Na Pamela Chilongola, Mwananchi
Kwa ufupi
- Mwaka 1971 shule hii ilijengwa bila ya kujengwa vyoo vya kudumu hivyo mimi hali hiyo nimeikuta nilikuja mwaka 2012 nimekikuta choo kilichopo hakifai kutumika hivyo tulilazimika kujenga choo cha nyasi kiweze kutumiwa na wanafunzi, huku walimu wakitumia choo kilichopo nyumbani kwangu ambayo ni nyumba ya walimu,” anasema Mahimbo.
Nilijaribu kuangaza huku na kule kutafuta choo
kilipo ili nikajisaidie mara kushoto kwangu nakutana na kibanda
kilichojengwa na nyasi huku wanafunzi wakiwa wamepanga foleni kuingia
katika kibanda hicho.
Wakati nikijaribu kutafakari mbele yangu nakutana
na mwalimu wa Shule ya Msingi ya Kibirashi iliyopo Wilaya ya Kilindi
ambaye jina lake hakutaka kulitaja anasema, hicho ni choo cha wanafunzi
ambacho wanajisaidia.
Ni miaka 42 imefika tangu Shule ya Msingi ya
Kibarashi iliyopo wilayani Kilindi Mkoa wa Tanga kujengwa mwaka 1971
ikiwa haina vyoo vya kudumu hivyo uongozi wa shule wa wakati huo
walilazimika kuchimba vyoo vya muda ili wanafunzi na walimu waweze
kutumia.
Mkuu wa Shule ya Msingi hiyo, Fatuma Mahimbo
anasema tokea mwaka 1971 shule hiyo ilipojengwa walimu na wanafunzi
wanaendelea kutumia vyoo vya muda ambavyo ni hatari kwa usalama wa
maisha yao.
Mahimbo anasema wanafunzi wapo zaidi ya 700 na
walimu wa shule hiyo wanatumia vyoo vya muda vilivyochimbwa na uongozi
wa shule hiyo.
Mahimbo anasema ameripoti shuleni hapo mwaka 2010
na kuikuta hali ya huduma ya vyoo ni mbaya, ambapo mwaka 2011 alijaribu
kuomba fedha ya ujenzi wa vyoo hivyo kwenye Halmashauri ya Kilindi na
kuelezwa kuwa mwaka huo wa fedha haijapangiwa kwenye bajeti.
““Mwaka 1971 shule hii ilijengwa bila ya kujengwa
vyoo vya kudumu hivyo mimi hali hiyo nimeikuta nilikuja mwaka 2012
nimekikuta choo kilichopo hakifai kutumika hivyo tulilazimika kujenga
choo cha nyasi kiweze kutumiwa na wanafunzi, huku walimu wakitumia choo
kilichopo nyumbani kwangu ambayo ni nyumba ya walimu,”anasema Mahimbo.
Mahimbo anasema walikaa kikao cha kamati ya shule
hiyo na kukubaliana suala hilo lipelekwe kwenye Serikali ya kijiji ili
iweze kuwasaidia.
Anaeleza baada ya kuwasilisha suala hilo kwenye
Serikali ya kijiji iliamua kujenga vyoo viwili kila kimoja kina matundu
matano. Hivyo ujenzi huo umeishia kwenye linta kutokana na Serikali ya
kijiji hicho kuishiwa fedha.
“Ujenzi huu umesimama mwaka 2012 hivyo tumekaa
kikao na wazazi na tumekubaliana kila mzazi atachangia Sh2000 kuanzia
Julai mwaka huu”anasema Mahimbo.
Mahimbo anasema kutokana na hali hiyo aliyaomba
mashirika na taasisi mbalimbali yajitokeze yaweze kusaidia ujenzi wa
vyoo vya shule ili kuokoa afya za wanafunzi ambazo zipo hatarini na hata
jamii inayowazunguka kupata magonjwa ya milipuko.
Anasema jamii haina mwamko wa elimu hawatambui
suala la kuchangia ujenzi wa choo linawahusu wao wanadhani suala hilo
ni la mwalimu mkuu hivyo wanatakiwa kuchangia fedha ili ujenzi wa vyoo
hivyo ukamilike.
Chanzo Gazeti la Mwananchi
Chanzo Gazeti la Mwananchi
No comments:
Post a Comment