Pages

Thursday, October 31, 2013

Sita kortini kwa kujeruhi wachezaji wa Prisons


MECHI baina ya Mbeya City na Prisons imeingiza Sh 31.6 milioni huku watu sita wa jijini Mbeya wakikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuwapiga mawe wachezaji wa Prisons na kuvunja vioo vya magari juzi Jumanne.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Robert Mayala, alisema mara baada ya kumalizika kwa mechi hiyo baadhi ya vijana walijikusanya nje ya uwanja huo eneo la Rift Valley na kufanya vurugu hizo.
“Mpira ulimaliza kwa amani kabisa, lakini mashabiki wakiwa wanatoka uwanjani kuna kundi la vijana walikuwa wamejikusanya eneo la Rift Valley na kulishambulia basi la wachezaji wa Prisons na kuwajeruhi baadhi ya wachezaji  pamoja na kuvunja vioo,” alisema Mayala.
Aliwataja waliokamatwa na kufikishwa mahakamani kuwa ni Enock Jeremeiya, David Daniel, Emmanuel Ndalu, Michael George, David Laurent na Vicent Ramadhan.
Awali, Katibu Mkuu wa Tanzania Prisons, Sadick Jumbe,  alilaani kitendo cha kushambuliwa kwao na kubainisha kwamba vurugu hizo ni dhahiri kuwa hazilengi kujenga umoja na mshikamano kwa wakazi wa jiji hilo na vitongoji vyake.
Katika hatua nyingine, mchezo huo uliingiza mashabiki 10,558. Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mbeya, Suleiman Haroub, alisema kutokana na mapato hayo kila timu ilipata asilimia 29.5 sawa na Sh 6, 987,000.CHANZO MWANASPOTI

No comments:

Post a Comment