Mwanaspoti linaweza kuthibitisha pasipo shaka kuwa
Berko atatua kwa usafiri wa Shirika la Ndege la Kenya kwa ajili ya
kufanya makubaliano ya kuidakia Simba kuanzia mzunguko wa pili wa Ligi
Kuu Bara unaoanza Januari 25 mwakani.
Simba imepanga kumpa mkataba wa miezi sita Berko
ambao utakwisha Juni mwakani na kuwepo kwake kutategemeana na kanuni
mpya za Ligi Kuu Bara kwani huenda kusiwe na makipa wa kigeni kuanzia
msimu ujao kama kanuni mpya zitaanza kutumika.
Tayari uongozi wa Simba umempa maagizo kipa wao wa
sasa raia wa Uganda, Abel Dhaira kumtaka atafute timu nyingine kutokana
na kupungua kiwango pamoja na gharama kubwa.
Mmoja wa waandishi maarufu wa Ghana aliliambia
Mwanaspoti jana Jumatano kuwa Berko amepokea tiketi hiyo na atatua
katika ardhi ya Tanzania Ijumaa.
Berko alipopigiwa simu kuthibitisha habari hizo,
kwanza aliguna, halafu akazungumza kwa Kiswahili; “Wewe nani? Baada ya
mwandishi kujitambulisha na kumuuliza kuhusu suala la kujiunga Simba
alicheka halafu akasema: ‘‘Nipigie baadaye tuzungumze nipo mazoezini.”
Hata hivyo hakupatikana tena.
Viongozi wa Simba walionekana kushangazwa kila walipotafutwa kuthibitisha hilo, huku wengi wakisema hawana habari na hilo.
Hata hivyo, uchunguzi wa ndani wa Mwanaspoti
unaonyesha kuwa Berko ameipokea tiketi ya ndege aliyotumiwa na Simba na
atatua kesho Ijumaa kufanya mazungumzo na klabu hiyo ya Msimbazi.
Berko aliondoka Yanga mwaka huu baada ya klabu
hiyo ya Jangwani kumpa dola 7,500 (Sh 12 milioni) alizokuwa anawadai
kutokana na kuvunja mkataba.
Yanga ilimtoa Berko kwa mkopo kwenda FC Lipopo ya
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ili wabadilishane na Mnyarwanda
Kabange Twite, pacha wa kiraka wa klabu hiyo, Mbuyu Twite, lakini mpango
huo ulishindikana msimu uliopita.
Baadaye kipa huyo bora wa Ligi Kuu Bara msimu wa
mwaka 2011/12 alibaki Jangwani lakini bila kucheza akawa mtu wa
kujifungia chumbani muda wote makao makuu ya Yanga.
No comments:
Post a Comment