Na Baraka Mpenja wa Fullshangwe Dar es salaam
Maandalizi
ya kuelekea msimu mpya wa ligi kuu soka Tanzania bara unaotarajiwa
kuanza kushika kasi Agosti 24 mwaka huu yanazidi kushika kasi kwa timu
shiriki kujifua vikali sana.
Huko
jijini Mbeya, klabu mpya ya ligi kuu, Mbeya City, imeanza mazoezi makali
ya “Gym” na kukimbia kwa kasi ili kutafuta pumzi ya kuhimili mitanange
ya ligi kuu.
Kocha mkuu wa klabu hiyo, Juma Mwambusi amezungumza na FULLSHANGWE
kwa njia ya simu kutokea jiji la kijani na kueleza kuwa kwa sasa ni
ngumu kutathimini maendeleo ya kikosi chake kwani ndio kwanza wanaanza
mazoezi, lakini kwa siku chache alizowaona vijana wake wameonesha morali
na uwezo mzuri.
“Ndio
kwanza nimeanza kujifua vijana wangu, baada ya wiki moja na nusu hivi,
nitaeleza namna kikosi changu kinavyoendelea, pia nitaweka wazi program
ya mechi za kirafiki, lakini kwa kifupi mechi za kujipima uwezo zitaanza
kufanyika mwezi wa nane”.Alisema Mwambusi.
Mwambusi
aliongeza kuwa wanatambua wazi kuwa ligi kuu ni ngumu, lakini
wanajiandaa vizuri kuhakikisha wanashindana na sio kushiriki.
Pia
kocha huyo alisisitiza kuwa yeye ana uzoezfu mkubwa na ligi ya Tanzania,
kwani aliwahi kuiongoza Tanzania Prisons kwa mafanikio makubwa, hivyo
matarajio yake ni kupata mafanikio makubwa zaidi ya yale aliyowahi
kupata akiwa na maafande wa jeshi la Magereza wa jijini Mbeya maarufu
kwa jina la wajelajela.
“Mashabiki
wawe na subira na uvumilivu, ndio kwanza timu yao inaandaliwa, lakini
nawasihi sana watuunge mkono, pale ligi itakapoanza waje kujenga
utamaduni wa kuhudhuria mechi zote kuona matunda ya kikosi chao ambacho
kwa sasa kinapiga jalamba la nguvu”.
Mbeya
City ni miongoni mwa timu tatu zilizopata nafasi ya kucheza ligi kuu
soka Tanzania bara msimu ujao, timu nyingine ni maafande wa Rhino
Rangers wa mjini Tabora na Wauza Mitumba, Ashanti United ya jijini Dar
es salaam.
Msimu
uliopita klabu za Africa Lyon ya jijini Dar es salaam, Toto Africa ya
Mwanza na Polisi Morogoro zilishuka daraja na kuzipisha timu tatu mpya.
Hapa Mbeya City walikuwa wanapambana na klabu ya Burkinfaso fc wakati wakisaka tiketi ya kupanda ligi kuu soka Tanzania bara
Picha kutoka Maktaba
No comments:
Post a Comment