Pages

Sunday, August 18, 2013

HII HAPA LIST YA VIGOGO WAKUBWA AMBAO NI VINARA WA UVAMIZI WA ARDHI


Getrude Lwakatare

 


WAMO DEWJI, LWAKATARE, RUTABANZIBWA

 
WABUNGE Mohamed Dewji wa Singida mjini na Mchungaji Getrude Lwakatare wote wa CCM pamoja na mfanyabiashara maarufu jijini Dar es Salaam Robery Mugishagwe wametajwa kuwa vinara wa uvamizi na uuzaji wa viwanja jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Patrick Rutabanzibwa, naye ametajwa kumkingia kifua mmoja wa wavamizi wa viwanja kwa kumuwekea dhamana alipofikishwa polisi.
Waziri wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk. Tereza Huviza ndiye aliyewataja vigogo hao jana jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza na wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Maliasili, Ardhi na Mazingira, iliyokwenda kutembelea ofisi za Baraza la Mazingira (NEMC).
Huvisa alikuwa akihofia kutaja majina ya vigogo hao, lakini Mwenyekiti wa kamati hiyo, James Lembeli, alimkasirikia na kumhoji ni nani hapa nchini aliye juu ya sheria kiasi cha kumfanya aogope kumtaja licha ya kuvunja sheria.
Lembeli alimtaka Waziri Huvisa kuyataja majina hayo kwani akiendelea kuwahofia watu wa aina hiyo, wataendelea na uvamizi huo na watakapofika 100 wenye tabia hizo nchi haitatawalika.
“Huna sababu ya kuogopa kuwataja watu waovu, kamati hii ina mamlaka kisheria…usihofie chochote, wataje tujue namna ya kuwashughulikia,” alisema Lembeli.
Shinikizo hilo la Lembeli liliungwa mkono na wajumbe wote wa kamati hiyo waliomuhakikishia usalama Waziri Huvisa aliyeonekana kuwa na hofu wakati akiulizwa maswali.


Baada ya kuhakikishiwa usalama, alianza kumtaja Dewji ambaye alisema anashinikiza kupewa eneo la ufukwe karibu na zilipo ofisi za ubalozi wa Urusi hapa nchini huku akijua ni kinyume cha sheria.
Waziri huyo alisema vielelezo walivyonavyo wizarani vinaonyesha kwamba Dewji alikinunua kiwanja hicho mwaka 1995, lakini kwa kuwa eneo hilo liligundulika kuwa na mikoko, Rais Benjamin Mkapa alifuta rasmi hati yake mwaka 1998.
Alibainisha kuwa baada ya kufutwa kwa hati ya kiwanja hicho, mbunge huyo alipeleka maombi tena wizarani ambako alikumbushwa namna kilivyotenguliwa, lakini bado akawa king’ang’anizi kwa kumtumia watu na baadhi ya wabunge.
Waziri Huvisa alisema miongoni mwa wabunge waliotumika kushawishi Dewji arejeshewe kiwanja hicho ni pamoja na Diana Chilolo (Viti Maalumu - CCM). Hata hivyo hadi sasa hawajafanikiwa.
“Mimi nimeendelea na msimamo wa kumkatalia Dewji. Kiukweli ndugu zangu wenye watu wenye nguvu kifedha na madaraka ndio wanaochangia mambo kutokwenda sawa kwenye sekta ya ardhi,” alisema.
Nyumba ya Lwakatare
Katika mkutano huo, pia suala la kubomolewa kwa nyumba ya Mbunge wa Viti Maalum, Mchungaji Lwakatare lilizusha majadala mkubwa. Wajumbe wa kamati hiyo walimbana Waziri Huvisa ili azungumze kwanini hajabomolewa.
Hata hivyo, Waziri Huvisa alisema hawezi kulizungumzia jambo hilo kwa kuwa kesi yake ipo mahakamani na anashangazwa na danadana za kesi hiyo kila inapotajwa kwa ajili ya kusikilizwa.
Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya (CCM), alisema kuwa jengo la mbunge Lwakatare limekuwa likilalamikiwa na wananchi kwa kutobomolewa hali inayotoa tafsiri ya upendeleo wa kimatabaka.
Wengine watajwa
Waziri Huvisa pia alimtaja mfanyabiashara maarufu Mugishagwe, aliyetakiwa kubomolewa jumba lake maeneo ya Kawe, lakini kushindikana baada ya Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rutabanzigwa, kuingilia kati na kumuwekea dhamana.
Alisema wizara yake imeshindwa kubomoa nyumba ya mfanyabiashara huyo kwa kuwa alipokamatwa na polisi, Rutabanzibwa alimwekea dhamana jambo lililozua utata.
Waziri huyo alisema kutokana na dhamana hiyo, hivi sasa anafanya taratibu za kukutana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Anna Tibaijuka walizungumze.
Alisema kutobomolewa kwa nyumba ya Mugishagwe kumesababisha malalamiko kwa wananchi ambao nyumba zao zilibomolewa katika maeneo kama aliyojenga mfanyabiashara huyo.
Wataka mahakama za mazingira
Wajumbe wa kamati hiyo wakichangia hoja mbalimbali za kuboresha uendeshaji wa NEMC, walitaka kuanzishwa kwa mahakama ya mazingira kwa kuwa sheria zinaonekana kukinzana inapotokea kesi ya mazingira.
“Hadi sasa tayari tuna Mahakama ya Ardhi na ile ya Kazi, kwa nini tusione ni wakati wa kuwa na Mahakama ya Mazingira ili kuepusha mlolongo wa kuendesha kesi zinazohusu mazingira?” alihoji Mbunge wa Magomeni Zanzibar, Mohamed Amour Chomboh.
Mbunge Viti Maalumu, Suzan Kiwanga (CHADEMA) alisema rushwa miongoni mwa watendaji wa serikali imekuwa kikwazo cha utunzaji wa mazingira na kushauri kwamba ili kujenga kizazi kitakachothamini mazingira, elimu itolewe kuanzia shule za awali.
Naye Mkurugenzi wa NEMC, Dk. Boniveture Baya, alizitaja baadhi ya changamoto wanazokumbana nazo ni pamoja na kutoeleweka vizuri kwa usimamizi wa sheria kwa watendaji na wananchi.
Alisema wakati mwingine wamekuwa wakishindwa kesi kutokana na watendaji wao kukurupuka kutoa uamuzi kwa sababu ya kutozifahamu vizuri sheria.
Aliitaja changamoto nyingine ni mwingiliano wa sheria na wizara ambazo wamekuwa wakifanya nazo kazi, ambako kila moja inatoa kibali kwa wakati wao hivyo inapokuja suala la mazingira unakuta linawadondokea wao.
Rasilimali fedha nayo imetaja kuwa kikwazo kwao kwani hii huwafanya kushindwa kwenda kufanya ukaguzi maeneo mbalimbali na kubomoa majengo ambayo yamejengwa kinyume na taratibu ikiwemo hoteli ya Coco Beach, ambayo hadi sasa ipo kutokana na kokosa fedha za kuibomoa.
Pia alionekana kukerwa na kutokuwepo kwa mfumo mahususi kwa ajili ya utupaji wa taka ngumu za viwandani hususani katika Jiji la Dar es Salaam ambako kutokana na kujisimamia wenyewe kwa sasa wamekuwa wakikiuka sheria za mazingira.
Chanzo Tanzania daima

No comments:

Post a Comment