Pages

Monday, August 12, 2013

MAJAMBAZI WAMTEKA DIWANI MKOANI KAGERA...!!




DIWANI wa Kata ya Chonyonyo (CCM) wilayani Karagwe, Arnold Rweshekerwa, amenusurika kuuawa na kundi la majambazi waliomteka nyara katika eneo la Kyanyamisa kabla ya kuwatoroka akiwa amewafungia ndani ya gari lake katika Pori la Kimisi.

 Tukio hilo limetokea siku chache tangu Rais Jakaya Kikwete, atoe siku 14 kwa majambazi katika mikoa ya Kagera, Geita na Kigoma kusalimisha silaha na kuacha vitendo hivyo kabla ya msako wa nyumba kwa nyumba kuanza.

Pia agizo hilo la Rais Kikwete liliwahusu wahamiaji haramu waliopo katika mikoa hiyo kuwa wameondoka ndani ya kipindi hicho.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana mjini hapa na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera, Phillip Kalangi, tukio hilo lilitokea Agosti 10, mwaka huu saa 2.00 katika eneo lenye kibao kinachoonesha sehemu ya hifadhi ya akiba katika pori la Kimisi kuelekea wilayani Ngara.

Baada ya kunusurika kuuawa na majambazi hayo, waliteketeza gari la diwani huyo kwa kitu kinachodhaniwa bomu. Habari hizo zinaeleza kuwa, Diwani huyo alikuwa ameenda Kijiji cha Kyanyamisa kumtembelea bibi yake mzaa mama, ambapo wakati akirudi nyumbani alikutana na watu wawili njiani, wakiwa na bastola, ambapo baada ya kumsimamisha walimtaka ageuze gari kurudi alikokuwa anatoka.

Wakati wa harakati za kugeuza gari hilo, huku majambazi hao wakiwa wamekaa ndani ya gari lake hilo alikutana na watu wengine tena.

Alisema watu hao walikuwa na mifuko minne iliyojaa bunduki, magazine na risasi, ambapo akiwa anawaendesha kwenye gari lake, watu hao walikuwa wanaingiza risasi kweye magazine.

Walipofika mbali jirani na hifadhi ya akiba walimwamuru diwani huyo kusimamisha gari na kuzima taa, huku wakiendelea kuingiza risasi kwenye magazine kwa tochi.

Wakiwa katikati ya Pori la Kimisi alifunga milango ya gari kisha kuruka kwa kupitia dirishani kutokomea porini.

Habari hizo zinaeleza kuwa diwani huyo alitembea zaidi ya kilomita mbili akirudi Karagwe, ambapo aliona pikipiki moja ikiwa na watu wawili wenye silaha wakitokea Kyanyamisa kwenda Ngara.

Inadaiwa alishindwa kuwasimamisha kwa kuhofia huenda wakawa ni wenzao, wakati alipokuwa ametekwa aliwasikia wakiwasiliana na watu wengine.

Baadaye alipata usafiri wa Hiace iliyokuwa ikitoka Benako wilayani Ngara saa 3.30. Alipanda gari hilo ambapo alianza kuwasimulia abiria kilichotokea. Habari zaidi zilieleza kuwa abiria hao walimwambia kuwa waliona gari likiteketea kwa moto.

Kamanda Kalangi alisema; “Tukio hilo lipo na gari limeteketezwa kweli, lakini suala la utekaji wa diwani huyo, inakuwa ngumu kulithibitisha kwani wakati likitokea, alikuwa peke yake.

Katika tukio , watu hao hawakuweza kumdhuru diwani huyo, bali walimpora simu, sh.100,000 na viatu vyake alivyokuwa amevaa.

Diwani huyo amelazwa Hospitali Teule ya Nyakahanga baada ya kupoteza fahamu


No comments:

Post a Comment