Meli hiyo ya Maersk Line. |
Biashara
katika bandari ya Dar es Salaam imeanza kushika kasi huku Watanzania
wakitarajia kunufaika na punguzo la bei ya bidhaa kutoka nje baada ya
meli kubwa yenye urefu wa meta 249 kuanza kutia nanga katika bandari
hiyo.
Hatua hiyo imekuja baada ya kuwepo kwa propaganda kuwa bandari hiyo
haina uwezo wa meli zenye ukubwa huo wenye kubeba makontena 4,500 kutia
nanga, lakini jana Tanzania iliandika historia kwa meli hiyo kutia nanga
asubuhi.
Meli hiyo ya Maersk Line ilitia nanga ikiwa inaendeshwa na kapteni wa
Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), Abdul Mwingamno ambaye alielezea wazi
kuwa hakupata tatizo lolote kutia nanga.
Kutia nanga kwa meli hiyo kulishuhudiwa na Waziri wa Uchukuzi, Dk
Harrison Mwakyembe na kusema kuwa kuanza kutia nanga kwa meli hizo kubwa
kutaongeza mizigo kupitia katika bandari hiyo.
“Kwa sasa biashara inazidi kuchanganya kwani nchi za Zimbabwe na
Kongo wanapitisha mizigo yao hivyo kwa kutumia meli hizo kubwa gharama
zitapungua zaidi ya kuongeza nchi kutumia bandari hiyo,” alisema.
Akizungumzia meli hiyo kutia nanga bandarini, Kaimu Mkurugenzi wa
Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Madeni Kipande alisema kila kitu
kinawezekana iwapo kila mtu atafanya juhudi na kuwajibika.
Alisema changamoto watakayokutana nayo sasa ni vifaa vya kupakulia
kuendana na ukubwa wa meli ili kuweza kupunguza muda wa kushusha shehena
na hivyo kuondoa misongamano bandarini.
Alisema kulikuwa na propaganda ya kuwa meli za ukubwa huo haziwezi
kutia nanga katika bandari hiyo hivyo kuishia Mombasa, Kenya na meli
ndogo kubeba mizigo mpaka bandarini hapo.
Pia Madeni alizungumzia mgomo wa malori na kusema ulisababisha
mlundikano wa mizigo hivyo kusababisha hasara ya Sh bilioni 1.5 na mpaka
jana asubuhi, bado kulikuwa na meli 18 zikisubiri huku tisa zikipakua
mzigo.
Alisema wamekuwa katika hatari ya hasara zaidi kwa uchumi kwani idadi
kubwa ya mbolea ambazo ni hatari iwapo zingenyeshewa, kwani zilishindwa
kusafirishwa.
Naye Meneja mwendeshaji wa kampuni hiyo ya Maersk Line, Amos
Mwansumbule alisema meli hiyo iliyotokea katika nchi za Asia na kupitia
Afrika Magharibi na kutia nanga Angola, ilisafiri kwa siku 10 kutoka
nchini humo hadi Dar es Salaam na ilitarajia kukaa bandarini hapo kwa
saa nane.
No comments:
Post a Comment