Na Baraka Mpenja wa Fullshangwe Dar es salaam
Wekundu
wa Msimbazi Simba, “Taifa Kubwa” jioni ya leo wanatarajia kucheza mechi
ya kirafiki dhidi ya Kahama United katika uwanja wa Manispaa ya Kahama
mkoani Shinyanga ikiwa ni muendelezo wa mechi za kujipima uwezo katika
ziara yao ya mikoani.
Simba
wapo Kahama wakitokea mkoani Katavi ambapo walicheza mechi moja dhidi
ya Kombaini ya Katavi na kushinda bao 2-1, lakini kabla ya kwenda
Katavi, ilitokea mkoani Tabora ambapo ilipiga mechi moja ya kirafiki
dhidi ya maafande wa Rhino Rangers na kuibuka kidedea kwa mabao 3-1.
Baada
ya mchezo wa leo, Simba itaelekea Musoma mkoani Mara ambapo itapiga
mechi moja dhidi ya Kombaini ya Musoma jumatano ya julai 17.
Akizungumza na FULLSHANGWE
kwa njia ya simu kutoka Kahama, kocha msaidizi wa Simba, Jamhuri
Kiwhelo “Julio Alberto” amesema maandalzi ya mchezo huo yamekamilika, na
wachezaji wote wapo salama salimini wakisubiri muda ufike ili waende
uwanjani.
“Kwanza
namshukuru Mungu mwingi wa rehema, ametupa uzima hapa Kahama, wachezaji
wote na viongozi wapo salama kabasi, tunasubiri muda wa mechi ufike ili
tukacheze huko”. Alisema Julio.
Picha kwa Hisani ya www.Globalpublisher.infor
Julio
aliongeza kuwa kikubwa ambacho mashabiki na wanachama wa Simba
wanatakiwa kuelewa kwa sasa ni kuwa benchi la ufundi linaijenga timu
upya kwa ajili ya mashindano ya siku zijazo.
“Kila
mchezo kwetu ni muhimu sana kwasababu tunautumia kuangalia mabadiliko
ya kikosi na mapungufu yako wapi na kuyafanyia kazi, kwahiyo muendelezo
huu wa mechi za kirafiki unatupa nafasi ya kujua nini cha kufanya”.
Alisema Julio.
Pia
kocha huyo msaidizi wa Simba aliongeza kuwa kwa sasa kikosi chao
kinaimarika kwa kila mechi, huku kocha mtaalamu, Abdallah King Kibaden
Mputa akionesha ufundi mkubwa wa kuwafanyisha mazoezi wanandinga wao na
kuwapa vitu adimu kiutalaamu.
“Simba
ina kocha mahiri na mtaalamu, Alhaji kibadeni, huyu mwalimu ana mambo
adimu sana, lazima niwahakikishie mashabiki wetu kuwa Simba ya sasa
iatakuwa tishio na hao mnaowaita wakali waleteni msimu ujao, mtaona
shughuli ya Mnyama”. Alisema Julio.
Msimu
uliopita Simba walikuwa wanatetea ubingwa wao, lakini waliishia nafasi
ya tatu, huku nafasi ya pili ikichukuliwa na wana lambalamba Azam Fc, na
ubingwa ukitwaliwa na wazee wa Uturuki, wazeee wa sambusa, Kwalalumpa
Malysia, Dar Young Africans chini ya kocha wake Mholanzi Ernie Brandts.
Picha kwa Hisani ya www.Globalpublisher.infor
Kocha
mkuu wa Simba, Abdallah King Kibaden Mputa, msimu uliopita aliibuka
kocha bora akiwa na kikosi cha Kagera Sugar, msimu ujao ataiongoza Simba
………
Ili
kuhakikisha wanarudisha ubingwa wao, Simba wameanza ziara yao mikoani na
wataenda mpaka Kenya ili kukisuka upya kikosi chao, pia wapo makini
sana na usajili na hivi majuzi wamemsainisha mkataba wa miaka miwili
alyekuwa mfungaji bora wa michuano ya kombe la Kagame iliyofanyika
nchini Sudan , Amis Tambwe ambaye alikuwa anaichezea Vital`O ya Burundi.
Nao
Yanga walikuwa na ziara ya mikoani ambapo walianzia mikoa ya Kanda ya
ziwa na kucheza mechi mbili za kirafiki kati ya KCC ya Uganda. Mechi ya
kwanza walicheza CCM kirumba na kutoka sare ya 1-1 na mechi ya pili
walirudiana uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga na Yanga kulala kwa
mabao 2-1. Mechi ya mwisho walipiga Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora na
kutoka suluhu ya bila kufungana na wenyeji wao Rhino Rangers.
Sasa Yanga wapo Dar es salaam wakiendelea na mazoezi kwa uzuri kabisa.
No comments:
Post a Comment