Pages

Wednesday, October 2, 2013

PICHA::UGAIDI WA AL SHABAB… UWANJA WA TAIFA SI SALAMA,KACHERO WA GAZETI LA CHAMPION AINGIA NA SILAHA BILA KUKAGULIWA.



Na Mwandishi Wetu
PAMOJA na tukio kubwa na la hatari la kutisha lililotokea katika nchi jirani ya Kenya, imebainika hakuna tahadhari yoyote iliyochukuliwa katika sehemu za mikusanyiko mikubwa ya watu kama vile Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Uwanja huo wa kisasa zaidi kuliko mingine yote katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, una uwezo wa kubeba watazamaji hadi 60,000, hali inayoweza kuwavutia magaidi kufanya jambo lolote.
Wiki chache zilizopita, magaidi wa Al Shabab wa Somalia, walifanya ugaidi wa kutisha na kuua watu zaidi ya 65 kwenye jumba la biashara la Westgate jijini Nairobi, hali ambayo inalazimisha kuwa na tahadhari kubwa katika sehemu zinazojumuisha watu wengi nchini kama Uwanja wa Taifa.
Ilielezwa vyombo vya usalama nchini Kenya vilidharau kuweka tahadhari baada ya kupata taarifa kulikuwa na maandalizi ya uvamizi kutoka kwa Al Shabab na sasa Mkuu wa Usalama wa Taifa Kenya (NIS), Michael Gichangi, atahojiwa kuhusiana na hilo.
Miezi kadhaa iliyopita, kulikuwa na tishio la kundi hilo la Al Shabab kufanya matukio ya kigaidi katika nchi za Afrika Mashariki ukiwemo uwanja huo.
Kutokana na hilo, Championi liliamua kutuma makachero wake ili kuthibitisha kama kuna tahadhari yoyote ambayo imechukuliwa kwenye Uwanja wa Taifa ambao ni moja ya sehemu nyeti nchini.
Kawaida zaidi ya watu 10,000 huingia karibu kila mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, hasa zile zinazohusisha Yanga au Simba.
Mageti matatu makuu yanayotumika, mawili yakiwa ya waenda kwa miguu na moja la magari, yana askari na walinzi wa kampuni binafsi ambao hawafanyi ulinzi wowote wa kitaalamu zaidi ya kuangalia kwa macho huku tiketi tu ndizo zikikaguliwa, kitu ambacho ni hatari.
Makachero wa Championi waliingia uwanjani hapo Jumapili iliyopita wakati Simba ikipambana na JKT Ruvu katika mechi ya Ligi Kuu Bara huku wakiwa na silaha.
Makachero hao wa Championi walifanikiwa kupita katika maeneo
yote yanayolindwa na kampuni ya ulinzi uwanjani hapo pamoja na askari wenye mafunzo kamili na kuingia hadi ndani katika jukwaa lenye watazamaji wengi.
Walianzia geti linalotumika kupitisha magari bila ya ukaguzi wowote, walipita na kuingia ndani akiwa na bunduki mbili, bastola na ‘shotgun’ ambayo ni kubwa na ingekuwa si rahisi kupenya nayo, hata ulinzi wa macho tu bila ya mitambo kama ungekuwa imara.
Baada ya hapo, kachero huyo kwa mwendo wa madaha, akiwa na bastola, alimuachia mwenzake bunduki kubwa naye kuanza kupiga hatua za madaha kwenda jukwaani akikatiza sehemu zenye ulinzi wa askari polisi na walinzi binafsi bila kukaguliwa wala kuhojiwa, kama picha katika ukurasa huu zinavyoonyesha.
Hiyo ni dalili kwamba, mtu yeyote mwenye nia mbaya, anaweza akapita kirahisi na silaha hadi kufika katika moja ya majukwaa na kufanya analotaka.
Kama kachero wa Championi Jumatano aliyetaka kujaribu kupima hali ya usalama uwanjani hapo alipita na silaha hizo mbili, maana yake si kazi kwa magaidi kufanya wanachotaka hata kuingia na bomu, tena kwa urahisi kabisa.
Kwa kuwa Al Shabab walililipua jengo la Westgate ambalo ni maarufu katika masuala ya biashara, haina maana sehemu nyingine zenye mikusanyiko ziko salama. Wamekuwa na mbinu nyingi na mambo yao hayajulikani kirahisi na tahadhari inaweza kupunguza uwezekano wa kutokea mambo kama hayo.
Akizungumzia suala hilo, Meneja wa Uwanja wa Taifa, Rish Urio alisema kuna ulinzi lakini wanaopaswa kulizungumzia hilo ni wanaohusika na usalama.
“Hatupendi kuyaweka kwenye magazeti lakini tuko makini na ningeomba uwasiliane na watu wa usalama kama Kamanda Kova, watakueleza vizuri kwa kuwa hicho ni kitengo chao,” alisema Urio.
Jana jioni, gazeti hili lilimtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova kuzungumzia suala hilo, lakini hakuweza kupatikana kutokana na simu yake kuita bila kupokelewa.CHANZO GPL

No comments:

Post a Comment