Pages

Wednesday, November 6, 2013

Ester Bulaya awasilisha maelezo bungeni kuhusu dawa za kulevya

Bulaya_akitoa_maoni_e4f00.jpg
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ester Bulaya, amewasilisha bungeni maelezo binafsi akiitaka serikali pamoja na mambo mengine, kufanya mabadiliko ya sheria ya dawa za kulevya na kuanzisha mahakama maalumu ya kushughulikia wahalifu wa dawa hizo. Aliwasilisha maelezo hayo chini ya kanuni ya 28 (8) ya Bunge toleo la mwaka 2013, kuhusu tatizo sugu la uagizaji, uuzaji na usafirishaji wa dawa hizo linaloongezeka kwa kasi kubwa nchini kwa lengo la kuitaka serikali ichukue hatua hizo.
Alisema ameona ni wakati mwafaka kutoa maelezo hayo, ili Bunge na serikali ipate fursa ya kuona uzito wa tatizo la dawa za kulevya kutokana na ukweli kwamba katika miaka ya karibuni tatizo hilo limeongezeka kwa kasi ya ajabu hali inayosababisha athari kubwa za kiuchumi, kijamii na kiafya nchini, huku kundi kubwa linaloathirika likiwa la vijana.
Bulaya alisema tafiti za hivi karibuni za Umoja wa Mataifa (UN) zinaonyesha kuwa kuna ongezeko kubwa na la kutisha katika matumizi ya dawa hizo aina ya heroin na kwa njia ya kujidunga katika nchi za Kenya, Libya, Mauritius, Shelisheli na Tanzania.
Pia alisema ripoti mpya ya hivi karibuni ya ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Mihadarati na Uhalifu (UNODC) imetamka bayana kwamba Tanzania ni kinara wa kupitisha dawa hizo katika nchi za Afrika Mashariki, na Mkoa wa Tanga ukitajwa kama wa hatari zaidi.
Hivyo, ameitaka serikali kuunda Mahakama Maalumu haraka iwezekanavyo itakayokuwa na jukumu la kushughulikia kesi za dawa hizo tu kama ilivyo Mahakama ya Biashara na iliyokuwa Mahakama ya Ardhi na kufanya marekebisho ya sheria ya hizo kwa kuongeza makosa ya kusafirisha, kuuza au kukutwa na kemikali bashirifu
Pia iundwe Tume ya kuchunguza baadhi ya watendaji wa mahakama na serikali, ambao kwa makusudi wamekuwa wakihujumu kesi za dawa hizo pamoja na jitihada za serikali katika kupambana na biashara hiyo haramu na kuleta taarifa katika bungeni.
Pia ametaka kiundwe haraka chombo huru chenye nguvu na mamlaka kamili kitakachokuwa na dhamana ya kupambana na dawa za kulevya nchini.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment