Rais wa TFF, Jamal Malinzi leo amekabidhiwa rasmi ofisi
tayari kwa kuanza kutekeleza ilani yake iliyompa ushindi kwenye uchaguzi mkuu
uliofanyika Oktoba 27 na kutangazwa mshindi alfajiri ya Oktoba 28
TANZANIA FOOTBALL FEDERATION
Ndugu mgeni rasmi ……..…………………………………………….
Ndugu…………………………………. Mwakilishi wa Wizara
Ndugu…………………………………. Mwakilishi wa BMT
Ndugu…………………………………. Mwakilishi wa wadhamini
Ndugu Leodegar Tenga
Rais aliyemaliza muda wake
Ndugu Said El
Maamry Mwenyekiti
mstaafu wa iliyokuwa FAT
Ndugu Muhidin Ndolanga
Mwenyekiti
mstaafu wa
iliyokuwa FAT
Wajumbe wa Baraza la Wadhamini
Wajumbe wa Kamati ya Utendaji
Wafanyakazi wa TFF
Wageni waalikwa
Mabibi na Mabwana
Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa
kutuwezesha kuwa hapa leo.
Awali ya yote naomba nichukue fursa hii kukupongeza
Rais wetu uliyemaliza muda wako Ndugu Leodegar Tenga na Kamati yako ya
utendaji . Mliyoufanyia mpira wa Tanzania ni makubwa, historia haitawasahau.
Mmetujengea taasisi imara isiyotetereka, taasisi inayoheshimika ndani na nje ya
mipaka ya nchi hii, nawashukuru na kuwapongeza sana.
Uchaguzi umekwisha. Mchakato ulikuwa mrefu. Wapo
walioshinda na wapo ambao kura zao hazikutosha. Wote tuna kazi moja tu kujenga
mpira. Kama tulikwaruzana kwenye kampeni tusameheane, tuwe kitu kimoja,
tuinyanyue soka yetu. Makundi hayajengi yanabomoa, tuachane nayo.
Ndugu zangu, uongozi wetu ulioingia madarakani alfajiri ya
tarehe 28-10-2013 unakabiliwa na changamoto nyingi. Nitaelezea changamoto
chache zinazohitaji ufumbuzi wa haraka.
Mashindano yanayotukabili.
Tunakabiliwa na mashindano mbalimbali ya kimataifa. Mfano
ni mechi ya marudiano ya U/20 wanawake dhidi ya Msumbiji wiki ijayo, Mitoano ya
mashindano ya Afrika wanawake mapema mwakani, Mashindano ya Chalenji Novemba
mwaka huu, na mashindano ya kufuzu AFCON 2015. Yote haya yanahitaji maandalizi
ya haraka.
Programu ya vijana.
Ilani yangu ya uchaguzi ilielezea azma ya Tanzania kuomba
uenyeji wa fainali za vijana za Afrika U/17 mwaka 2019. Jambo hili
tutalizungumzia kwenye kikao chetu cha utendaji leo. Ili tuwe na timu nzuri ya
kucheza fainali hizo tukiwa wenyeji hatuna budi mwaka kesho kuunda timu ya
Taifa ya U/12 itakayokua pamoja kuelekea 2019. Programu yetu ya vijana
tutakayoiandaa sharti ijielekeze kwenye ratiba hii.
Udhamini wa timu za vijana na za wanawake
Hii ni changamoto kubwa sana kwa TFF. Timu zetu za Taifa
kuanzia zile za wakubwa hadi za vijana ni brands, na kama ni brands inabidi
ziingizwe sokoni, ziuzwe kwa tunaodhamiria wawe wadhamini wa hizo timu. Kitengo
cha masoko lazima kiimarishwe ili kukabiliana na changamoto hizi. Mdhamini ni
mfanyabiashara, anapotoa pesa kudhamini brand fulani anategemea matokeo mazuri
kwake kwa njia ya kukuza biashara zake. Twende kwa wadhamini tuwashawishi waone
watafaidikia nini (leverage) kwa kudhamini timu zetu. Tusisubiri waje tuwafuate
sisi.
Uwekezaji
Jitihada za haraka lazima zifanyike kuiongezea TFF uwezo
wa kiuchumi. Ni muhimu mtaalam mshauri (consultant) atafutwe atufanyie
mchanganuo wa uwekezaji katika ardhi yetu hii ya Karume ili tuwekeze kitega
uchumi kama ilivyokubaliwa kwenye mkutano mkuu. Aidha bidhaa zenye nembo yetu
zianze kuuzwa kwa utaratibu maalum ili shirikisho lipate haki yake.
Kabla sijamaliza kuzungumza, niongelee suala la fujo
viwanjani. Mpira ni dakika tisini. Katika kipindi hicho uamuzi wa mwamuzi
unakuwa ni wa mwisho. Tusifiche upungufu wa timu zetu kwa kujificha nyuma ya
kivuli cha mwamuzi. Waamuzi wakionekana wamefanya makosa yawe ya makusudi au ya
bahati mbaya vyombo vya kuwahukumu vipo, mahakama ya waamuzi sio mashabiki.
Kitendo cha mashabiki kufanya fujo kabla, wakati na baada ya mechi ya mpira
kamwe hakikubaliki mahali popote duniani. Kanuni za FIFA, CAF na TFF ziko
wazi na adhabu zinajulikana. Moja ya adhabu hizi ni timu husika kucheza kwenye
uwanja mtupu usio na mashabiki kama ilivyowatokea Al Ahly na Zamalek huko Misri
au kucheza nje ya uwanja wako kama ilivyowatokea Senegal ambao baada ya vurugu
Dakar, Senegal waliamriwa na FIFA mechi zao za nyumbani wachezee nje ya nchi na
wakachagua kuchezea Morocco.
Ndugu zangu yaliyotokea majuzi Mbeya na Dar es salaam wote
tumeyasikia na wengine miongoni mwetu hapa ni mashuhuda. Ninasema iwe mara ya
kwanza na y a mwisho. Kwenye masuala ya kutekeleza mahitaji ya kanuni uongozi
wangu hautaionea haya klabu yoyote, iwe mpya au kongwe kwenye ligi yetu. Ni
jukumu la viongozi wa klabu kudhibiti wanachama na wapenzi wao. Tabia ya benchi
la ufundi kutoa matamshi yanayoweza kuamsha hisia za mashabiki ni kinyume na
taratibu na kanuni ziko wazi kuhusu jambo hili. Viongozi wa klabu na mabenchi
yao ya ufundi wakishindwa kutekeleza wajibu wao tusilaumiane.
Ndugu zangu ya kufanya ni mengi katika kuiendeleza soka
yetu. Tunashukuru Mungu kuwa uwezo wa kukabiliana na changamoto hizi tunao na
tuna ari na nia ya kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya mpira. Ombi langu
kwenu nyote ninaomba ushirikiano wa wadau wote kuanzia Serikali, Halmashauri,
mashirika ya umma na binafsi na NGO’s, nina imani tukishikamana tutaifikia
ndoto yetu ya kuing’arisha Tanzania kimpira kwenye anga za dunia.
Ahsanteni nawashukuru sana.
No comments:
Post a Comment