Dar
es Salaam. Mfanyabiashara maarufu nchini, Alex Massawe ambaye alikuwa
anatafutwa na Polisi wa Tanzania kwa muda mrefu, amekatwa Dubai, Falme
za Kiarabu (UAE).Mkuu wa la Shirika la
Polisi la Kimataifa (Interpol), Tawi la Tanzania, Kamishna Msaidizi wa
Polisi (ACP), Gustav Babile aliliambia gazeti hili jana kwamba Massawe
alikamatwa kati ya Juni 20 na 25 mwaka huu kwenye Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Dubai akitokea Afrika Kusini.Babile alisema hivi sasa walikuwa wanaandaa taratibu za kumrudisha nchini ambako amekuwa akisakwa kwa muda mrefu.“Ombi
la kuleta mhalifu nchini kutoka nje ya nchi (extradition request), lina
hatua ndefu. Unajua kuna mlolongo wa taratibu za kutekeleza ili Massawe
aletwe. Kwanza lazima Polisi wa Tanzania watoe tangazo kwa Interpol
kuhusu kumsaka mtu huyo ili aletwe,” alisema Babile.Alisema Massawe alikamatwa wakati akifanya taratibu za ukaguzi baada ya kuwasili UAE.Massawe
ambaye anamiliki majumba na biashara ya utalii katika Miji ya Arusha,
Dar es Salaam na Moshi, inadaiwa kwamba alikutwa na pasi tatu bandia za
kusafiria zilizokuwa na majina tofauti wakati alama zake za vidole
zilionyesha anaitwa Alex Massawe.“Maofisa
wa Usalama wa uwanja wa ndege walimuuliza kuwa wewe ndiye Alex Massawe?
Alikana lakini alielezwa kuwa alama za vidole vinaonyesha anaitwa
hivyo,” kilidokeza chanzo cha habari hizi kwa simu kutoka Dubai. Hata
hivyo, Babile alisema hakuwa na taarifa za Massawe kukutwa na pasi
bandia za kusafiria
.
Uvumi wa Aprili
Mapema
Aprili 27, mwaka huu kulikuwa na habari kwamba Massawe amekamatwa
katika mji mmojawapo ulioko katika Pwani ya Afrika Kusini.
Habari
hizo za kukamatwa kwa Massawe, ambaye pia hufadhili masuala ya kisiasa
na michezo, zilisambaa kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii ya
Facebook, Twitter na Jamii Forum. Kulikuwa kuna mkanganyiko wa taarifa
huku wengine wakidai alinaswa akiwa ndani ya boti huko Afrika Kusini,
wengine wakidai alikamatwa wakati akijaribu kuingia Msumbiji akitokea
Malawi.
Akizungumzia
hilo Babile alisema huo ulikuwa ni uzushi na baada ya kuzisikia taarifa
hizo walifuatilia katika maeneo aliyohusishwa kukamatwa na kubaini
kwamba hapakuwa na ukweli wowote
Kwa nini Massawe anatafutwa
Aprili 4
mwaka huu, mfanyabiashara huyo alitajwa mahakamani katika kesi ya mauaji
ya mfanyabiashara Onesphory Kituly ambaye aliuawa katika mazingira ya
kutatanisha Novemba 6, 2011 akiwa nyumbani kwake Magomeni, Dar es
Salaam.
Katika
kesi hiyo ambayo mshtakiwa wa kwanza ni mfanyabiashara maarufu, Abubakar
Marijani ‘Papaa Msofe’ na mshtakiwa mwingine, Makongoro Joseph Nyerere
alitoa malalamiko mbele ya Hakimu Mkazi, Agnes Mchome baada ya Wakili wa
Serikali, Mwanaisha Kombo kudai upelelezi wa kesi hiyo bado
haujakamilika na kuomba tarehe mpya ya kuitaja. Mshtakiwa huyo, aliomba
jalada la kesi yao lipelekwe mahakamani hapo kwa ajili ya kulifanyia
kazi na kutuhumu kuwa ndugu wa marehemu Kituly hawataki maendeleo ya
kesi yao hadi Massawe akamatwe.
chanzo:mwananchi
No comments:
Post a Comment