Ripoti ya Benki Kuu ya Dunia (WB) ya mwaka 2013, imebainisha kwamba kukosekana kwa mwingiliano sahihi wa kiutendaji kwenye taasisi za umma kunakwamisha kwa kiwango kikubwa utendaji wa Bandari ya Dar es Salaam.
Benki ya Dunia kupitia ripoti yake, inashauri
mamlaka husika kufanya maboresho makubwa ya ukusanyaji wa mapato ili
kugharimia programu za uwekezaji zenye mambo mengi ndani ya kipindi cha
mwaka 2014 na 2015.
Wakati benki hiyo ikishauri hayo Waziri wa
Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, anaitupia lawama Mamlaka ya Mapato
Nchini (TRA) kwa kutotoa huduma katika siku saba za juma. Anasema hali
hiyo inarudisha nyuma ufanisi wa bandari hiyo.
“Kinachohitajika ni TRA wanapaswa kushirikiana na
taasisi za kibenki ili watoe huduma za kibenki kila siku na ikiwezekana
saa 24 ili kwenda sambamba na bandari ambao wanafanya kazi saa 24, lengo
ni kutochelewesha meli zinazoleta mizigo bandarini hapo,” anasema.
Dk Mwakyembe anasema kila taasisi inapaswa
kutekeleza wajibu wake ipasavyo ili kuinua pato la taifa na kwenda
sambamba na Mpango wa Matokeo Makubwa wa (BRN).
“Watendaji wa bandari wanafanya kazi saa 24 kila
siku za juma bila kupumzika, lakini TRA wao wanalala siku za sikukuu na
za mwisho mwa juma, jambo hili hatutakubali liendelee,” anasema Dk
Mwakyembe.
Waziri huyo anakwenda mbali zaidi na kuzitaka
Bandari za Nchi Kavu (ICDs) kutoa huduma hizo kila siku ili kuepusha
usumbufu kwa mteja kuingia gharama atakazotakiwa kulipa kwa muda wakati
mzigo wake utakapokuwapo sehemu hiyo.
Ufanisi wa TPA
Kaimu Meneja wa Tanzania Port Authority (TPA),
Awadhi Massawe anasema katika kipindi cha mwaka 2012/2013 bandari
ilihudumia tani milioni 12.5 za mizigo, ukilinganisha na tani milioni
10.9 zilizohudumiwa mwaka 2011/12 ikiwa ni zaidi kwa asilimia 15.0.
Shehena ya kichele (nafaka) iliongezeka kwa
asilimia 37.4, nafaka mchanganyiko asilimia 7.8 na mafuta iliongezeka
kwa asilimia 19.0 huku shehena yote kwa ujumla ikiongezeka kwa asilimia
12.6 kwa mwaka.
Anasema mgomo wa malori uliathiri upakuaji wa
mizigo bandarini kwa sababu asilimia 99 ya mizigo inayopakuliwa
bandarini inatumia usafiri wa barabara.
“Idadi ya siku kwa meli kusubiri kupakuliwa mizigo
bandarini imepungua kutoka siku 6.1 mwaka 2011/12 hadi siku 4.9 mwaka
2012/13 huku idadi ya siku meli kusubiri nje kuingia kwenye geti
imepungua kutoka siku 3.2 mwaka 2011/12 hadi kufikia siku 1.7 mwaka
2012/13.CHANZO MWANANCHI
No comments:
Post a Comment