Pages

Monday, October 21, 2013

HII NDO HISTORIA FUPI YA MAISHA YA MAREHEMU JULIUS NYAISANGAH AKA ANKO J,

Nyaisanga( wakwanza kushoto) akiwa na wanamuziki wa Sikinde na MK Sound

Jina
la Julius Nyaisanga hakika litabaki kutajwa katika historia ya muziki 
Tanzania. Mtangazaji huyu ambaye alitokea Kenya na kuja kujiunga na 
Radio Tanzania Dar es Salaam, alikuja na aina mpya ya utangazaji ambayo 
ilimfanya apate nafasi ya pekee katika nyoyo za wasikilizaji wa RTD kwa 
miaka yote aliyokuweko huko. Julius ambaye mwenyewe alisema alitengeneza
staili yake ya utangazaji kwa kumuiga mtangazaji maarufu wa KBC Leonard
Mambo Mbotela aliyejulikana sana kwa kipindi chake 'Je huu ni 
uungwana?' alikuja na utangazaji uliochangamsha sana kumsikiliza. 
Nyaisanga alikuwa Producer wa mamia ya nyimbo za bendi zilizorekodiwa na
bendi mbalimbali katika studio za RTD miaka ya 80. Nilipata bahati ya 
kufanya nae kazi wakati nilienda kurekodi nikiwa katika bendi tatu 
tofauti, Orchestra Mambo Bado, Tancut Almasi Orchestra, na  Vijana Jazz 
Band. Alishauri vizuri na matokeo yake ni nyimbo nyingi zilizopitia 
mikononi mwake zingali zinapendwa mpaka leo.
Pamoja
na utangazaji, na u producer wa muziki, Nyaisanga alipenda muziki na 
wanamuziki, alikuwa rafiki wa wanamuziki wengi sana, alikuwa na tabia ya
kutembelea bendi zinapopiga na aliweza hata kutembelea bendi nne au 
tano kwa usiku mmoja. Na hasa kama bendi iko katika ratiba ya 
kurekodiwa. Aliwahi hata kufika Iringa kutembelea tancut Almasi 
Orchestra kabla ya kurekodi toleo lao lililokuwa naule wimbo usiochosha 
Masafa Marefu. Nyaisanga alipita kwenye bendi kadhaa kututaarifu kuhusu 
kuanza kwa radio mpya ambayo ingekuwa katika masafa ya FM, na ndipo muda
si mrefu Radio One ikaingia hewani wakati huo ikiwa pale katika jengo 
la NASACO ambalo lilikuja kuungua na baada ya kukarabatiwa sasa linaitwa
Waterfront. Pia akiwa Radio One Nyaisanga aliendelea kuwa Nyaisanga, 
japo sera za Radio One hakika zilikuwa tofauti na zile za RTD, lakini 
pia huko mchango wake katika muziki ulikuwa mkubwa sana. Hatimae 
Nyaisanga alihamia Abood Radio Morogoro ambako amekuweko mpaka hatimae 
usiku wa kuamkia leo 20 October 2013, umauti umemkuta katika hospitali 
ya Mazimbu Morogoro kutokana na kusumbuliwa kwa muda mrefu na Kisukari.
MUNGU AMLAZE PEMA PEPONI UNCLE J

No comments:

Post a Comment