Pages

Friday, October 4, 2013

Rais Kikwete azindua gati Mafia, jiwe la msingi Chuo cha Tereni

5338209 orig a4c7a
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewataka Watanzania kuachana na hulka ya kukejeli jitihada za maendeleo na kujenga fitina kuhusu miradi ya maendeleo.
Amesema kuwa baadhi ya Watanzania, badala ya kuunga mkono jitihada za maendeleo, wanapiga kasi mpya ya kurudi nyuma kwa kupinga na kukejeli miradi ya maendeleo. (hd)
Rais Kikwete alikuwa anazungumza leo, Alhamisi, Oktoba 3, 2013, Kisiwani Mafia wakati alipoanza ziara ya siku tano kukagua shughuli za maendeleo na kufungua miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Pwani.
Akizungumza na wananchi baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Chuo cha Ufundi, Tereni, nje ya mji mkuu wa
Mafia wa Kilindoni, Rais Kikwete ameimwagia sifa Mfuko wa Maendeleo ya Mafia (MIDEF) ambao umefanikisha mambo makubwa ya maendeleo katika Wilaya hiyo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Chuo hicho ambacho kitagharimu kiasi cha sh. bilioni 5.33 na kuchukua wanafunzi 400 kitakapokamilika. Chuo hicho pia kitakuwa na sehemu ya Chuo cha Michezo – Sports Academy.
Mbali na ujenzi wa chuo hicho, MIDEF imejenga shule ya sekondari ya bweni, imeunga mkono shule za sekondari za kata za Serikali kwa kuzipa kompyuta na madawati, inatoa mikopo ya maendeleo kwa wananchi, imetoa zana za kazi kwa taasisi za Serikali na imesimamia kupatikana kwa fedha za kusambaza umeme katika vijiji vyote vya Mafia kupitia Mamlaka ya Kusambaza Umeme Vijijini (REA).
Kwenye mradi wa kusambaza umeme vijijini, kwa mfano, MIDEF imechangia kiasi cha Sh. Milioni 500 katika mradi ambao utagharimu Sh. Bilioni tano.
Rais Kikwete amewaambia wananchi wa Mafia: "Jitihada hizi za MIDEF lazima ziungwe mkono. Sina maneno mazuri ya kuwaambieni kuwa kama hamtaunga mkono jitihada hizo mtakuwa na matatizo, tena matatizo makubwa sana. Mtakuwa mnafikia kwa kasi mpya ya kurudi nyuma."
Amesisitiza Rais Kikwete: "Nasema hivyo kwa sababu sisi Watanzania kazi yetu imekuwa ni kujenga fitina, kubeza na kukejeli jitihada za maendeleo. Hiyo ndiyo hulka yetu kujenga fitina kuhusu miradi ya maendeleo."
"Tunashangaza sana. Mtu anayekuhubiria upate maendeleo unamwona mtu mbaya, lakini mtu anayekuhubiria usipate maendeleo unamuona mtu mzuri na mwema. Tabia hii ndiyo naiita ya kupiga kasi mpya ya kurudi nyuma," amesema Rais Kikwete.
Katika ujenzi wa Chuo hicho cha Ufundi, Serikali imechangia kwa kutoa ardhi ya kujenga chuo hicho katika eneo la Tereni na kukamilika kwa Chuo hicho kuitaiwezesha Tanzania kuongeza idadi ya vyuo vya ufundi nchini. Kwa sasa kuna vyuo vya ufundi 742 vyenye wanafunzi 145,510, kati ya hivyo 17 vikiwa vya Serikali, na vilivyobakia vikiwa vya watu na taasisi binafsi.
Rais Kikwete ambaye ameshinda siku nzima katika Wilaya hiyo ya Mafia amerejea Dar Es Salaam jioni ya leo na kesho atafanya ziara ya Wilaya ya Mkuranga.

No comments:

Post a Comment