ALIYEKUWA golikipa namba moja wa Simba na timu ya
taifa ya Tanzania Taifa Stars, Juma Kaseja amesema anasubiri kupewa fedha
walizokubaliana na Yanga ili asaini kuichezea klabu hiyo.
Kaseja amesema tayari amefanya mazungumzo na klabu
hiyo ya Yanga ambayo aliwahi kuitumikia kwa msimu mmoja 2008/2009 kabla ya
kurejea Simba msimu uliofuata na kuipa ubingwa wa rekodi ya bila kufungwa hata
mchezo mmoja wakipata sare mbili chini ya kocha raia wa Zambia Patrick Phiri.
Kipa huyo ambaye alimaliza mkataba na Simba na klabu
hiyo kukataa kumuongeza mkataba mwingine amesema wamekubaliana na Yanga kila
alichohitaji na anachosubiri ni klabu hiyo kumpatia fedha walizokubaliana ili
asaini mkataba.
"Bado sijasaini Yanga lakini kweli nimefanya
nao mazungumzo na makubaliano yote tumeafikiana lakini nitasaini baada ya
kupewa fedha tuliyokubaliana,wakinipa fedha hata leo nasaini"alisema
Kaseja.
Kipa huyo maarufu kwa uhodari wake langoni anasema
mpira ndio kazi yake kwahiyo anaweza kucheza kwenye klabu yoyote inayomuhitaji
na kufikia naye makubaliano na ndio maana hata Yanga walipomfuata amekaa nao na
kufikia makubaliano yanayosubiri kutia saini mkataba.
Akiwa Yanga msimu wa 2008/2009 Kaseja aliandika rekodi
ya kuwa kipa aliyefunga goli katika mchezo wa ligi kuu, akitumbukia wavuni
kwenye mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa CCM Kirumba Yanga walipocheza dhidi ya
Toto Africans ambao kwasasa wapo ligi daraja la kwanza.
Baada ya kumaliza mkataba wake na Simba Juni mwaka huu klabu ya FC Lupopo ya Congo DRC ilijaribu kumsajili lakini mpango huo ukashindwa kukamilika baada ya kutokea matatizo kadhaa ikiwemo kukamatwa kwa wakala aliyekuwa akishughulikia mpango huo huku mkataba nao ukiwa umetumwa kwa lugha ya kifaransa.
No comments:
Post a Comment