CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimempuuza Katibu wa
Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, Nape Nnauye, kikisema kuwa madai yake
yanalenga kuhamisha wananchi kwenye hoja.
Mkurugenzi wa Mawasiliano na Habari wa CHADEMA, John Mnyika, amesema
kuwa madai hayo ya Nape yanadhihirisha kile alichowahi kukisema bungeni
kuwa nchi imefika hapa ilipo kutokana na upuuzi wa CCM.
Kauli ya CHADEMA inafuatia madai yaliyotolewa na Nape juzi mjini
Kahama, mkoni Shinyanga juzi kwenye mkutano wa hadhara kuwa chama hicho
kupitia kwa katibu mkuu wake kilipewa fedha na wafadhili nje ya nchi ili
kuvuruga mchakato wa Katiba unaoendelea sasa.
Mnyika alisema kuwa ameshangazwa na madai hayo ya Nape ambayo aliyaita
ya kipuuzi kutolewa mbele ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.
“CCM kupitia Nape imetoa madai hayo kwa lengo la kuhamisha mjadala
kutoka kwenye muswada mbovu wa sheria ya marekebisho ya Katiba
uliopitishwa kwa nguvu bungeni,” alisema.
Alisema kuwa Katibu wao Mkuu, Dk. Willibrod Slaa, hajawahi kupewa
fedha zozote nje ya nchi kwa ajili ya kukodi helikopta ili kuvuruga
mchakato wa Katiba kama alivyodai Nape.
Aliongeza kuwa katika tukio hilo kanuni za Bunge zilivunjwa na Naibu
Spika, Job Ndugai, hivyo kuathiri hadhi na heshima ya Bunge kwa kuruhusu
wabunge kushambuliwa, kudhalilishwa na kuhamishwa bungeni na watu
wasiohusika.
Mnyika alihoji kuwa kwenye udhaifu kama huo wa kiti cha spika kwa
maelekezo ya CCM inawezekanaje CHADEMA kuvuruga mchakato huo
unaoendeshwa kimizengwe licha ya wao kuwa waasisi wa hoja ya Katiba
mpya.
“Madai ya CCM kupitia Nape ni ya kipuuzi na yanalenga kuwakatisha
tamaa wananchi juu ya kazi inayofanywa na CHADEMA ya kuunganisha nguvu
ya umma wa Watanzania dhidi ya udhaifu wa rais na uzembe wa Bunge
linalohodhiwa na CCM katika mchakato wa Katiba mpya,” alisema.
Aliongeza kuwa CCM inalenga kurudisha nyuma Watanzania kwenye uamuzi unaosubiliwa kwa hamu.
Mnyika aliongeza kuwa CCM ilikataa kuandika Katiba mpya mbali ya
Watanzania kuidai kwa nyakati tofauti na kuzimwa mpaka CHADEMA
iliposhinikiza kupitia wabunge wake kutoka bungeni.
Kwamba baada ya kuandaa maandamano ndipo rais akakubali mchakato wa Katiba mpya uanze.
“CCM haikuwa na sera ya kuanzisha mchakato wa Katiba mpya, haina
uhalali wa kimaadili wa kuinyooshea kidole CHADEMA iliyokuwa na sera ya
Katiba mpya kwa madai ya kutumwa na mataifa ya nje kukwamisha mchakato
huo,” alisema.
Mnyika alisema kuwa CCM imetoa msimamo na ufafanuzi wa maoni ya
kupinga mazuri kwenye rasimu ya Katiba mpya. Kwamba inashangaza badala
ya kuboresha mchakato wa kupata Katiba mpya yenyewe inataka
kuuchakachua.
“Baada ya kushindwa kufanya hivyo kupitia mabaraza ya Katiba
yaliyosimamiwa na Tume ya Marekebisho ya Katiba na mabaraza ya wazi
yalioendeshwa na CHADEMA mengine kwa helikopta na mengine bila helikopta
katika maeneo mbalimbali nchini, imeanza kuhadaa watu.
“Mbinu iliyobaki sasa kwao ni kuichakachua kwenye Bunge Maalumu la
Katiba kwa kupenyeza watu wake kupitia kumpa rais mamlaka makubwa kwenye
kuteua wajumbe 166 na pia kufanya uamuzi upite kwa wingi wa kura,”
alisema.chanzo http://freemedia.co.tz
|
No comments:
Post a Comment