Mwanamuziki
mkongwe wa bendi ya Msondo Ngoma Mzee Muhidin Gurumo (katikati)
akizungumzia kustaafu rasmi kazi ya muziki aliyoifanya kwa muda wa miaka
53 katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo jijini Dar es Salaam leo.
(Picha na Magreth Kinabo).
Mwanamuziki
mkongwe wa bendi ya Msondo Ngoma Mzee Muhidin Gurumo amestaafu rasimi
kazi ya muzika alioifanya kwa muda wa miaka 53.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mzee Gurumo mwenye
umri wa miaka 73 amesema ameamua kustaafu kazi hiyo kwa hiari yake
mwenyewe kutokana na umri wake kuwa mkubwa.
Mzee
Gurumo amesema “Muziki kwangu umekuwa kama asili yangu na kazi yangu
lakini nimeamua kustaafu kutokana na umri wangu na nitabaki kuwa mshauri
tu kwa mwanamuziki yeyote atakayetaka ushauri wangu” .
Pamoja
na kufanya kazi ya muziki Gurumo amesema kuwa hakupata mafanikio
makubwa zaidi ya kujenga nyumba anayoishi na familia yake.
Amesema
ameimba kwa muda mrefu sana lakini hata baiskeli hana, hata hivyo Mzee
Gurumo akasema anashukuru kuwa ana nyumba ya kuishi na familia.
Vilevile
Mzee Gurumo amewaasa vijana kuwa wabunifu na kuupenda mziki wa zamani,
kwani ndio chimbuko la bongo fleva na kuwashauri wanamuziki wa sasa kuwa
wavumilivu kukaa muda mrefu kwenye bendi moja ili hata wanapoondoka
mchango wao uthaminiwe.
Mzee
Gurumo ambaye ana mke na watoto wanne amesema kuwa katika maisha yake
ya muziki alifanikiwa kutunga nyimbo 60,000 na anavutiwa zaidi na
mwanamziki Hussein Jumbe na Hassani Rehan Bichuka na kwa wanamuziki wa
kizazi kipya anavutiwa na Nassibu Abdul ’Diamond’.
Mwanamuziki
huyo mkongwe alianza kufahamika katika tasnia ya muziki wa dansi kwenye
miaka ya 1960, ambapo mwaka 1964 alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa
bendi ya Mlimani Park.
Alidumu
na Mlimani Park mpaka mwaka 1985 na kuhamia Safari Sound, aliyofanya
nayo kazi mpaka mwaka 1990 na kujiunga na Msondo Ngoma mpaka sasa
anaamua kustaafu Muziki.
No comments:
Post a Comment