneo ya vijijini
kuzaa idadi kubwa ya watoto ni kitu cha kawaida. Anaongeza kuwa na
endapo utaonekana mvivu wa kuzaa mwanaume anaweza kukuongezea mke
mwenzako ili akusaidie.
Anabainisha
kuwa baadhi ya wanaume wa kisukuma wanaamini kwamba kuwa na idadi kubwa
ya watoto ni sawa na kuwa na uwezo kiuzalishaji, yaani watoto
watatumika kama nguvu kazi shambani. Lakini kwa kuwa kaya nyingi za
maeneo ya wasukuma mama (mke) pamoja na watoto huwa ndiyo watendakazi
wakubwa mashambani huku baba akibaki kuwa msimamizi na kiongozi wa
familia wanawake ndiyo wenyemzigo mkubwa katika familia nyingi za
kuangaika na watoto.
Hata
hivyo si familia zote zenye mzigo mkubwa wa watoto wanashindwa
kuzimudu. Ally Sosoma (60) ni mkulima na mkazi wa Kijiji cha Isoso,
katika familia yake ana jumla ya watoto 20 ambao wamepatikana ndani ya
wake watatu. Anasema familia yake imeanza kuwa mzigo mkubwa kwake baada
ya kuanza ukame mfululizo yaani mwaka 2011 hadi sasa. Anaongeza kuwa
hapo nyuma haikuwa mzigo kwa kuwa alikuwa anajituma na ardhi ya kutosha
hivyo alizalisha chakula na ziada ya kutosha jambo ambalo haikuwa tabu
kuendesha familia yake.
Anasema
mila na desturi ya kuwa na idadi kubwa ya watoto ameirithi kutoka kwa
baba yake ambaye alikuwa na wake watatu. “…Pamoja kwamba baba alikuwa na
wake watatu lakini baba yangu mkubwa alikuwa na wake saba hivyo alikuwa
na watoto wengi sana, hivi ndio chanzo cha kuwa na idadi kubwa ya
watoto…mimi nilipenda na ndiyo maana nimezaa wengi. Lakini si kweli
kwamba watu wanasema ukioa mwanamke wa kisukuma na kutozwa ng’ombe
nyingi lazima akuzalie watoto wengi,” anasema Sosoma.
Kwa
upande wake, Yamesa Sheka mkulima mkazi wa Kishapu; anasema mila na
desturi za kuwa na idadi kubwa ya watoto kwa sasa zimepitwa na wakati
kutokana na kupanda kwa gharama za maisha. Idadi kubwa ya watoto
inachangia umaskini katika familia nyingi kwa kile wazazi kushindwa
kuwahudumia watoto. Kijana huyu anawatoto saba kwa sasa lakini anajuta
kuwapata kwani ni mzigo kuwalea. “…Ningelipata elimu ya uzazi mapema
ningelikomea watoto wanne tu, lakini haikuwa hivyo,” anasema Sheka.
Maxmilian
Lugembe ni Ofisa Mtendaji Kata ya Kishapu, akizungumzia utaratibu wa
familia kuzaa idadi kubwa ya watoto anasema inachangiwa na mfumo dume
ambao wameuendekeza familia nyingi za kisukuma. Anasema katika mfumo huo
baba ndiye mwenye maamuzi ya kuongeza watoto bila kushauriana na mwenza
wake.
“…Maeneo
haya familia kuwa na watoto 10 au 8 ni kitu cha kawaida. Elimu
inatolewa ya uzazi wa mpango ambayo anaipata mama pekee lakini kutokana
na mfumo dume mama hana uamuzi katika familia hivyo unakuta
aisaidii…kwanza wanaume hawataki wake zao kujiusisha na uzazi wa mpango
(kutumia dawa kupanga uzazi) na wengine wakifanya kwa siri na
kugundulika unakuwa ugomvi mkubwa,” anasema Lugembe.
“Inafikia
wakati hata wanawake wanaoonekana kupanga uzazi katika ndoa zao
wanaaminika kuwa ni wahunu, yaani wanataka kupumzika kuzaa ili wapate
nafasi ya kufanya maovu (uhuni) nje ya ndoa. Wapo wanaoamini kuwa ishara
ya kumpenda mwanaume ni kumzalia watoto…unazaa uwezavyo hadi uchoke,”
anasema.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com
No comments:
Post a Comment