Katika mechi ya leo asubuhi ya raundi ya pili ya mtoano iliyochezwa kwenye viwanja vya chuo kikuu cha Dodoma(UDOM), Afya imewachabanga magoli matatu wenyeji timu ya wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) ya mkoani hapa na hivyo kufanikiwa kuingia raundi ya tatu ya mtoano itakayoanza mapema kesho.
Afya iliweza kuona nyavu za GST katika dakika ya kumi ya kipindi cha kwanza cha mchezo huo, ambapo goli la kwanza lilifungwa na mchezaji mwenye jezi namba 10 mgongoni Patrick Mangungulu.
Kipindi cha pili dakika ya tatu Afya ilifanikiwa kuziona tena nyavu za wapinzani hao, goli lililofungwa na Christopher Nandadya aliyepewa pasi nzuri na mshambuliaji Emmanuel Zunda.
Katika kipindi cha lala salama mchezaji wa afya dkt. Iddy Ramadhani alipokea pasi nzuri toka kwa Japhari Ngalipa na hivyo kusababisha kumaliza mchezo huo kwa kifua mbele.
Katika raundi ya kwanza ya ligi, Afya iliibamiza RAS Singida kwa mabao 7 kwa Sifuri na mechi ya pili walifanikiwa kuwazamisha RAS Kilimanjaro kwa mikwaju minne kwa moja.
Hatahivyo katika mechi ya tatu RASMorogoro waliwaotea Afya na hivyo kufanikiwa kuifunga bao moja kwa sifuri. Chanzo: Catherine Sungura (MOHSW)
Dodoma
No comments:
Post a Comment