Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Saturday, October 12, 2013

Operesheni maalumu ya GIBOIA yakamata dawa bandia 273

6070897_orig_29bde.jpg
Jumla ya dawa bandia za aina 273 zenye thamani ya shilingi 49,634,733/= zimekamatwa katika operesheni maalumu iliyoendeshwa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Shirikisho la Polisi la Kimataifa (Interpol), Baraza la Famasi, TAMISEMI, Bohari ya Dawa (MSD), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Shirika la Viwango (TBS), Tume ya Ushindani (FCC), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Ofisi ya Rais na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii katika maeneo 138 nchini.
Operesheni hiyo ijulikanayo kama 'Giboia' iliendeshwa kwa lengo la kufuatilia, kukamata na kuwafikisha katika vyombo vya
sheria wanaojihusisha na biashara ya dawa bandia, zisizosajiliwa, zisizo na ubora na zilizoisha muda wa matumizi.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Manumba alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana wakati akitangaza matokeo ya operesheni hiyo. Alisema operesheni hiyo ilifanyika kwa siku tatu, Oktoba 1-3 mwaka huu, kwa kukagua maduka ya dawa ya jumla na rejareja, waingizaji wa dawa nchini, vituo vya afya na maabara binafsi.
Aliyataja maeneo , ambayo ukaguzi huo ulifanyika na idadi ya vituo kwenye mabano kuwa ni Dar es Salaam (67), Mbeya (6), Kilimanjaro (8), Arusha (5), Mwanza (11), Geita (7), Shinyanga (6) na Dodoma (20).
"Dawa bandia zilizokamatwa zilikuwa aina mbili (Asdoxin na Penizin-V), zilizoisha muda wa matumizi zilikuwa 76, dawa za serikali na miradi mbalimbali ya serikali 28, zisizosajiliwa 86 na zenye ubora duni 40," alisema.
Alisema dawa nyingine ni zilizofutiwa usajili 41 na 19 zinazohisiwa kuwa ni bandia, ambazo zilikamatwa na kufanyiwa uchunguzi wa kimaabara kuhakiki ubora wake.
Manumba alisema hatua zimechukuliwa, ikiwa ni pamoja na majalada 42 ya kesi kufunguliwa katika vituo mbalimbali nchini.
4972088_orig_d1168.jpg
MAELEZO YA UTANGULIZI YA MKURUGENZI MKUU WA MAMLAKA YA CHAKULA NA DAWA (TFDA) BW. HIITI B. SILLO KATIKA MKUTANO WA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU MATOKEO YA OPERESHENI "GIBOIA" KATIKA UKUMBI WA MIKUTANO WA TFDA TAREHE 10 OKTOBA, 2013
Naomba nichukue fursa hii kwa niaba ya Menejimenti na Wafanyakazi wa TFDA kuwakaribisha, katika ofisi za Mamlaka ya Chakula na Dawa. TFDA ni taasisi iliyo chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii yenye jukumu la kudhibiti ubora na usalama wa vyakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba.
Naamini wote tunaelewa dhima ya TFDA ambayo ni kulinda afya za wananchi kwa kuzuia athari zinazoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya vyakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba. Katika kufikia dhima hii, changamoto kubwa tunayokabiliana nayo katika udhibiti ni uwepo wa bidhaa duni, bandia na zisizosajiliwa kwenye soko.
Ndugu wanahabari,
Tumewaalika ili tuwape taarifa juu ya matokeo ya Operesheni Giboia iliyofanyika hapa nchini kwa pamoja baina ya Mamlaka ya Chakula na Dawa na Jeshi la Polisi nchini kwa kushirikiana na Shirikisho la Polisi la Kimataifa (Interpol) na taasisi na idara nyingine za Serikali. Taasisi na idara nyingine za Serikali ambazo majukumu yake yanagusa masuala ya dawa au udhibiti zilizoshiriki operesheni hii ni mpamoja Baraza la Famasi, TAMISEMI, Bohari ya Dawa (MSD), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Shirika la Viwango (TBS), Tume ya Ushindani (FCC), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Ofisi ya Rais na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Napenda kuzishukuru taasisi hizi kwa ushirikiano wao katika kufanikisha operesheni mbalimbali za kupambana na biashara haramu ya dawa bandia na kwa namna ya pekeeOperesheni Giboia. Mamlaka itaendelea kushirikiana na taasisi hizi katika kukabiliana na changamoto ya udhibiti wa bidhaa bandia na duni za chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba bandia na vile ambavyo havisajiliwa na Mamlaka ili kuwalinda wananchi dhidi ya madhara ya kiafya wanayoweza kuyapata.
Ndugu wanahabari,
Operesheni hii ni mwendelezo wa operesheni za awali za kufuatilia dawa bandia na duni katika soko. Lengo la Operesheni hii lilikuwa ni kukamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria wale wote wanaojihusisha na biashara ya dawa bandia. Dawa zilizolengwa zilikuwa ni dawa za kutibu ugonjwa wa malaria, dawa za kupunguza makali ya virusi vya ukimwi, viuavijasumu (antibiotics), dawa za kuongeza nguvu za kiume na dawa za kupunguza maumivu. Dawa hizi zilichaguliwa kutokana na kuwa na matumizi makubwa zaidi hapa nchini na hivyo kuwa na soko kubwa kiasi cha kuvutia biashara haramu ya dawa bandia. Vile vile, katika Operesheni hii dawa za Serikali na miradi mbalimbali ya Serikali, dawa zisizosajiliwa, dawa duni na dawa zilizoisha muda wa matumizi zilifuatiliwa.
Ndugu wanahabari,
Operesheni Giboia imefanyika sanjari katika nchi saba zilizopo kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo ni Afrika Kusini, Angola, Malawi, Msumbiji, Swaziland, Zambia na Tanzania kwa muda wa siku tatu kuanzia tarehe 1 hadi 3 Oktoba 2013.
Makubaliano ya kufanyika kwa Operesheni Giboia yalifikiwa katika mkutano uliohusisha nchi nilizozitaja uolifanyika jijini Luanda, Angola tarehe 10 hadi 12 Juni 2013. Pamoja na mambo mengine, mkutano huo uliweka mikakati ya namna ya kuendesha Operesheni Giboia kwa mafanikio.
Napenda kuwajulisha kwamba ushirikiano baina ya nchi mbalimbali katika vita dhidi ya dawa bandia ni utekelezaji wa Azimio la Mawaziri wa Afya Duniani la mwaka 2012 (World Health Assembly Resolution 65.19). Azimio hilo pamoja na mambo mengine limeelekeza ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika kupambana na biashara haramu ya dawa bandia.
Kwa upande wa Tanzania, Operesheni Giboia imefanyika katika mikoa tisa ya Mwanza, Shinyanga, Mara, Geita, Mbeya, Arusha, Kilimanjaro, Dodoma na Dar es salaam. Maeneo yaliyokaguliwa ni pamoja na famasi, maghala ya kutunzia dawa, vituo vya afya na maabara binafsi na maeneo yote yaliyotiliwa mashaka ya kuwepo kwa dawa hizo bandia.
Ndugu wanahabari,
Kwa kumalizia maelezo yangu, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru sana Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini, Kamishna wa Polisi, Bw. Robert Manumba na Jeshi la Polisi kwa ujumla kwa ushirikiano mkubwa wanaoutoa kwa TFDA katika kupambana na tatizo hili kubwa la dawa bandia katika nchi yetu. Aidha, natoa shukrani za dhati kwa taasisi na vyombo vyote vya dola kwa ushiriki wao katika operesheni hii na vile vile kwa kuwa tayari wakati wote kushirikiana na TFDA katika mapambano haya. Imani yangu ni kwamba ushirikiano uliopo ukiendelezwa na kwa ushirikiano kutoka kwa wanahabari na wananchi kwa ujumla tutashinda vita dhidi ya biashara haramu ya dawa bandia.
Baada ya maelezo haya, ninayo heshima kumkaribisha Kamishna wa Polisi, Robert Manumba, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini ili aweze kutoa matokeo ya Operesheni Giboia.
Asanteni kwa kunisikiliza.
Source: http://www.wavuti.com

No comments:

Post a Comment