Pages

Saturday, November 9, 2013

ALIYEOA WAKE 15 AELEZA SIRI YA KUOA NA KUZAA WATOTO WENGI


aoa_1ffb1.jpg
Lukata Singu na baadhi ya wake, watoto na wajukuu zake katika picha ya pamoja. Picha Elias MsuyaMzee Lukata Singu (65) anayeishi katika Kijiji cha Nyamwage wilayani Rufiji Mkoa wa Pwani, anajivunia kuwa na familia kubwa yenye wake wengi wanaofikia 15 na watoto zaidi ya 70.Nimemtembelea kijijini hapo ambapo amejenga boma analoishi na baadhi ya wake, watoto na wajukuu.Singu amenikaribisha nyumbani kwake na kutaka apate picha ya ukumbusho na familia yake japo haijakamilika. Kisha anaanza kusimulia:"Mimi nilizaliwa Shinyanga, sijui mwaka gani ila wakati Mwalimu Nyerere anaanza kutawala wakati wa uhuru nilikuwa na miaka 13. Wazazi wangu walihamia Tabora na baadaye Manyoni. Nimeishi Manyoni kwa muda mrefu hadi nikawa na familia. Nimeishi pia Igunga na Tabora. Huko kote nimeacha wake zangu na watoto," anasema Singu.Anasema alihamia wilayani Rufiji miaka saba iliyopita akiwa na ng'ombe 600 hata hivyo wengi walifia njiani wakati wa kuwasafirisha na magari.

"Hapa ninaishi na wake zangu 12. Wengine hawakuja hapa kupiga picha, wamebaki kwenye maboma wanalinda vyakula. Hawa wengine unaowaona ni watoto na wajukuu. Nina wake wengine watatu wilayani Igunga, Tabora na Manyoni, kote huko nimeacha familia," anasema Singu.
Licha ya wingi wa wake na watoto, bado Singu anasisitiza kuwa hajaacha kuzaa kwani baadhi ya wake zake bado ni wajawazito.
"Siyo kwamba nimemaliza kuzaa wala kuoa, tena baadhi ya wake zangu wana mimba. Kwa nini niache kuzaa wakati bado nina nguvu?" anahoji.
Siri ya kuoa wake wengi
Singu anaeleza siri ya kuoa wanawake wengi kuwa ni nguvu za kiume alizonazo kulingana na umri wake mwenyewe akisema ni nguvu alizojaaliwa na Mwenyezi Mungu.
"Ni uwezo tu wa Mwenyezi Mungu, maana mimi nilizaliwa hivyohivyo, ndivyo Mungu alivyoniumba... Situmii dawa yoyote. Kama Mungu asingeniwezesha nisingekuwepo kwa sasa," anasema na kuongeza:
"Sina dini yoyote, ila ninaamini Mungu yupo na ndiye anayeniwezesha. Huwa ninamwomba na kumshukuru. Tumezaliwa tumemkuta kwa hiyo kusali ni muhimu... naamini yupo na kama asingeniwezesha ningeshafutika."
Akizungumzia elimu kwa watoto na wajukuu wake, anasema hiyo siyo kipaumbele kwake, huku akisisitiza kuwa kuna uhaba wa shule katika kijiji hicho.
"Watoto hawa hawasomi, tatizo huku hakuna shule, hata wenyeji wa huku hawasomi kazi ni kukata miti tu. Hata hivyo kuna watoto wangu wako Tabora ndiyo wamesoma, lakini sijui wamefikia darasa la ngapi," anasema.
Ndoa za utotoni
Mbali na mzee Singu, yupo mjukuu wake, Jiraa Lukanda Lukata anayekadiriwa kuwa na miaka 30 anayeonekana kufuata nyayo za babu yake.
Jiraa ameoa wake watatu na anaishi na babu yake kwenye boma hilo. Kwa mke wa kwanza, Gindu Shija mwenye umri wa miaka 21 ana watoto wanne huku mke wa pili, Lawi Kulwa (miaka 21) na Holo Shija (miaka 15) walioolewa miaka miwili iliyopita bado hawajapata watoto.
Hata hivyo, Jiraa anakanusha kufuata nyayo za babu yake:
"Siyo kwamba nafuata nyayo za babu, mimi naishia hawa wake watatu tu wanatosha," anasema Jiraa.
Akieleza taratibu za kupata wake hao, Jiraa anasema wazee hasa babu yake wamehusika kumtafutia.
"Kwa taratibu zetu za Kisukuma, wazee huchunguza wanawake wenye tabia nzuri kutoka kwenye koo nyingine. Hawa wake zangu babu yangu alinioza baada ya kuridhishwa na tabia zao," anasema na kuongeza:
"Mke wa kwanza nilimwolea katika kijiji cha Muhoro hapa hapa Rufiji.
Akizungumzia ufahamu wake kuhusu sheria za ndoa anasema licha ya kutokuwa na elimu yoyote anazifahamu sheria zinazokataza ndoa za utotoni.
"Mimi sina elimu yoyote wala wake zangu hawana elimu, lakini naelewa baadhi ya sheria za ndoa. Najua sijafanya kosa kosa lolote kuoa wake wenye umri huu," anasema.
Nao wake wadogo wa Jiraa Lawi na Holo wanasema kuwa wameridhika kuolewa naye.
Kuhusu elimu ya wake hao, Gindu, Lawi na Holo wanasema wamemaliza darasa la saba lakini hawajui kusoma wala kuandika.
Uhusiano na kijiji
Licha ya kudai kuwa eneo analoishi katika kijiji hicho kuwa lake, inaelezwa kuwa Singu hana uhusiano mzuri na wanakijiji wenzake.
Akiwa nyumbani kwake, Singu anasema maeneo yote yanayozunguka makazi yake anayamiliki kihalali.
Haya yote unayoyaona hapa ni mashamba yangu, nimekuwa nikilima mihogo na mahindi. Kwa sasa watoto wangu wanatayarisha mashamba kwa ajili ya kilimo.
Hata hivyo Mwenyekiti wa kijiji hicho, Ibrahim Mboweto anasema kuna utata katika umiliki wa eneo hilo.
"Singu ni kati ya wafugaji waliokuja na kuvamia maeneo ya vijiji. Baadaye waliomba ndiyo akaruhusiwa. Lakini kwa kuwa ana mifugo mingi ilionekana lile siyo eneo la mifugo na wananchi wanalalamika kuwa mifugo yake inaharibu mashamba yake," anasema na kuongeza:
"Kuna wakati alifukua kisima cha asili akawa akitumia kunywesha mifugo yake, lakini aliwakataza wanakijiji wasikitumie, ndiyo nao wamekasirika wanamlazimisha ahame. Mwenyewe amegoma akisema ili ahame wanakijiji wamhamishe kwa gharama zao. Tumemwachia mkuu wa wilaya maana hatuna uwezo tena."
Naye Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Nurdin Babu amekiri kuufahamu mgogoro huo na kwamba anaushughulikia.
"Mgogoro huo ulifika kwangu na nilifika kwenye mkutano wa kijiji, Singu akaonyesha nyaraka zake za kumiliki hilo eneo," anasema Babu na kuongeza:
"Yule mzee alimilikishwa eneo na kijiji hivyo amewaambia kama wanataka ahame inabidi wamlipe Sh90 milioni alizowekeza pale. Ndiyo nimewaambia wanakijiji wasubiri wakati mwanasheria wangu anaangalia uwezekano mwingine, wataambulia kesi."
Kuhusu suala la elimu kwa wa watoto wake, Babu anasema amekuwa akihamasisha jamii za wafugaji kupeleka watoto wao shule, ila kama hawataki ni juu yao.
"Kila ninapokuwa kwenye mikutano nawahamasisha hasa jamii za wafugaji wapeleke watoto shule. Tumejenga shule nyingi na walimu wapo. Kuna baadhi ya wafugaji wamewanunulia watoto wao baiskeli wanakwenda shule. Kama yeye anaona starehe ni kuoa wake wengi na kuzaa, basi hiyo shauri yake," anasema Babu.
Utility
Kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012, idadi ya Watanzania imefikia 44,928,923 ukilinganisha na idadi ya 12,313,469 ya mwaka 1967 wakati ambao kulikuwa na ukuaji wa asilimia 2.9 kwa mwaka.
Watoto walio chini ya umri kwa miaka 15 ni sawa na asilimia 44.1, huku walio kati ya umri wa miaka 15 hadi 35 wakifikia asilimia 35.5, asilimia 52.2 ikiwakilisha kundi la watu wenye umri kati ya 15 hadi 64 na asilimia 3.8 ni kundi la watu wenye umri zaidi ya 64.
Idadi yay a Watanzania inahusisha makabila zaidi ya 120 huku makabila ya Wasukuma, Wahaya, Wanyakyusa, Wanyamwezi na Wachaga wakiwa na zaidi ya watu milioni moja.
Mkakati wa Kukuza uchumi na kupunguza umaskini (Mkukuta) umelenga kufikisha huduma za kudhibiti uzazi kwa asilimia 60 ya wanawake wote ifikapo mwaka 2015 na utagharimu kiasi cha dola 88.2 milioni kati ya mwaka 2010 na 2015.
Hata hivyo bajeti ya Taifa na utekelezaji wa mkakati huo umekuwa dhaifu licha ya fedha za uzazi wa mpango zimeongezeka mara tatu tangu mwaka 2010 hadi 2011.
Licha ya Serikali kuukubali mpango wa 'Kila mwanamke Kila mtoto' ambao ni wa kwanza duniani na unaohamasishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon kuhusu afya ya wanawake na watoto, Mpango wa maendeleo wa miaka mitano uliotangazwa mwaka 2012 na Rais Jakaya Kikwete una kipengele kimoja tu cha uzazi wa mpango.

No comments:

Post a Comment