Moshi. Chama cha Wamiliki wa Mabasi Nchini(Taboa), kimesema Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, alidanganywa kuhusu ubora wa magari ya Toyota Noah kuhusu kuruhusu magari hayo kubeba abiria.
Kauli hiyo ya Taboa inafuatia hatua ya Dk
Mwakyembe kuruhusu magari hayo kubeba abiria na kufanya safari zenye
umbali wa zaidi ya kilometa 50, jambo wanalodai ni kinyume cha sheria.
Uamuzi huo wa Dk Mwakyembe aliutoa bungeni mjini
Dodoma, ikiwa ni siku moja baada ya kukutana na wawakilishi wa chama cha
magari hayo waliofunga safari kwenda kumuona.
Hata hivyo Katibu Mkuu wa Taboa, Enea Mrutu
alisema jana kuwa, uamuzi huo wa Dk Mwakyembe utasababisha kuparaganyika
kwa huduma ya usafiri kwa baadhi ya mikoa.
“Wamiliki wa mabasi makubwa wameanza kuondoa
magari yao kwa baadhi ya barabara na hii itasukuma nauli kupanda na
tayari Toyota Noah wameomba kupandisha nauli,” alisema.
Mrutu alisema, uwezo wa magari hayo ni kubeba
abiria wanane hivyo ni hasara gari kwenda umbali mrefu na ndiyo maana
wameomba kupandisha nauli jambo litakaloumiza wananchi.
Alisema uamuzi wa Dk Mwakyembe hauungwi mkono na
Shirika la Viwango (TBS) na Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu
(Sumatra) kutokana na ubora wa magari hayo.
“Tumeshaomba appointment (miadi) ya kukutana na
Waziri (Dk Mwakyembe) ili kumsihi arudi kwenye mstari wa sheria kwa
maslahi ya nchi na Watanzania,” alisema Mrutu.
Akiwa Dodoma, Dk Mwakyembe pia aliiagiza Sumatra
kufikiria ombi la wamiliki wa magari ya Toyota Noah kubeba abiria 10
badala ya wanane, jambo ambalo Taboa wanasema ni hatari.
No comments:
Post a Comment