Pages

Thursday, July 18, 2013

HUZUNI::Mwanafunzi wa kike DSM ajinyonga kupinga kusoma

Mwanafunzi  wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Tegeta jijini Dar es Salaam, Bertha Amir (14), pichani, amejinyonga hadi kufa akipinga kulazimishwa na mama yake mzazi kusoma.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, alisema mwanafunzi huyo alijinyonga juzi  saa 11:00 jioni, maeneo ya Tegeta Namanga, jijini Dar es Salaam.
Alisema marehemu alikutwa amejinyonga chumbani kwa kutumia mtandio ulioning’inizwa juu ya dari.
Kamanda Wambura alisema sababu za mwanafunzi huyo kujinyonga bado hazijafahamika, lakini akasema inasadikika kuwa wakati wa enzi za uhai wake, siku moja kabla ya kifo chake, alikuwa ameongea na mama yake, Angelina Maiko Mshami (30), ambaye alimtaka achukue fedha kwa ajili ya kujiandaa kwenda shule.
Alisema mtoto huyo alimjibu mama yake kuwa hahitaji kusoma, bali anataka kufanya kazi. 




Kamanda alisema kuwa mwili wa mwanafunzi huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala kwa uchunguzi na kwamba, polisi wanaendelea na upelelezi kuhusiana na kifo chake.
 Mama wa mtoto huyo, Angelina Mshami, alisema alishangazwa na kitendo cha mtoto wake kuamua kukataa shule ghafla wakati alikuwa ana uwezo mzuri darasani.

Alisema kuwa mtoto wake alikuwa na akili darasani akishika nafasi ya kwanza ama ya pili wakati akisoma shule ya msingi na hivyo kumfanya afaulu kujiunga  kidato cha kwanza.

Hata hivyo, alisema kabla ya kifo chake, binti yake alimweleza kuwa hataki shule bali anataka kufanya kazi.

Alisema alipomuuliza kazi gani anataka kuifanya, hakuitaja bali alisisitiza kuwa anaifahamu mwenyewe.

Betha ambaye ni mtoto wa kwanza kati ya watoto wawili katika familia yao, alizaliwa mwaka 1999, Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga.

Alianza  darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Malindi mkoani Tanga na kufanikiwa kujiunga na Shule ya Sekondari Mtumbi na baadaye kuhamishiwa katika Shule ya Sekondari Tegeta.

Aidha, baadhi ya majirani waliokuwapo msibani hapo, walielezea masikitiko yao na huzuni kuhusiana na kifo cha msichana huyo.

Marehemu anatarajiwa kusafirishwa leo kuelekea mkoani Tanga kwa mazishi yatakayofanyika kesho kijijini Malindi


No comments:

Post a Comment