Septemba 18,2013-Jumatano. BAADA ya siku
chache wavuti hii(http://www.fahamutz.com) kuripoti juu ya tamko la
Waziri Mwakyembe kutaka uongozi wa Mamlaka ya Bandari (TPA) kutaja
majina ya wezi wa mafuta toka bomba kuu la serikali, imebainika kuwa
vigogo wa serikali akiwemo mbunge mmoja wa CCM wanadaiwa kumiliki vituo
vya mafuta, kando kando ya Bahari ya Hindi wametajwa kuwa vinara wa
hujuma na wizi wa mafuta kwenye bomba kubwa la TPA.
Akizungumza na mwandishi wetu jana kwa
sharti la kutotajwa jina lake, mmoja wa wafanyakazi wa kituo cha mafuta
kilichoko kandokando ya Bahari ya Hindi alikiri kuwepo kwa hujuma hiyo
hasa kwa vituo vya mafuta.
Alisema kuwa baadhi ya vigogo hao wamekuwa
wakifanya hujuma hiyo kwa kuunganisha mabomba yao pale TPA inapokuwa
ikipakua mafuta hayo. “Yaani Dk. Mwakyembe kama amechelewa
ninavyokwambia hapa kuna kile kituo cha mafuta ninachofanyia kazi (jina
linahifadhiwa) ambacho kinamilikiwa na mbunge mmoja wa Chama cha
Mapinduzi (CCM) kinacheza huo mchezo sana tu huu karibia mwaka wa tatu,”
alisema
Alisema kuwa mbali na kuunganisha mabomba
vituo hivyo vimekuwa vikipakua mafuta hayo na kuyajaza katika magari na
kisha kusafirisha katika vituo vingine vikiwemo vya mkoani. Chanzo cha
habari kimesema kuwa kwa utaratibu, mafuta yakishapakiwa katika magari
hayo yasisafirishwe siku hiyo lakini vituo hivyo vimekuwa vikisafirisha
kuhofia kukamatwa.
“Niwaombe mjipange na kama mtakuwa na muda
mje majira ya saa 12:30 au saa 1:30 usiku wakati kumetulia siku za
Ijumaa na Jumamosi ambapo hujuma hiyo ndiyo hufanyika,” alisema.
Hata hivyo wavuti ilimtafuta kigogo
aliyetajwa katika hujuma hiyo ambaye hakuwa tayari kupokea simu wala
kujibu ujumbe mfupi wa mkononi aliotumiwa na mwandishi wetu.
Siku ya Ijumaa iliyopita Dk. Mwakyembe
alisema kuwa anaamini kuwa watu hao wanafahamika kwa kuwa si rahisi
hujuma kama hiyo kufanywa na mtu asiyekuwa mtaalamu wa sekta hiyo na
kuamuru watajwe majina yao haraka .
Dk. Mwakyembe alisema wezi hao bila hofu
wamejaribu kulitoboa bomba hilo kubwa ambalo limeigharimu serikali
mamilioni ya shilingi na kuunganisha mabomba yao chini kwa chini kisha
kunyonya mafuta hayo hadi kwenye stesheni zao za kuhifadhia
mafuta. Alisema kuwa wezi hao wamekuwa wakiibia serikali lita 35,000
hadi 40,000 katika kipindi kisichojulikana kitendo ambacho ni sawa na
uhujumu uchumi.
“Tiper ndio vinara wa wizi huo hivyo
naagiza kuvunja mkataba, pia muwalete ili waje wawataje waliohusika na
wizi huo, kwani umefanywa kitaalamu pia nasikia kuna Mzungu ambaye
amezoea kutoa rushwa lakini kwa hili naamini watarudi kwao Ulaya,”
alisema na kuongeza:
“Baada ya wizi kupungua kwenye Mamlaka hiyo
Bandari nawapongeza sana lakini wapo watu ambao si waaminifu, wamebuni
mbinu mpya za kuihujumu serikali kwa kutumia mbinu nyingine,” alisema
Dk. Mwakyembe. Alisema kuwa alimfahamisha Waziri wa Nishati na Madini
Sospeter Muhongo juu ya hujuma hiyo inayofanywa na kampuni hiyo ya
Tiper, kitendo ambacho kilimsononesha.CHANZO
NI:http://www.fahamutz.com/2013/09/vigogo-wa-serikalimbunge-watuhumiwa.html Mwandishi : Margreth Itala.
No comments:
Post a Comment