Pages

Thursday, October 31, 2013

Mbunge atuhumiwa kwa ufisadi, aundiwa kamati

 
Mbunge wa Bahi, Omar Baduwel, anatuhumiwa kutafuna fedha za Mfuko wa Jimbo zilizokuwa zikirejeshwa na wananchi baada ya kukopeshwamajembe ya kukokotwa na ng’ombe.

Mbali na hilo pia Mbunge huyo anadaiwa kutafuna fedha za mradi wa maji wa kijiji cha Chibelela ambao serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo ilitenga Sh. milion nne kwa ajili ya mradi huo ambao wananchi pia walichangia Sh. milioni 1.7.

Akiwasilisha hoja binafsi katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Bahi, Diwani wa Kata ya Lamaiti, Donald Mejitii (CCM), alilitaka Baraza la Madiwani kuunda kamati kwa ajili ya kuchunguza fedha hizo baada ya halmashauri kushindwa kusimamia makusanyo ya fedha za Mfuko wa Jimbo kwa mwaka mmoja.

Alisema hatua ya kuwasilisha hoja binafsi imefuatia taarifa kuwa kuna mtu anayepita kuzikusanya fedha hizo wakati si mfanyakazi wa serikali na hazifikishwi halmashauri.

“Kinachonishangaza hata hizi pia Mbunge huyo aliamua kuchukua fedha hizo na mpaka sasa hazijulikani zilipo na wananchi bado hawana huduma ya maji … kwa mwaka huu peke yake Mfuko wa Jimbo ulitoa kiasi cha Sh. milioni 17 na wananchi wamerejesha kiasi cha Sh.   milioni 8.5 ambazo zimeshakusanywa, lakini hakuna hata kiasi kidogo kilichoingia halmashauri,” alisema Mejitii.

Alibanisha kuwa katika kata yake pekee alipokea majembe 15 na mpaka sasa wamerejesha zaidi ya Sh. milioni 1.5, lakini kwa taarifa alizonazo ni kuwa fedha hizo hazijafikishwa halmashauri.

Mejitii alisema fedha za Mfuko wa Jimbo zimekuwa zikitumiwa vibaya na mbunge huyo kwani amekuwa akizitumia kama fedha zake binafsi hali inayowafanya wananchi kuamini kuwa fedha hizo hutolewa na mbunge na siyo kutoka serikalini.

Aliongeza kuwa wamekuwa wakishuhudia mara kwa mara mbunge akizitumia fedha hizo na kuzipa jina la ‘Kopa kwa mbunge lipa kwa jirani’, hali inayowafanya wananchi kuamini kuwa fedha hizo zinatoka mfukoni mwake na siyo serikalini.

Diwani huyo alisema wananchi wengi hawajui kama fedha hizo zinatoka serikalini kwa kupitia Mfuko wa Jimbo kwani wengi wao wanajua kuwa hutolewa na mbunge na ndiyo maana anapofika kuzikusanya au kumtuma msaidizi wake, wanampa bila ya wasiwasi wakijua ni zake.

“Kwa kuthibitisha hili, hata wananchi wanapotakiwa kurejesha fedha hizo mbunge huyo huzichukua na hazijulikani matumizi yake kwani hazifiki hata halmashauri,” alisema.

Aidha, alitolea mfano katika mradi wa majembe ambao ulianzishwa na Mfuko wa Jimbo kwa ajili ya kuwakopesha wakulima na baadaye walipe nusu ya gharama, lakini makusanyo hayo hayajafikishwa halmashauri.

Alisema anasikitishwa na kitendo cha kumuona msaidizi wa mbunge akipita kwa wananchi kukusanya fedha hizo wakati siyo mtendaji wa serikali na hajawahi kufikisha kiasi chochote halmashauri.

“Hakuna hata shilingi moja iliyofika kwenye halmashauri, sasa nataka kujua kama huo mradi ni wa Mfuko wa Jimbo au ni kwa ajili ya kuwanufaisha watu wachache,” alisema.

“Pia kikundi kilichopewa jukumu la kukopesha majembe  cha Basada kimekuwa kikiwatoza wananchi kiasi kikubwa cha fedha kuliko bei halisi ya kununulia majembe ya kukokotwa na ng’ombe wakati bei halisi ya jembe moja ni kati ya Sh. 180,000 hadi 170,000, lakini wananchi wanatozwa Sh. 110,000 kama nusu ya bei ya jembe badala ya Sh.  80,000 au 85,000 ambacho ndiyo kiasi sahihi kwani  mwananchi anatakiwa kutoa kama nusu ya bei,” alifafanua Mejitii.

Baada ya Diwani huyo kuwasilisha hoja hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Hussein Kamau, aliwahoji madiwani na baadhi yao walisema kwamekuwa wakiona fedha hizo zikikusanywa, lakini hawajui zinapokwenda.

Kamau baada ya kusikiliza hoja hiyo, aliamua kuunda kamati kwa ajili ya kuchunguza tuhuma hizo na kuwateua wajumbe wanne. Kati yao wawili ni madiwani na wawili  ni watumishi wa halmashauri.

Alipoulizwa na NIPASHE kuhusiana na tuhuma hizo, Mbunge huyo alisema: “Mkienda Chibelela mtakuta maji yanatoka, hakuna shida yoyote katika kijiji hicho.”

Kuhusu fedha za mradi wa majembe, alisema kuwa yeye hakusanyi fedha za majembe kwani siyo kazi yake na kuwa kazi yake ni kukabidhi, hivyo waulizwe waliozikusanya.

“Msaidizi wangu wana uhakika gani kama nimemtuma, wangeniuliza mimi kama nimemtuma, watu wanaongea tu wala hawajui mimi nina matatizo gani na msaidizi wangu. Kiukweli maji yanatoka Chibelela na fedha za majembe mimi sijakusanya,” alisema na kuongeza:

“Najua kuna mtu anataka ubunge ndiyo maana wanasema hivyo.”

Mbunge huyo angali anakabiliwa na kesi ya kuomba rushwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment