Pages

Tuesday, October 1, 2013

UNHCR yamtuza mtawa wa kikongo


zzzzcongo_32eff.jpg
Tuzo ya Nansen ya shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR, mwaka huu itatolewa kwa mtawa kutoka Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo Angelique Namaika kutokana na mchango wake katika kuwasaidia wanawake.
Mtawa huyo Angelique Namaika amesema amefurahi juu ya tuzo atakayoipokea leo lakini pia amesema kuwa hakuitarajia. Imekuja kwake kama jambo la kushangaza .
''Niliposikia kwamba miongoni mwa washindani kutoka kote duniani, mimi ndiye niliyechaguliwa kupata tuzo, sikutaka kuamini kwa sababu nipo mbali sana na nilidhani kwamba dunia haiwezi kujua juu yangu" Amesema mtawa huyo.
Mtawa huyo mwenye umri wa miaka 46 alisafiri kwa muda mrefu kutoka kwenye mji wake wa Dungu hadi kufika mji mkuu wa Jamhuri wa Kidemokrasi ya Kongo Kinshasa, na kuendelea hadi Uswisi.
Kujitoa kwa wanyonge
Kwa muda wa miaka mingi mtawa huyo Namaika amekuwa anawasaidia wanawake na watoto nchini mwake. Miongoni mwa wanawake na watoto hao ni wale walionusurika kifo.
Kwani katika kipindi cha miaka 30 waasi wa kundi la Lord's Resistance Army wamekuwa wanaeneza hofu kwenye maeneo ya mipakani kati ya Uganda, Jamhuri ya Kidemkrasi ya Kongo, Jamhuri ya Afrika ya kati na Sudan ya Kusini. Waasi hao wamewaua watu, wamewabaka wanawake na wamewatumikisha watoto kama askari.
Wanapovamia sehemu waasi hao wa LRA wanawateka nyara watoto. Watu karibu milioni tatu na nusu wametimuliwa kutoka kwenye vijiji vyao kutokana na uhalifu wa makundi ya kigaidi kama LRA.
Hasa wasichana wanaobakwa na ,magaidi wanabakiwa na majeraha ya moyoni. Mtawa Angelique Namaika ambae leo anatunukiwa tuzo ya shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR anafanya kazi kubwa ya kujaribu kuwasaidia wanawake na akina dada hao.Anawasaidia ili waweze kujitambua tena, kujifunza kazi na kujipatia riziki.
Baadhi ya akina dada waliteswa vibaya sana na waasi wa LRA.Wengine walikatwa hata midomo ya juu.
Hata yeye aliathirika
Mtawa Angelique Namaika mwenye amepitia katika masaibu, na ndiyo sababu analijua neno hofu. Alipokuwa msichana alilazimika kukikimbia kijiji chake na kujificha maporini kwa muda wa mwaka mzima.
Mtawa Namaika anawasaidia wasichana na wanawake wapatao 2000 kusoma, kushona na kuwasaidia kupambana na majeraha ya roho. Na pia anawasaidia yatima. Lakini pia amekabiliwa na matatizo katika kuwasaidia yatima hayo kama anavyoeleza.
Mara nyingine sikuwa na fedha ili kuwapeleka kwa daktari yatima hao waliotelekezwa maporini. Lakini kwa uwezo wa Mungu nilipata nguvu na kuweza kuwaomba watu wengine msaada", Ameeleza mtawa Namaika
Mtawa Namaika alihamasishwa na mtawa wa kijerumani katika kiji chake cha Kembisa kaskazini mwa Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo. Mtawa wa Kijerumani alikuwa anawahudimiwa watoto wagonjwa katika kijiji hicho.
Namaika alisema hata yeye anataka kuwa kama mtawa huyo wa kijerumani. Tuzo anayotunukiwa Angelique Namaika leo nchini Uswisi inaandamana na donge la Euro 74,000.
Mwandishi: Matthaei,Katrin

No comments:

Post a Comment