Amewahishwa katika zahanati ya kijiji ambayo hata hivyo haina dawa wala vifaa zaidi ya mkunga wa zamu wa siku hiyo.
Kwa kuwa hakuna usafiri wa ku mwahisha Naomi
katika hospitali ya wilaya, mkunga anajaribu kumsaidia katika
kujifungua, lakini baada tu ya kujifungua, dada huyu anatokwa na damu
kwa wingi, lakini pia, kichanga kilichozaliwa kinashindwa kupumua na kwa
bahati mbaya wote… wanapoteza maisha.
Roho za kinamama na watoto wengi zinapotea kila
kukicha kutokana na ukosefu wa huduma za afya, jambo ambalo
limesababisha idadi ya vifo vya makundi haya kuwa milioni 6.9 kwa
mwaka.
Vifo vya mama na mtoto vinaepukika na katika
kupunguza vifo hivyo wataalamu wa afya wamebuni teknolojia nyepesi na
nafuu itakayowezesha wataalamu wa afya katika eneo lolote Kusini mwa
Jangwa la Sahara kuokoa maisha ya viumbe hawa muhimu duniani.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema kuwa,
uvumbuzi wa teknolojia rahisi utaweza kuokoa maisha ya wanawake na
watoto zaidi ya milioni 7.5 kwa mwaka.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban ki- Moon
amesema, uvumbuzi huo ni sehemu muhimu kwa kila mwanamke na kila mtoto
duniani kwani ni miongoni mwa harakati za kuokoa maisha ya wanawake na
watoto milioni 16 ifikapo mwaka 2015.
Kupunguza vifo vya wanawake na watoto ni miongoni
mwa malengo ya Milenia ya Umoja wa Mataifa. Ripoti za Umoja wa Mataifa
zinaeleza kuwa, kati ya watoto 1,000 wanaozaliwa nchini kila siku, 26
hufariki kwa sababu zinazoweza kuzuilika. Wasaidie watoto kupumua
(Helping Baby Breath) ni teknolojia inayotumiwa na wataalamu wa afya
sehemu yeyote ile kuwasaidia watoto wanaozaliwa na kushindwa
kupumua.(birth asphyxia) Teknolojia hii imesaidia kupunguza asilimia 47
ya vifo vya watoto wanaozaliwa na tatizo la kupumua nchini.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya wanawake, Profesa
Cyriel Massawe anasema, iwapo teknolojia zaidi zingevumbuliwa, basi vifo
vya wanawake na watoto vingekwisha kabisa.
“Tatizo kubwa ni kuwawezesha wataalamu wa afya.
Hata kama teknolojia hizi zitavumbuliwa bado wataalamu wanahitaji
usafiri ili kuzifikisha vijijini ambako kuna vifo zaidi, ” anasema
Profesa Massawe.
Profesa Massawe anasema ni teknolojia rahisi
kutumika kwani inafundisha mbinu za kumkausha mtoto pindi anapozaliwa na
kumvalisha kifaa maalumu kinachomsaidia kupumua.
Wakunga nchini walipewa mafunzo hayo na jinsi ya
kutumia kifaa aina ya ‘Neonatalie’ ambacho ni kifaa rahisi kutumiwa na
mtaalamu yeyote hata mkunga wa jadi ili kumsaidia mtoto mwenye matatizo
ya kupumua pindi tu anapozaliwa. Teknolojia nyingine inayofanana na HBB
ni ‘Bubble CPAP,’ kifaa cha njia ya upumuaji ambacho huwasaidia watoto
waliopata matatizo ya mfumo wa upumuaji ikiwemo nimonia.CHANZO GAZETI LA MWANANCHI
No comments:
Post a Comment