Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam,Kamishna Suleiman Kova
Gaidi
Samantha Lewthwaite maarufu kama ‘mjane mweupe’ raia wa Uingereza
anayedaiwa kuhusika katika tukio la shambulizi la kigaidi jijini
Nairobi, Kenya mwezi uliopita, amezua tafrani kubwa baada ya kuzuka
uvumi kuwa ameonekana katika benki moja jijini Dar es Salaam.Mjane
mweupe ni gaidi anayehusishwa na tukio la ugaidi kwenye kituo cha
biashara cha Westgate jijini Nairobi Septemba 14, mwaka huu na
anatafutwa na vyombo vya usalama vya Kenya na polisi wa kimataifa
(Interpol) kwa udi na uvumba.
Kutokana na kutoroka kwa gaidi huyo,
vyombo vya usalama katika nchi za Afrika Mashariki vimekuwa macho
kufuatilia watu ambao wanahisiwa kuwa wanahusika na shambulizi hilo
linalodaiwa kusukwa na kutekelezwa na mtandao wa kigaidi wa al Shaabab
kwa kushirikiana na Al Qaeda.
Kufuatia hali hiyo, mwanamke mmoja
raia wa Uingereza, jana alikamatwa na Jeshi la Polisi Tanzania baada ya
kutiliwa shaka akifananishwa na gaidi huyo mtukutu.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo NIPASHE
imezipata ambazo pia zimesambazwa katika mitandao ya kijamii, mwanamke
huyo alikamatwa katika benki ya Exim tawi la Tower jijini Dar es Salaam
baada ya wafanyakazi wa benki hiyo kumtilia shaka.
Chanzo cha habari kutoka katika benki
hiyo kilieleza kuwa mwanamke huyo shombe alifika katika ofisi za benki
hiyo makao makuu kuomba tenda ya kusafisha jengo.
Mwanamke huyo ambaye Jeshi la Polisi
bado halijataja jina lake, alifika katika benki hiyo Jumatatu ili aonane
na meneja, lakini aliambiwa aende kesho yake yaani juzi.
Habari zinasema kuwa baada ya kufika
makao makuu ya benki hiyo, aliambiwa meneja hayupo, ndipo alipoibua hoja
mpya na kuwaambia wafanyakazi wa benki kuwa angelipenda kufungua
akaunti kwenye tawi la benki hiyo.
Baada kukubaliwa aliambiwa awasilishe
nyaraka za kumtambulisha, lakini akadai ni raia wa kigeni na hana
nyaraka zozote na alipoulizwa anakaa wapi, alidai kwenye nyumba za
kupanga za Uhuru Heights.
Wafanyakazi wa benki hiyo baada ya
kuona maelezo yake hayajitoshelezi, walitoa taarifa polisi wanaolinda
jengo la Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi jirani na benki hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Polisi
walifika eneo hilo na kumkamata mwanamke huyo na kumpeleka Kituo Kikuu
cha Polisi na alipofanyiwa uchunguzi, ilibainika alivaa lenzi kwenye
macho na pia usoni alikuwa amejipaka vitu ambavyo vilikuwa havionyeshi
vizuri uso wake.
Kufuatia hali hiyo, polisi
walimwamuru anawe uso na baada ya kufanya hivyo, sura yake ya Kishombe
ikapotea na kubaki kama Mzungu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Manongi, alipolizwa kuhusu tukio hilo, alisema hakuwa na taarifa.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Kanda
Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, alithibitisha kukamatwa
kwa mwanamke huyo katika benki ya Exim baada ya kutiliwa shaka na
wananchi.
Alisema baada ya kumfanyia uchunguzi,
ilibainika kuwa siyo gaidi kama ilivyokuwa inahisiwa, badala yake na
ana mume ambaye yupo jijini Dar es Salaam.
“Huyu mwanamke ni raia wa Uingereza,
alipokamatwa alikutwa amevaa hijab na kimsingi wananchi ndiyo
waliomtilia shaka, lakini siyo gaidi kama yule anayetuhumiwa kufanya
ugaidi jijini Nairobi, Kenya,” alisema Kova. Kamishna Kova alisema
mwanamke huyo aliachiwa baadaye baada ya kubainika kuwa ameolewa na mume
wake yupo Dar es Salaam.
Alisema kilichowafanya wananchi
wamtilie wasiwasi ni uvaaji wake wa nguo ambao uliwafanya wahisi huenda
anafanana na gaidi wa tukio la Kenya.
Kamishna Kova alipongeza wananchi kwa
jinsi wanavyokuwa makini katika suala la ulinzi na usalama wa nchi yao
kwa kuwashuku watu ambao hawawaelewi na kuwataka kuendelea kushirikiana
na jeshi hilo.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Mkuu wa
Rasilimali watu wa Jeshi la Polisi, DCP Thobias Andengenye, alitoa
taarifa kuwa jeshi hilo litamsaka gaidi Samantha Lewthwaite anayedaiwa
kupitia mpaka wa Namanga mkoa wa Arusha kabla ya kwenda kufanya tukio
Nairobi ili kumzuia kufanya uhalifu zaidi.
Andengenye alikuwa akihojiwa katika
kipindi cha kipima joto kinachorushwa na kituo cha televisheni cha ITV
kilichokuwa kikijadili Watanzania wamejifunza nini katika kuchukua hatua
juu shambulio la ugaidi lililotokea Nairobi.
Andengenye alisema Jeshi la Polisi
limejipanga kumsaka gaidi huyo ili asije akatenda uhalifu zaidi na
kwamba ufuatiliaji wa mwanamke huyo hautafanywa kwenye mipaka bali hata
ndani ya nchi.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment