Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Wednesday, October 30, 2013

DARAJA LA KIKWETE KATIKA MTO MALAGARASI LAKAMILIKA

Picha_Na_1_85040.jpg
Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli (Katikati) akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kanali Msataafu Issa Machibya (kulia) pamoja na Watendaji mbali mbali wakikagua maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Kikwete katika Mto Malagarasi mkoani Kigoma.
Picha_Na_2_cf357.jpg
Sehemu ya barabara pamoja na Daraja la Kikwete kama inavyoonekana hivi sasa baada ya kukamilika kwa ujenzi wake.
Picha_Na_3_ff984.jpg
Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli (Katikati) akiongozana na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kanali Msataafu Issa Machibya (wa pili kulia) na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Eng. Joseph Nyamhanga (kulia) wakipita kwa pamoja na Watendaji mbali mbali katika Daraja la Kikwete.(P.T)
Ujenzi wa Daraja la Kikwete katika mto Malagarasi mkoani Kigoma umekamilika. Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt John Pombe Magufuli akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Kigoma aliweza kutembelea eneo hilo na kujionea magari yakiwa yanapita katika daraja hilo.
Kampuni ya M/S Hanil Engineering and Construction Company Limited kutoka Korea ya Kusini iliingia mkataba na kuanza ujenzi wa daraja hilo mwezi Desemba 2010 na kutakiwa kukamilisha kazi hiyo ifikapo mwezi Desemba 2013. Mradi huo unajumuisha ujenzi wa madaraja matatu yenye jumla ya urefu wa meta 275 pamoja na barabara ya lami yenye urefu wa kilometa 48 kwa gharama ya Dola za Kimarekani milioni 64 ambazo ni sawa na Shilingi bilioni 90 za Kitanzania zilizotolewa na Benki ya Exim ya Korea ya Kusini kwa asilimia 90 na kiasi kilichobaki kikiwa ni fedha za ndani.
Akitoa maelezo ya mradi huo Mhandisi Yu Sing kutoka kampuni ya Hanil Engineering alimfahamisha Waziri Magufuli kuwa, Mradi huo umegawanywa katika sehemu mbili. Sehemu ya kwanza ambayo ndiyo iliyokamilika ni ujenzi wa madaraja matatu yenye urefu wa meta 25, meta 200 na meta 50 pamoja na kilometa 11 za lami. Sehemu ya pili ni ujenzi wa kilometa 37 za lami ambazo ndizo zinazoendelea kukamilishwa kwa sasa.
Baada ya kutembelea eneo hilo la mradi, Mheshimiwa Magufuli alielezea kuridhishwa kwake na utendaji wa mkandarasi huyo kutokana na kukamilisha ujenzi wa sehemu hiyo ya kwanza kwa mujibu wa mkataba na kwa viwango vya hali ya juu. "Nimeridhishwa na utendaji wa mkandarasi huyu na hasa kwa jinsi alivyoweza kumaliza sehemu hii ya kwanza kwa muda mzuri na viwango vya hali ya juu" alibainisha Mheshimiwa Magufuli.
Kwa muda mrefu usafiri katika eneo hilo ulikuwa ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya mkoa wa Kigoma hasa nyakati za mvua kutokana na kukosekana kwa daraja la uhakika. Kwa hivi sasa kumenza kuonekana ongezeko kubwa la magari kati Manyoni – Itingi – Tabora hadi Kigoma kupitia katika Daraja hilo la Kikwete hali ambayo awali ililazimu kupitia barabara ya Manyoni – Singida - Nzega – Kahama – Nyakanazi – Kibondo – Kasulu hadi Kigoma.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kanali Mstaafu Issa Machibya aliyeambatana na Waziri wa Ujenzi katika ziara hiyo, aliishikuru Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi kwa niaba ya Wananchi wa Kigoma kwa kutimiza ahadi ambayo imekuwa ikisuburiwa kwa muda mrefu. "Kukamilika kwa mradi huu pamoja na mingine mingine ambayo inaendelea kujengwa katika barabara ya Kigoma kuelekea Tabora hadi Manyoni mkoani Singida, ni ufumbuzi mkubwa wa matatizo yaliyokuwa yakikwamisha maendeleo katika ukanda huu wa magharibi, hii ni fursa ya pekee kwa amendeleo ya ukanda huu wa Maharibi" alimalizia Mhe. Machibya.

No comments:

Post a Comment