Alisema mizigo ikishaondoka mikononi mwa abiria
hukaguliwa tena kwa kutumia mbwa wa Idara ya Usalama wa Taifa, lakini
siku ya tukio hilo mbwa hao walichelewa na walitumika baada ya mizigo
kuingizwa kwenye masanduku ya chuma.
“Kwa abiria watatu kuwa na mabegi makubwa tisa
yanayofanana si kitu cha kawaida kukwepa jicho la maofisa wa ushuru wa
forodha na vyombo vya usalama, sijui walikuwa wapi siku hiyo?” alihoji
Mwakyembe.
Juzi waziri huyo aliahidi kuyaweka hadharani
majina ya watu wanaosafirisha dawa za kulevya nchini, na alitekeleza
ahadi hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari, kusema kuwa
watu hao wamenaswa baada ya mfumo wa kamera (CCTV) za uwanja huo kudaka
matukio kadhaa yaliyotokea siku ya tukio hilo, kuanzia saa 9:25 hadi saa
10:30 alfajiri.
Ameagiza wafanyakazi hao wanne pamoja na askari
polisi mwenye cheo cha koplo, mbeba mizigo na mfanyabiashara aliyekuwa
na wasichana wawili waliokamatwa Afrika Kusini, (ambao hatuwezi kuwataja
kutokana na kushindwa kuwapata kujieleza) kuchukuliwa hatua za
kinidhamu, kukamatwa na kuunganishwa na watuhumiwa waliokwenda na mzigo
huo Afrika Kusini.
Mabegi hayo yaliyokuwa na dawa za kulevya aina ya
‘Crystal Methamphetamine’, yalipitishwa na wasichana wawili wasanii
aliowataja kuwa ni Agnes Gerald ‘Masogange’ na Melisa Edward ambao
walidakwa siku hiyohiyo katika Uwanja wa Ndege wa Oliver Tambo, Afrika
Kusini na tayari wameshafikishwa mahakamani.
Juzi Dk Mwakyembe alifanya ziara JNIA kukagua
utendaji kazi kwenye uwanja huo ikiwa ni siku tatu baada ya ahadi
aliyotoa akiwa Mwanza kwamba katika kipindi cha wiki mbili, atahakikisha
anawakamata vigogo wote walio katika mtandao wa usafirishaji na
uingizaji wa dawa za kulevya kupitia viwanja vyote vya ndege nchini.
Saa nane baada ya ziara hiyo, Maofisa wa Mamlaka
ya Viwanja vya Ndege wanadaiwa kumkamata Edwin Monyo akiwa na kete 86 za
dawa aina ya heroini na misokoto 34 ya bangi aliyokuwa akiisafirisha
kwenda Italia kupitia Zurich.
Mpango ulivyosukwa
Alisema siku ya tukio saa 9:28 kamera hizo za
usalama zilimwonyesha mbeba mizigo wa uwanja huo akiwa anazungukazunguka
eneo la kuingilia abiria kama mtu ambaye ana ahadi na kukutana na mtu
fulani.
“Kamera pia zilimnasa ofisa mwingine wa TAA kwa
mara kadhaa akitoka na kuingia ndani ya jengo la abiria huku akizungumza
na simu, kitendo ambacho hakiruhusiwi kabisa kwa wafanyakazi wa eneo la
ukaguzi wa abiria,” alisema na kuongeza;
“Wakati huohuo, kamera zilikuwa zinamwonyesha
askari polisi anayetuhumiwa kuhusika katika mpango huo akiwa
anarandaranda eneo la uhakiki wa hati za kusafiria kama vile anasubiri
kitu fulani.”CHANZO http://www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment