Rais
Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na wafanyakazi wa Swissport katika
uwanja wa ndege wa kimataifa ya Julius Nyerere wakati akielekea kwenye
ndege jioni
ya jana, Jumatatu, Oktoba 28, 2013, kwenda London, Uingereza, kwa ziara
ya kikazi ya siku nne ambako atahudhuria Mkutano wa Kimataifa wa
Serikali Uwazi (Open Government) uliotishwa na Serikali ya Waziri Mkuu wa Uingereza, Mheshimiwa David Cameroun. Kulia
kwake ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe Bernard
Membe na Meneja wa Shirika la ndege la Emirates uwanjani hapo Bw.
Aboubakar Jumaa. (PICHA NA IKULU)
…………………………………………………………………………………………..
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya
Mrisho Kikwete ameondoka nchini jioni ya jana, Jumatatu, Oktoba 28,
2013, kwenda London, Uingereza, kwa ziara ya kikazi ya siku nne ambako
atahudhuria Mkutano wa Kimataifa wa Serikali Uwazi (Open Government)uliotishwa na Serikali ya Waziri Mkuu wa Uingereza, Mheshimiwa David Cameroun.
Mkutano huo wa siku mbili utafanyika keshokutwa Jumatano na Alhamisi kwenye Ukumbi wa Queen Elizabeth 2 mjini London.
Miongoni mwa mambo makuu
ambayo mkutano huo utazungumzia ni Serikali Uwazi na Ajenda ya
Maendeleo Baada ya Mwaka 2015 wakati muongo wa utekelezaji wa Malengo ya
Maendeleo ya Milenia (Millenium Development Goals) unafikia mwisho.
Masuala
mengine ambayo yatazungumzwa katika mkutano ambao Rais Kikwete
anaambatana na Mawaziri wake watatu ni pamoja na uwazi katika manunuzi
ya umma, uwazi katika mikataba, haki ya kupata habari, uwazi katika
ukaguzi wa fedha za umma, uwazi wa Serikali na vyombo vya habari, uwazi
katika mikataba ya maliasili, uwazi katika maendeleo ya nchi
zinazoendelea.
Mawaziri
wanaoambatana na Rais Kikwete katika ziara hiyo ni Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mheshimiwa Bernard Membe, Waziri wa
Sheria na Katiba Mheshimiwa Mathias Chikawe na Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Utawala Bora Serikali ya Mapinduzi, Zanzibar Mheshimiwa Mwinyihaji
Makame.
Rais Kikwete anatarajia kurejea nyumbani Jumamosi, Novemba 2, 2013.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
29 Oktoba, 2013
No comments:
Post a Comment