Ripoti
mpya ya utafiti imebainisha kuwa mishahara mikubwa wanayolipwa viongozi
wa juu serikalini na wanasiasa hailingani na utendaji wao wa kazi.
Ripoti
hiyo iliyozinduliwa jana jijini Dar es Salaam, imeeleza kuwa viongozi
hao wanalipwa mishahara inayotofautiana kwa kiwango kikubwa na pato la
mwananchi wa kawaida.
Huku
ikitaja mapato ya mishahara ya marais wa baadhi ya nchi za Afrika
Mashariki ikiwamo Tanzania, imesema kuwa hali hiyo ni kuibebesha jamii
mzigo wa kugharimia malipo ya viongozi.
Akizindua
ripoti hiyo iliyochunguza gharama za kuwalipa viongozi wa Serikali na
wanasiasa, Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti kuhusu Kuondoa Umaskini
(Repoa), Dk Theodore Valentine, alisema kuwa viongozi wa Afrika
Mashariki ndio wanaoongoza kwa kulipwa mishahara mikubwa zaidi chini ya
Jangwa la Sahara.
"Kama
viongozi wakuu watakuwa wanalipwa mishahara mikubwa, nchi za Kusini mwa
Jangwa la Sahara zitaweza kugharimia demokrasia?" alihoji Valentine.
Utafiti
huo uliofanyika kati ya mwaka 2009 na 2012, umebainisha kuwa Rais wa
Tanzania analipwa mshahara dola 172,014 kwa mwaka (Sh275 milioni) sawa
na Sh22.9 milioni kwa mwezi, huku Rais wa Kenya, akiongoza kwa kulipwa
dola 515,021 kwa mwaka (Sh824 milioni) kwa mwaka sawa na Sh68.6 milioni
kwa mwezi.
Rais wa
Rwanda analipwa dola 199,000 kwa mwaka (Sh124 milioni) sawa na Sh10
milioni kwa mwezi, wakati rais wa Nigeria akipokea dola 161,902 (Sh259
milioni) ambazo ni sawa na Sh21 milioni kwa mwezi.
Pia
umeeleza kuwa Rais wa Kenya analipwa mara 320 zaidi ya pato la mwananchi
wa kawaida wa nchi hiyo, wakati rais wa Afrika Kusini anapata mara 46
na Rwanda mara 150 zaidi ya mwananchi wa kawaida.
Ripoti
hiyo imeendelea kubainisha kuwa rais wa Tanzania analipwa mara 8.2 ya
mshahara wa hakimu, huku rais wa Kenya akipokea mara 13.1 na kumpita
rais wa Rwanda anayechukua mara 12 zaidi ya mshahara wa hakimu.
Kwa
upande wa wabunge, utafiti huo umeeleza kuwa wabunge wa Tanzania
wanalipwa mara 3.0 ya mshahara anaolipwa hakimu, Kenya (5.5) na Rwanda
(3.0). Viwango hivyo vimetajwa kuwa vikubwa kuliko vya wabunge wa
Nigeria na Afrika Kusini.
Naibu Spika anena
Naye
Naibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Job Ndugai alisema kuwa umefika
wakati ambapo mishahara ya viongozi wa umma inabidi iwekwe wazi kwa
wananchi.
"Ningependa mishahara ifahamike kama ilivyo kwa nchi nyingine, hii itaondoa uongo kwa wabunge," alisema.
Alisema
mishahara wanayolipwa wabunge siyo mikubwa na kwamba inapaswa kuongezwa
zaidi kwa kuwa hivi sasa imetofautiana kidogo na ya wakuu wa wilaya.
"Mshahara
wangu mimi kama Naibu Spika ni mdogo..., hata wa Waziri Mkuu siyo
mkubwa. Siku zote mtu anapoongezewa mshahara inamwongezea motisha ya
kufanya kazi," alisema Ndugai.
Serikali yajibu
Naibu
Waziri wa Kazi na Ajira, Dk Makongoro Mahanga, alisema viongozi
wanalipwa mshahara kutokana na nyadhifa walizonazo, hivyo haoni sababu
ya jambo hilo kujadiliwa.
Alisema
mshahara ni siri ya mfanyakazi husika, na kwamba iwapo itawekwa wazi
baadhi ya watu wataacha kujadili mambo ya maendeleo na badala yake
wataanza kuzungumzia malipo hayo.
"Tujadili kuhusu namna ambavyo gesi itatuletea maendeleo kwenye uchumi wa nchi yetu na siyo mishahara," alisema.
Alipopigiwa
simu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia, alihoji kuwa anazungumza na nani,
mwandishi alipojitambulisha alitaka apewe muda hadi baadaye kwa madai
kuwa hakuwa sehemu nzuri.
Rais Kikwete na OGP
Akinukuliwa
na gazeti la Serikali, Rais Jakaya Kikwete, ambaye Oktoba 31 hadi
Novemba Mosi 2013, alihudhuria Mpango wa Pamoja wa Uendeshaji wa
Serikali kwa Uwazi (OGP) uliofanyika London, Uingereza, ambapo
alizungumzia uwazi kwenye Serikali yake likiwemo suala la mishahara.
Mkutano
huo ulihudhuriwa na washiriki 1,000 kutoka nchi 60 wanachama na Rais
Kikwete alipata nafasi ya kuuelezea mkutano huo, namna Tanzania
ilivyoanza utekelezaji wa masharti ya mpango huo.
Rais Kikwete alisema kuwa mshahara wa mtumishi wa umma hauwezi kuwa siri na ndiyo maana unawekwa katika bajeti ya serikali.
"Mishahara
haiwezi kuwa siri. Si ipo kwenye bajeti za Serikali?" Alijibu Rais
Kikwete alipoulizwa kama suala la mishahara litaendelea kuwa siri katika
utekelezaji wa mpango huo.
Rais
Kikwete alisema: "Changamoto iliyopo ni kwamba mpango huu unabadili
mazoea yetu ya kufanya kazi. Sisi katika kila Serikali kila kitu
kilikuwa siri. Sasa OGP inataka mambo haya yawe wazi, ifike hatua mtu
aone kutoa habari ni wajibu."
TUCTA yatoa kauli
Katibu
Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Nicolas Mgaya
alisema wabunge wanalipwa mishahara mikubwa lakini baadhi yao
hawaonekani kwenye vikao.
Alitaka mishahara yao iwekwe wazi kwa wananchi kwa kile alichokieleza kuwa kwa sababu wanalipwa kwa kutumia kodi za wananchi.
Anavyosema Profesa Wangwe
Akizungumzia
matokeo ya utafiti huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Repoa, Profesa Samuel
Wangwe alisema kuna haja ya kuangalia gharama za kuwalipia viongozi.
"Tuangalie
gharama ya demokrasia, lakini jambo la msingi ni kuwa kama wabunge
wanalipwa kiasi kinachotajwa basi wafanye kazi yao wanayostahili na
wasisahau kwamba wanawawakilisha wananchi ambao ni maskini," alisema.
Profesa Lipumba
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi - CUF, Profesa Ibrahim
Lipumba, ambaye ni mchumi kitaaluma alisema kuwa hakuna ushahidi
unaoonyesha kuwa viongozi wakilipwa mishahara mikubwa wanafanya kazi
zaidi.
"Hakuna ushahidi wowote kwamba kwa kuwalipa wabunge mishahara mikubwa basi wanafanya kazi vizuri zaidi," alisema.
Akitolea
mfano wabunge wa Kenya alisema: "Katika kipindi cha miaka mitano mbunge
wa Kenya analipwa dola za Marekani dola 1milioni (sawa wa Sh1.6 bilioni)
kiasi ambacho ni sawa na Sh26 milioni kwa mwezi."
Aliongeza kuwa mishahara ya wabunge wa Tanzania ni zaidi ya mara 40 ya pato la kawaida la mwananchi.
Alipendekeza
kuanzishwa kwa taasisi ambayo itapewa jukumu la kusimamia mapato ya
viongozi wa umma, na kwamba ni vyema katiba izungumze kuwa mishahara na
marupurupu ya wabunge itapangwa na taasisi ambayo ipo huru
itakayozingatia mapato ya nchi yalivyo.
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment