Pages

Monday, September 30, 2013

Neno La Leo: Zitto, Katiba na Meza...

zitoo_e9191.jpg
Ndugu zangu,
Kwenye andiko lake; " Katiba Ni Mwafaka wa Kitaifa- Viongozi Zungumzeni"
Mheshimiwa Zitto Kabwe anaandika...
"Kutosaini muswada huu kunaweza kuleta mgongano kati ya Wabunge wa CCM na Rais. Hata hivyo Rais lazima aweze kushawishi chama chake kwamba umoja wa kitaifa ni muhimu ziadi kuliko maslahi ya kisiasa ya chama chao."
Na hapa ndipo panapomfanya Rais Jakaya Kikwete na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi kuwa ndiye Mtanzania pekee kwa sasa anayeweza, kwa atakavyolikabili suala hili, kuamua kwa kiasi kikubwa, mustakabali wa nchi yetu. Na kihistoria, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi ni mtu mwenye nguvu na ushawishi mkubwa kimaamuzi.
Tusingependa Rais wetu, na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi afikishwe kwenye ' kuangukiwa na jumba bovu' kwa wengine kumshinikiza huku wakitanguliza zaidi maslahi yao binafsi kuliko ya NCHI.
Na ndipo hapa unakuja umuhimu wa MEZA kwa maana ya mazungumzo. Hakuna namna yeyote ile ya kumaliza tofauti zilizopo juu ya Katiba bila kutumia njia ya mazungumzo na bila kutambua nafasi ya Rais katika kufikia muafaka.
Na nimepata kuandika, kwamba kawaida ya wanadamu hawazungumzi kulimaliza jambo wakiwa wamesimama. Huitafuta MEZA. Ndio, meza ya mazungumzo. Yaweza kuwa meza ya duara au mstatiri, lakini, lililo muhimu ni MEZA.
Kabla ya ujio wa Wareno hatukuwa na neno meza. Hili ni neno la Kireno, linatamkwa ' Mesa'.
Ni imani yangu, ni imani ya wengi pia, kuwa viongozi wa kisiasa wataacha jazba na ubinafsi, badala yake kutangulizambele maslahi mapana ya nchi yetu.
Ndio, zifanyike jitihada za kukutana na kuzungumza. Hivyo basi, nikiwa kama mwandishi na Mtanzania, naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Zitto Kabwe. Juu ya umuhimu wa MAZUNGUMZO.
Maggid.
Msamvu, Morogoro.
0754 678 252

No comments:

Post a Comment