Pages

Sunday, September 1, 2013

tatizo ni bandari au kagame?

bandari 5193c
KITENDO cha Rwanda na Uganda kutangaza kujitoa kutumia Bandari ya Dar es Salaam kuanzia leo, kimeibua hisia na maoni tofauti kutoka kwa wachambuzi mbalimbali, ambao sasa wameanza kuhoji jambo hilo kwa namna ya kuangalia hali halisi, ukiachilia mbali msuguano wa kidiplomasia unaojitokeza baina ya Tanzania na Rwanda. (HM)
Baadhi ya wachambuzi hao wanaona kuwa mgogoro uliojitokeza baina ya wakuu wawili wa dola, Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania na Paul Kagame wa Rwanda, unaweza ukawa umechochea hatua hiyo, ambayo pia msingi wake unatokana na wivu pamoja na huduma mbovu zinazodaiwa kutolewa katika Bandari ya Dar es Salaam.
Kwamba kero kama mizigo kuchukua muda mrefu hadi kupakuliwa, udokozi, ukiritimba, rushwa na utitiri wa vizuizi barabarani kwa kiasi kikubwa kumesababisha hatua hiyo ya sasa ya Rwanda na Uganda kuamua kutumia Bandari ya Mombasa nchini Kenya, licha ya umbali mkubwa kwao ukilinganisha na Bandari ya Dar es Salaam.
Uhalisia wa uamuzi huo wa Rwanda unaelezwa pia kujengwa na yale ambayo yamekuwa yakijitokeza kwenye ripoti mbalimbali kuhusu matumizi ya bandari za Afrika Mashariki, huku Bandari ya Dar es Salaam ikidaiwa kushindwa kuchukua hatua stahiki za kurekebisha matatizo yake ili iweze kushindana kibiashara na bandari nyingine.
Mfano wa hilo ni ripoti ya miaka miwili iliyopita, inayozungumzia hali ya kibiashara katika nchi zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambayo ilibaini kuwa jumla ya saa 172,236 zinapotea kwa mwaka kutokana na wingi wa vizuizi vya barabarani, huku kiasi cha dola milioni 9.6 kikipotea kutokana na kuwahonga maofisa wa polisi.
Tayari wachambuzi hao wameonya kuwa, hatua hiyo ya Rwanda na Uganda kutangaza kuacha kutumia Bandari ya Dar es Salaam na kujielekeza kutumia ile ya Mombasa, Kenya, itaathiri uchumi wa nchi, na hivyo kuitaka serikali kuchukua hatua za kuboresha huduma zinazotolewa na bandari yake.
Takwimu za mwaka jana za ushushaji mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam, kutoka bahari ya kina kirefu, inaonyesha kuwa nchi ya Rwanda inashika nafasi ya nne kati ya nchi nane zinazozusha mizigo mingi.
Tanzania inaongoza kwa asilimia isiyopungua 66, ikifuatiwa na Zambia asilimia 16, Kongo DRC asilimia 8, Rwanda yenyewe asilimia 5, Burundi asilimia kati ya 2.5 na 3, huku nchi za Uganda, Malawi na Zimbabwe zikiwa na asilimia ndogo ya uingizaji wa mizigo yao.
Kwa mwaka jana pekee, Rwanda ilipitisha tani 528,617, ikishika nafasi ya nne kwa kupitisha tani nyingi za mizigo na Uganda ilipitisha tani 61,225, ikishika nafasi ya sita kati ya jumla ya tani 11,626,765 zilizoshushwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam.
Takwimu zinaonyesha kuwa mapato yanayotokana na Bandari ya Dar es Salaam, yanachangia pato la taifa dola za Kimarekani bilioni 2.6, kwa maana Tanzania peke yake inaingiza dola bilioni 1.8, huku nchi zinazotumia bandari hiyo zikiingiza dola milioni 800.
Akizungumzia msimamo huo wa Rwanda na Uganda kutotumia Bandari ya Dar es Salaam, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana, amesema licha ya azimio hilo kuchukuliwa kisiasa zaidi, lakini ukweli ni kwamba Bandari ya Dar es Salaam ni bomu na haivutii wafanyabiashara.
Naye Mwanasheria na Mjumbe wa Kamati Kuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Profesa Abdallah Safari, alisema ukiritimba na urasimu mwingi ndani ya Bandari ya Dar es Salaam ndiyo sababu kubwa iliyowafanya Rwanda na Uganda kufikia uamuzi wao wa kusitisha upitishaji wa mizigo yao katika Bandari ya Dar es Salaam.
Mkuu wa Ushirikiano na Mawasiliano wa Mamlaka ya Bandari, Janeth Ruzangi, alisisitiza kuwa Bandari ya Dar es Salaam ipo safi.
Alisema huduma za Bandari ya Dar es Salama ni nzuri na zinazidi kuboreshwa, huku akielezea mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika udhibiti wa suala la udokozi na ucheleweshaji wa mizigo bandarini.
"Tumefanikiwa kupunguza matukio ya udokozi wa mizigo inayopitishwa katika Bandari yetu kwa kiasi kikubwa, ambapo mwaka juzi kulikuwapo na matukio 21, mwaka jana matukio saba na katika kipindi cha Januari hadi Agosti mwaka huu, kuna matukio matatu tu na haya ni ya jumla katika mzigo wote unaoingia bandarini...pia tunashukuru teknolojia ya Tehama inatusaidia kwa kiasi kikubwa na sasa mizigo inatolewa bandarini haraka kuliko ilivyokuwa siku za nyuma," alisema Ruzangi.
Hata hivyo, alisema wao kama Bandari hawana taarifa rasmi za Rwanda na Uganda kujitoa Bandari ya Dar es Salaam na kwamba bado nchi hizo zina mizigo yao mingi tu inayosubiri kupakuliwa bandarini.
Hivi karibuni marais Uhuru Kenyatta wa Kenya, Yoweri Museveni wa Uganda na Paul Kagame wa Rwanda, sanjari na mawaziri waliokuwa wakiziwakiisha nchi za Burundi na Sudan Kusini walishiriki katika uzinduzi wa gati namba 19 ya Bandari ya Mombasa, inayoaminika kuwa na kina kirefu kuliko bandari nyingine zote za Afrika Mashariki.
Gati hiyo inaelezwa itasaidia Bandari ya Mombasa kuongeza uwezo wake mara mbili zaidi wa kupakua mizigo.
Wakati Bandari ya Dar es Salaam ikidaiwa kutumia siku 24 kwa meli kupakua mizigo yake, Bandari ya Mombasa ni siku nne tu. Chanzo: Mtanzania Jumapili

No comments:

Post a Comment