Pages

Tuesday, September 10, 2013

HUU NDIO UTAJIRI WA MAREHEMU ASKOFU KULOLA


Mashaka Baltazar, Mwanza na Haruni Sanchawa Dar
NI maswali tata yameibuka baada ya mazishi ya aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Evengelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT), Dk. Moses Samuel Kulola (85) kwamba, ameacha utajiri wa kiasi gani wakati wa uhai wake, Uwazi limechimba.
Ghorofa la Marehemu Kulola lililopo Mwanza.
Baadhi ya waombolezaji msibani jijini Mwanza walikuwa wakiulizana kama marehemu Kulola ameacha utajiri wa mali na fedha wa kuweza kuwafikia baadhi ya watumishi wa Mungu waliopo leo Tanzania?
Musa Salum yeye ni Mchungaji wa Kanisa la Anglikana la Mji Mwema, Mwanza anaweka wazi kuwa alimfahamu marehemu Kulola miaka 27 iliyopita, kwamba hakuwa mtu aliyetaka kumiliki mali.
Toyota Prado New Model.
Akizungumza na Uwazi baada ya mazishi, mchungaji huyo alisema marehemu Kulola ambaye hakuwahi kujiita nabii bali mwinjilisti, katika maisha yake alijitolea kuhubiri Neno kwa nia ya kuwapeleka watu kwa Mungu na si kwa kutafuta utajiri na maisha ya anasa.
Alisema anavyojua yeye, kwa kutumia kipato chake kilichotokana na utumishi wake serikalini na baadaye uchungaji, mwaka 1970 marehemu alijenga nyumba moja ya kawaida ya kuishi ambayo ipo Capri Point, jijini Mwanza.
“Kwanza nyumba yenyewe ni ya kawaida sana, kwa kipato chake asingeshindwa kujenga nyumba kama hiyo, ila kwa utumishi wake uliopata kibali kwa Mungu asingeshindwa kujenga kubwa na ya kisasa zaidi,” alisema mchungaji huyo ambaye ni mmoja wa majirani  wa marehemu.
Nyumba ya Marehemu Askofu Moses Kulola (kushoto) iliyopo Chanika.
Jijini Dar mwandishi wetu alifika Chanika, wilayani Ilala ambako pia Askofu Kulola anasemekena kujenga makazi yake.
Nyumba hiyo ni ya kawaida katika eneo hilo kitu ambacho si rahisi watu kuamini kwamba ni ya mtumishi wa Mungu na shujaa wa Injili Tanzania kama Moses Kulola. 
Gazeti hili lilizungumza na baadhi ya majirani zake kuhusu uhusiano wao na marehemu hasa ikizingatiwa kuwa eneo hilo limezungukwa na waumini wa dini ya Kiislamu.
Ally Suleiman: Natamani viongozi wote wa dini katika nchi  hii wangekuwa kama Askofu Kulola kwa sababu hakuwa na makuu, alikuwa akishirikiana na sisi bila ubaguzi, hakika hafanani hata chembe na wachungaji au maaskofu wengine.
Nyumba ambazo bado zinajengwa Chanika.
Kwa upande wa usafiri, tofauti na baadhi ya maaskofu au wachungaji wanaovuma siku hizi wakidaiwa kumiliki magari ya kifahari, marehemu Kulola enzi za uhai wake alimiliki magari mawili tu ambayo kidogo yana hadhi ya juu kiasi  cha watu kuhoji aliyanunuaje kama kweli hakujilimbikizia utajiri?
Habari zinadai kuwa, magari hayo yote alipewa na Kanisa la EAGT kwa miaka mbalimbali baada ya kuona mtumishi huyo hana usafiri wa maana.
Awali alipewa gari aina ya Toyota Land Cruiser VX (thamani yake haikujulikana) ambalo alilitumia mpaka lilipoanza kuchoka. Novemba  mwaka jana alipewa Toyota Prado New Model lenye namba za usajili T 164 CED likiwa na thamani ya shilingi 80,000,000 ambalo alilitumia mpaka mwisho wa uhai wake.
Toyota Land Cruiser VX kama aliyokuwa akimiliki Kulola.
Magari hayo kwa sasa yameegeshwa nyumbani kwake Mwanza kwa kusubiri taratibu nyingine za kifamilia, hasa mambo ya mirathi.
Mambo mengine ni kwamba, imeelezwa katika maisha yake ya utumishi wa Mungu, marehemu Kulola aliwahi kutembea kwa miguu kutoka jijini Mwanza hadi Singida na baadaye Manyara kwa lengo la kuhubiri Neno.
Hali hiyo ilijidhihirisha pia alipokuwa mkoani Mbeya ambapo alilazimika kutembea kwa miguu kutoka mjini hadi Songea, mkoani Ruvuma kuhubiri Injili.
Mtoto mkubwa wa marehemu ambaye hakutaka kutaja jina lake alipoombwa na gazeti hili kutoa ufafanuzi kama marehemu baba yake alikuwa ni tajiri kupindukia kama ilivyo kwa baadhi ya maaskofu wengine, hakuwa tayari akidai huko ni kuivua nguo familia.
Marehemu Askofu Moses Kulola.
“Sitaki kuingia kwenye mgogoro na familia yangu ambayo kwa sasa imetulia. Kuzungumzia mambo hayo ni sawa na kujivua nguo ukizingatia kwamba magazeti mengi yameandika,” alisema mtoto huyo bila kufafanua.
Kwa mujibu wa wasifu wa kiongozi huyo wa kiroho uliosomwa wakati wa mazishi yake Jumatano wiki iliyopita, marehemu Kulola, aliwahi kunusurika kuuawa mara 20, kati ya hizo  mara tatu ni kwa silaha za jadi na nyingine ni kwa ajali za kutegeshewa.
Askofu Moses Kulola alifariki dunia Agosti 29, mwaka huu kwenye Hospitali ya Ami, jijini Dar na kuzikwa kwenye kaburi lililochimbwa katika kiwanja cha Kanisa la EAGT, Bugando, Mwanza.
Mungu ailaze pema peponi, roho yake. Amina.

No comments:

Post a Comment