Pages

Friday, October 11, 2013

Tumetoka kifungoni na hamasa kubwa

MwananchiKurudiClip_1a8e4.jpg
Hata hivyo, huu hakika sio wakati wa kumtafuta mchawi, kwa maana ya kutaka kujua nani hasa serikalini alitoa amri ya kulifungia gazeti hili kwa sababu ambazo sisi tunaona hazikuwa na chembe ya mashiko. Tulishangazwa kuona amri hiyo ya Serikali ikitolewa wakati mkuu wa nchi, Rais Jakaya Kikwete akiwa nje ya nchi, tena akiwa katika majukumu mazito ambayo dunia nzima ilikuwa ikiyafuatilia kwa shauku na umakini mkubwa.
Kulifungia gazeti wakati huo hatuoni kama ilikuwa kwa masilahi ya taifa kwa sababu hatua hiyo iliichafua taswira ya nchi yetu na bila shaka Rais Kikwete alijikuta katika wakati mgumu kila alipoulizwa kuhusu hatua hiyo iliyochukuliwa na Serikali yake.
Ni habari zipi zilizolipeleka gazeti hili kifungoni? Habari ya kwanza ilikuwa juu ya waraka kuhusu mishahara mipya ya watumishi wa Serikali ambayo tuliithibitisha pasipo kuacha shaka yoyote kutoka katika vyanzo vyetu vya habari vya kuaminika katika mamlaka za juu serikalini.
Tuliuchukulia kama taarifa muhimu sana kwa watumishi wa Serikali na wananchi kwa jumla na hatukuona sababu ya Serikali kutaka wananchi wafichwe kuhusu kuwapo kwa mishahara mipya kwa watumishi wake.
Itakumbukwa kuwa, wiki chache kabla ya gazeti hili halijachapisha habari hiyo, lilikuwa pia limechapisha habari kuhusu mishahara mipya katika sekta binafsi kwa mujibu wa waraka wa Serikali uliotolewa na Wizara ya Kazi na Ajira. Swali linalojitokeza hapa ni hili: Inakuwaje mishahara mipya ya watumishi wa Serikali iwe siri na mishahara mipya kwa sekta binafsi iwe kinyume chake?
Tunaamini kwamba utamaduni wa Serikali kuficha habari na taarifa zenye manufaa kwa umma siyo utawala bora hata kidogo. Ni hivi majuzi tu Rais Kikwete alipomwagiwa sifa na Rais Barrack Obama kwa kutia saini mkataba wa uendeshaji wa shughuli za Serikali kwa uwazi.
Habari ya pili iliyochapishwa Agosti 17 mwaka huu na kusababisha gazeti hili kufungiwa ilihusu Serikali kuimarisha ulinzi katika maeneo ya karibu na misikiti jijini Dar es Salaam jana yake kufuatia kuwapo tetesi kwamba waumini wa Kiislamu siku hiyo wangeandamana kupinga kitendo cha Jeshi la Polisi kumuweka mahabusu Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda. Baadhi ya waumini walikuwa wameonyesha kukasirishwa na kitendo cha polisi kumwondoa Sheikh Ponda katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi) na kumpeleka katika Gereza la Segerea, jijini Dar es Salaam.
Habari hiyo yenye kichwa cha habari; 'Waislamu wasali chini ya ulinzi mkali wa polisi' ilichapishwa ikiwa na mmoja wa mbwa waliokuwa na polisi katika doria kutokana na hofu ya kuzuka vurugu baada ya Swala ya Ijumaa, Agosti 16. Habari hiyo ilisema Waislamu hawakuandamana na waliswali kwa amani na utulivu na kwamba polisi hao waliokuwa na mbwa, huku wengine wakitumia pikipiki kufanya doria walitanda katika mitaa mbalimbali kwa lengo la kuimarisha ulinzi. Lakini kwa mshangao wetu, Serikali katika kujaribu kuhalalisha kulifungia gazeti hili ilitoa tafsiri ya uongo kwamba habari tuliyochapisha ilisema kwamba mbwa walipelekwa katika maeneo ya ibada, wakati habari hiyo haikuwa na kitu kama hicho. Serikali ilidai katika taarifa hiyo, kwamba lengo la habari hiyo lilikuwa kuichonganisha na waumini wa Kiislamu ili waichukie pamoja na vyombo vyake vya ulinzi na usalama, kwani kwa Waislamu mbwa ni haramu na picha hiyo iliudhalilisha Uislamu. Taarifa hiyo potofu ya Serikali imetuthibitishia pasipo kuacha shaka kwamba haikuwa na nia njema na gazeti hili.
Hatua ya kulifungia gazeti hili kwa sababu za kufikirika imesababisha maumivu kwa watu wengi. Vijana (vendors) waliokuwa wakiuza na kusambaza gazeti hili pamoja na familia zinazowategemea wameumia. Waandishi wa kujitegemea wanaolipwa kutokana na habari wanazotuma gazetini wameumia pamoja na familia zao. Hivyo hivyo, watoa matangazo na wasomaji waliokuwa wakilitegemea gazeti hili kwa habari za uhakika nao pia wameumia. Hasara ambayo MCL imepata kutokana na hatua hiyo ya Serikali haitamkiki.
Pengine huu ni wakati mwafaka wa kuikumbusha Serikali kwamba, gazeti hili pamoja na mengine yanayochapishwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), ni magazeti makini sana yenye waandishi wa habari wanaoheshimu maadili ya taaluma yao. Hatusemi kwamba hatuwezi kufanya makosa, kwani sisi ni binadamu.
Hata hivyo, inapotokea tukafanya makosa tunafanya masahihisho stahiki haraka kwa lengo la kupunguza maumivu kwa yeyote tuliyemkosea. Makosa ya makusudi kama kuandika habari za uongo hayavumiliki na kila mwandishi wa kampuni yetu anatambua fika kwamba kufanya hivyo ni kujitakia kiama.
MCL imeweka miongozo ya sera na malengo ya uhariri kwa waandishi. Lengo ni kuhakikisha habari zinazochapishwa ni sahihi, zinatenda haki na haziegemei upande wowote. Kwa maana hiyo, vyombo vyake vya habari vinasimamia ukweli na haki na waandishi wake wana jukumu la kuhakikisha wanakuwa na kiwango cha juu cha weledi na maadili ili kuwawezesha kutoa habari kwa umma.
Tumetoka kifungoni tukiwa na somo muhimu. Kwamba sheria kandamizi kama Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 haisimamii masilahi ya taifa, bali kundi la watu wachache. Ni sheria kandamizi ambayo kwa umoja wetu tunaweza kuifuta. Tungependa kuwashukuru wasomaji wetu na wananchi kwa jumla kwa kuwa nasi katika kipindi kigumu tulichokuwa kifungoni. Vilevile, tunavishukuru kwa namna ya pekee vyombo vyote vya habari vya ndani na nje ambavyo vilisimama imara kupinga hatua ya Serikali kufungia magazeti.
Tutakuwa watu wasio na shukurani kama hatutatambua mshikamano mkubwa ulioonyeshwa na asasi za kiraia, mabalozi na watu mbalimbali kupinga matumizi ya sheria hii kandamizi. Hatujakata tamaa, bali tumetoka kifungoni tukiwa na hamasa kubwa kuendelea kuwapa habari wananchi pasipo woga wala upendeleo.
Hatupambani na Serikali, lakini tutaendelea kuikosoa pale inapofanya makosa na tutaipongeza pale inapotimiza wajibu wake. Tunawaomba wasomaji wetu mwendelee kutuunga mkono.

No comments:

Post a Comment