Tangu kumalizika kwa vikao vya Kamati Kuu ya CHADEMA, iliyoketi kwa siku mbili mfululizo Novemba 20-21, mwaka huu, kisha maazimio yake kutolewa kwa wanachama na umma wa Watanzania siku ya jana, kumeanza kuibuliwa propaganda nyingi zenye makusudi maalum.

Ni wazi kuwa hatuwezi kukimbizana na wapika propanda (rumourville is back?), kwa kujibizana nao kwa kila wanachokisema. Itakuwa ni kufanya kazi wanazotaka wao tufanye badala ya kuendelea kutekeleza majukumu ya kuimarisha taasisi na mifumo, hasa katika wakati huu ambapo CHADEMA inaendelea kutimiza wajibu mkubwa kwa wanachama wake na Watanzania wote kwa ujumla.

Pamoja na kwamba propaganda hizo nyingi zinapuuzwa, si kila upuuzi unaweza kupuuzwa. Mathalani zimeenezwa habari za uongo kuwa Mbunge wa Karatu, Mchungaji Israel Natse amekuwa Makamu Mwenyekiti Bara, Mbunge wa Iringa Mjini na Mjumbe wa Kamati Kuu, Peter Msigwa ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Bara na Prof. Mwesiga Baregu, amejiuzulu nafasi yake ya ujumbe wa Kamati Kuu.

Kwa mtu makini, ukisikia na kuzisoma propaganda hizo katikati ya maneno kama si mistari, mara moja unang'amua zinalenga kitu gani. Kwa sasa si lazima kuingia undani wa malengo hayo, lakini ni vyema ikajulikana kuwa yanajulikana tayari. Hazitafuzu.

Tunatambua kuwepo kwa watu wa CCM, wakiwemo viongozi wa juu kabisa wa chama hicho, wanaoonekana eti 'wanaipenda' CHADEMA leo ghafla, wanahusika katika kueneza uongo na propaganda hizo. Bila shaka ni dalili ya kushindwa kushughulika na mambo yao (ufisadi, kujivua gamba, kukataliwa na wananchi, n.k), kiasi wanapata muda wa 'kujali' ya wengine.

Tunajua wanatishika na namna ambavyo CHADEMA inaendelea kujiimarisha (huku wao wakizidi kukataliwa), kupitia CHADEMA ni msingi na Operesheni ya M4C, kupitia kanda za chama na kazi nyingine zinazeondelea yakiwemo mafunzo kwa viongozi.

Wanachama makini wa CHADEMA na Watanzania kwa ujumla wanaoamini kwa dhati katika mapambano ya mabadiliko ambayo chama hiki kimeyasimamia consistently, bila kuyumba, kikionesha kila sifa ya kuwa mbadala wa status quo ya CCM, wataendelea kusikiliza chama chao kinasema nini (hasa kupitia maamuzi ya vikao), kuhakikisha nguvu ya mshikamano wa pamoja inaendelea kuwa ndiyo nguzo imara ya mafanikio kwa ajili ya haki nha matumaini ya Watanzania.

Propaganda za hivi sasa, kama ambavyo zimeshindwa zote zingine, hazitawaondoa katika mstari wanachama na Watanzania wenye matumaini makubwa na CHADEMA kuwa ni chama mbadala chenye kujenga uongozi bora, sera sahihi, mikakati makini na oganaizesehni tahibiti, mijini na vijijini kwa ajili ya kutoa utumishi bora kwa wananchi.

Makene

0752 691569