Shirika
la Kimataifa la Mtandao wa Ulaya wa Madeni na Maendeleo, European
Network on Debt and Development (Eurodad) watafanya ziara ya
kiuchunguzi kuhusu masuala ya uwazi katika kodi katika nchi za Ulaya
kuanzia tarehe 20 Oktoba mpaka tarehe 5 Novemba mwaka 2013.
Uchunguzi
huo utaendeshwa na wataalamu waliobobea wa masuala ya kodi na
maendeleo. Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali wa Bunge
la Tanzania Zitto Zuberi Kabwe ameteuliwa kuongoza Jopo la uchunguzi
huo.
Eurodad
ni Mtandao wa Mashirika yasiyo ya kiserikali yapatayo 48 kutoka nchi 19
za Ulaya ambayo yanajihusisha na masuala ya kufutia madeni nchi
zilizoendelea, misaada yenye maana na kodi za haki. Mashirika haya
yamekuwa kwenye kampeni ya kupinga utoroshwaji wa fedha kupitia ukwepaji
kodi unaofanywa na mashirika ya kimataifa kwa nchi zinazoendelea.
Zitto
amekuwa mmoja wa wabunge wanaosimamia hoja ya kutaka Watanzania
waliotorosha fedha kwenda nje warejeshe na kufunguliwa mashtaka. Mwaka
2012 aliwasilisha hoja binafsi Bungeni na kupitishwa kuwa Azimio la
Bunge ya kutaka uchunguzi kuhusu utoroshwaji wa fedha na kufichwa nje
kama Uswiss.
Kikosi
Kazi cha Serikali kutekeleza Azimio hilo la Bunge kinatarajia
kuwasilisha taarifa yake katika Mkutano wa Kumi na Sita wa Bunge. Siku
ya Jumatatu tarehe 21 Oktoba Zitto atakutana na Waziri wa Fedha wa
Uswiss na maafisa wa mabenki na asasi zisizo za kiserikali zilizopo
jijini Geneva. Pia Zitto atahudhuria mkutano wa Kamati ya Kodi ya Umoja
wa Mataifa katika kampeni ya kubadili mfumo wa kodi za kimataifa ili
kuzuia unyonyaji wa nchi za Kiafrika unaofanywa na Makampuni makubwa ya
Kimataifa.
Baada
ya Geneva Zitto atatembelea nchi za Luxembourg na Brussels kabla ya
kwenda Norway ambapo atamalizia ziara yake kwa Jopo la Wataalamu wa
masuala ya kodi na Maendeleo kuandika taarifa maalumu yenye mapendekezo
kuhusu kuzuia utoroshaji wa fedha kutoka Afrika.
Zitto
atakwenda jijini London kutoa mada kuhusu masuala ya kodi za kimataifa
katika mkutano wa Uwazi (Open Government Partnership). Mwenyekiti wa PAC
Tanzania atafanya mazungumzo na Mwenyekiti wa PAC Uingereza Bi Margaret
Eve Hodge, Lady Hodge MBE, PC, MP kuhusu masuala mbalimbali ya
ushirikiano wa mabunge mawili na kuendeleza wito wake kwa makampuni ya
kimataifa kulipa kodi zao barani Afrika na kuacha tabia ya kutumia ‘Tax
Havens’ kukwepa kodi na kufukarisha nchi za Kiafrika.
No comments:
Post a Comment