Pages

Sunday, October 20, 2013

Watumshi wa Mahakama nchini waaswa kufuata sheria na maadili ya utumishi wa umma


01_164ca.jpg
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Angellah Kairuki akisisitiza umuhimu wa kutoa adhabu mbadala kwa watuhumiwa baada ya hukumu zao kukamilika alipokuwa anaongea na watumishi wa Mahakama ya Mwanzo ya Kerege (hawapo pichani) iliyopo Wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani kwenye ziara yake ya siku moja wilayani humo. Wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa PwaniBahati Ndeserua, wa kwanza kushoto ni Msajili Mahakama kuu, kanda ya Dar es salaam Projestus Mhagama.
02_22ecc.jpg
Hakimu Mfawidhi Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo Liadi Mohamed Chamshama akimwonesha Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Angellah Kairuki (mwenye gauni kitenge) na ujumbe wake eneo la mahakama ya Mwanzo ya Kiwangwa alipokuwa kwenye ziara ya kikazi ya siku moja wilayani mkoa wa Pwani.
(Picha zote na Eleuteri Mangi- Maelezo)
Na Eleuteri Mangi -MAELEZO
Serikali imewataka watumishi wa Mahakama nchini kuendesha shughuli zao kwa kuzingatia weledi, sheria, kanuni, taratibu, misingi ya kazi na maadili ya utumishi wa umma ili waweze kufikia malengo yao ya kazi katika kutenda haki kwa wateja wao.
Wito huo ulitolewa hivi karibuni na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Angellah Kairuki alipokuwa katika ziara ya kikazi ya siku moja wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Naibu Waziri Kairuki aliwataka watumishi hao wafikie malengo yao ya kazi kwa kuzingatia ushirikiano baina yao na wadau wengine wa mahakama, lengo ni kufanikisha utendaji wao wa kazi.
"Mnapimwa kwa kupunguza mrundikano wa mashauri mliyonayo, ni vema muwe na mkakati wa kuyapunguza au kuyamaliza kwa wakati mashauri hayo na kutenda haki kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu, misingi ya kazi na maadili ya utumishi wa umma" alisema Kairuki.
Aidha, Naibu Waziri Kairuki aliwaasa watumishi wa mahakama kutojihusisha na rushwa wakati wote wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao ili wananchi waendelee kuwaamini.
"Kila mmoja wenu awe ni mwangalizi mzuri na balozi wa mwenzake, mfanye kazi kwa kushirikiana ili haki itendeke", alisema Kairuki
Naibu Waziri huyo aliendelea kusisitiza "kwa yeyote mwenye tabia ya kujihusisha na rushwa aache mara moja na atambue kuwa yeye ni mtumishi wa umma"
Watumishi wanapojiingiza kwenye rushwa mara zote hawazitendei haki familia zao, taaluma zao na wateja wao ambao ndio wanaotegemea kupata haki kupitia watumishi wa mahakama mahalia.
Kwa upande wake Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo Liadi Chamshama alimwahidi Naibu Waziri Kairuki kwa niaba ya watumishi wa mahakama zilizo chini yake kuwa watatekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria, kanuni, taratibu, misingi ya kazi na maadili ya utumishi wa umma.
Pia Hakimu Chamshama aliwaasa watumishi wa mahakama hizo waelewe kuwa watapata heshima na kuaminiwa na wananchi pale ambapo mahakama haitakuwa na upendeleo na kuzingatia sheria na maadili ya kazi na taaluma.
Idara ya Mahakama nchini inakabiliwa na changamoto ya kuwa na miundo mbinu na majengo ya mahakama machakavu yaliyoanzishwa muda mrefu uliopita pamoja na uhaba wa watumishi wa kada mbalimbali wakiwemo wapiga chapa.
Kwa sasa Serikali ipo kwenye mpango na utaratibu wa maboresho ya Mahakama zote nchini ambapo mwaka huu wa fedha 2013/14 zinatarajiwa kujengwa Mahakama za Wilaya sita (06) na Mahakama za Mwanzo 12.
Katika ziara hiyo ya kikazi ya siku moja Naibu Waziri Kairuki alitembelea Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo na Mahakama za Mwanzo sita ambazo ni Kerege, Mwambao, Kiwangwa, Msata, Msoga-Lugoba na Chalinze.
MWISHO

No comments:

Post a Comment