Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Friday, November 1, 2013

Diwani CHADEMA afariki dunia

 
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Wilaya ya Bunda kimepata pigo la kuondokewa na Diwani wake wa Kata ya Nyasura, Zamberi Mwisarya (68).
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Kaimu Katibu wa CHADEMA wilayani hapa, Samweli Alfred, alisema kuwa diwani huyo alifariki dunia juzi saa mbili usiku katika Hospitali ya Bugando jijini Mwanza alikokuwa amelazwa.
Alisema kuwa wamepokea kwa masikitiko makubwa msiba huo na kwamba wameondokewa na kiongozi shupavu ambaye alikuwa akitetea wananchi wa Kata ya Nyasura na kwamba chama kimeondokewa na mpiganaji wa kweli.
Naye Katibu Mwenezi wa kata hiyo, Benjamin Kasonde, alisema kuwa wananchi wa kata hiyo walikuwa wakimtegemea sana diwani wao katika mambo mbalimbali na kwamba alikuwa ni mtetezi wao katika masuala mbalimbali ya maendeleo.
Mtoto wa marehemu, Mgendi Ngabayi, alisema kuwa baba yake alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kiharusi tangu mwaka jana na kupelekwa Bugando kwa matibabu kisha alipata nafuu lakini baadaye mwaka huu hali yake ilirudia kuwa mbaya, hivyo waliamua kumrudisha huko tena kwa matibabu hadi juzi alipokutwa na mauti.
Alisema kuwa mazishi yalitarajiwa kufanyika jana katika makaburi ya Nyasura saa kumi jioni.
Naye Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Joseph Marimbe, alisema kuwa ameshutushwa na msiba huo kwani diwani huyo alikuwa ni mmoja wa madiwani mashuhuri na kwamba halmashauri imepoteza mmoja wa madiwani wake.

No comments:

Post a Comment