Mtoto
Kudra aliyekuwa ameunganika na kiwiliwili cha pacha mwenza, anaendelea
vizuri na matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Mtoto
huyo alifanyiwa upasuaji Alhamisi iliyopita katika Taasisi ya Mifupa ya
Muhimbili (Moi) na kulazwa katika wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi
maalumu (ICU), lakini mwishoni mwa wiki iliyopita alitolewa katika wodi
hiyo.
Mama
mzazi wa mtoto huyo, Pili Hija, alisema hivi sasa Kudra ananyonya vizuri
na kwamba amekuwa akitaka kufanya hivyo kila wakati .
"Kwa
kweli kudra za Mwenyezi Mungu ndizo zimemweka hai mpaka leo hii,
nilikuwa nimeshakata tamaa kuwa nampoteza mwanangu, nazidi kumuomba
Mungu amwekee mkono wake apone kabisa," alisema Hija.
Daktari
Bingwa wa Upasuaji wa Watoto katika Hospitali ya Muhimbili, Dk Zaitun
Bokhary, alisema mtoto huyo anaendelea vizuri na mwishoni mwa mwezi huu
atafanyiwa upasuaji mwingine.
"Tunamwacha
achangamke kwanza, mwishoni mwa mwezi huu tutamfanyia upasuaji mwingine
wa kumwekea njia ya muda ya kutolewa haja kubwa, kwa kumpasua ubavuni
baada ya hapo ataruhusiwa kwenda nyumbani," alisema Dk Bokhary.
Kudra
alipewa jina hilo Alhamisi usiku, saa kadhaa baada ya upasuaji kufanyika
chini ya jopo la madaktari saba, walioongozwa na Dk Hamis Shaaban,
mtaalamu wa Ubongo na Uti wa Mgongo kutoka Moi.
Alizaliwa
Agosti 18, baada ya mwanamke huyo kujifungulia nyumbani watoto pacha,
huku mmoja akiwa hajakamilika viungo vyote. Pia, kiwiliwili
kilichoungana hakikuwa na kichwa, macho, maini, figo ila alikuwa na
mshipa mmoja wa fahamu ambao ulikuwa umeshikana na mwenzake na
kulazimisha madaktari hao kumfanyia upasuaji.
CHANZO:MWANANCHI
CHANZO:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment