MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imekubali kampuni za simu
nchini kujiunga pamoja na Chama cha Kutetea Walaji kwenye kesi ya
kupinga tozo ya kadi ya simu ya Sh. 1,000 kwa kila laini na mtumiaji kwa
kila mwezi dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wizara ya Fedha
baada ya kutupilia mbali pingamizi la awali la upande wa walalamikiwa.
Uamuzi
huo ulitolewa jana na jopo la majaji watatu wakiongozwa na Mwenyekiti,
Jaji Aloysius Mujuluzi, akisaidiana na Lawrence Kaduri na Salvatory
Bongole.
Jaji
Mujuluzi alisema baada ya kupitia hoja zilizotolewa na pande zote mbili
kuhusu pingamizi hilo, mahakama imeona upande wa walalamikiwa hauna
sababu za msingi za kupinga kampuni za simu kujiunga kwenye kesi hiyo na
kwamba inazitupilia mbali.
Aidha, baada ya uamuzi huo mahakama iliziamuru pande zote mbili
kubadilishana nyaraka za majibishano ya kisheria kwa njia ya maandishi
na kesi ya msingi itasikilizwa Oktoba 21, mwaka.
Kampuni zilizojiunga kwenye kesi hiyo ni, Vodacom, Airtel, Mic Tanzania
Ltd, TTCL na Zantel Tanzania.
Jumatatu iliyopita, upande wa walalamikiwa
ukiongozwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju,
akisaidiana na Wakili wa Serikali Mkuu, Edson Mweyunge, Alisia Mbuya na
Sara Mwaipopo, walipinga ombi la mawakili wa kampuni za simu la kutaka
kujiunga kwenye kesi hiyo kwa kuwa hati ya kiapo ilikosewa kisheria.
Mweyunge alidai kuwa hati ya kiapo iliyowasilishwa mahakamani
imeonyesha kutolewa na Tumaini Shija ambaye anawawakilisha walalamikiwa
wengine zikiwamo makampuni za simu.
Hata hivyo, wakili wa kampuni za simu, Fatuma Karume, alidai kuwa
pingamizi la jamhuri halina sababu za msingi kwa sababu siyo kila
mlalamikaji anatakiwa kuwasilisha kiapo chake katika kesi moja kwamba
mahakama itupilie mbali pingamizi la jamhuri halina msingi kisheria.
Katika kesi ya msingi Chama cha Kutetea Walaji kimewaburuza mahakamani
Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wizara ya Fedha kikitaka wapewe amri ya
kusimamisha tozo ya kadi ya simu ya Sh. 1,000 kwa kila laini kwa
watumiaji wa simu kila mwezi, baada ya kupitishwa na Bunge miezi
michache iliyopita.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment